Advertisements

Wednesday, September 10, 2014

SHOGA, HUWEZI KUITENGANISHA SHUKA KWA MANENO

Hehehe.. heeeeee, heiiiya, acha nicheke miye mtoto wa marehemu sijui wazazi wangu huko walipo wapo katika hali gani. Waweza ukaona nacheka kwa furaha, la hasha, kuna watu wengine kwa kweli kila kitu watende wao wakitenda wenzao huwa mwao.

Hivi kweli inaingia akilini wewe mama mtu mzima kutaka kuongoza ndoa ya mwanao wa kike au wa kiume pengine ndoa yako ilikushinda sasa unataka kubomoa za wenzako.

Nalisema hili kwenu wote wenye tabia hii, huu ndiyo muarobaini, uchungu ndiyo ladha yake lakini dawa. Nayasema haya kutokana na shoga yangu mmoja kunijia mikono kichwani nikijua labda kafiwa. Alipofika kwangu alichonieleza nilibakia mdomo wazi nisijue nimjibu nini kwa wakati ule.

Eti mwanaye amekuwa akiendeshwa na mkewe kama gari bovu, mkwewe wa kike amekuwa mama huruma jamvi la mtaani kila mwanaume kwake sawa. Kila akimwambia mwanaye, amekuwa haoni wala hasikii juu ya yule mwanamke. Na siku ile ndiyo mwanaye kampa makavu, kuwa hawezi kuachana na mkewe.


Mmh! Makubwa limao alambe mwingine wewe ukunje uso kama ngozi ya goti, leo nataka niwaeleze ninyi kinamama mnaokosa kazi kufuatilia ndoa za watoto wenu.

Jamani mbona aibu mama mkwe kuacha kazi zake kufuatilia ndoa ya mtoto wake, kwanza matusi kwa mila zetu mama mkwe kufuatilia nyendo za mkwewe kila kona kumfuatilia kama mkia.

Sawa umeona lakini mwanao hajaona pengine akitoka kwenda kazini huku nyuma mkeo anatoka, kwa vile huna kazi unamfuatilia na jioni akija mwanao unampa full data. Cha ajabu mwanao haoneshi chochote kutokana na shutuma hizo.

Unajua ni jambo la kushangaza kwa mtu aliyedumu kwenye ndoa yake kufanya ujinga kama huu. Wapo walioachika kwa kukosa uaminifu katika ndoa zao na leo ndiyo haohao waliokosa uso wa haya kufuatilia maisha ya mkwewe kisha kumpelekea mwanaye.

Akikataa unataka kumtolea radhi, mmh! Wewe nani alikutolea radhi mbona yako mengi tunayajua, ikiwemo kumbambikia mumeo mtoto si wake. Mbona sisi tumekaa kimya kwa kuelewa ndoa ni siri ya watu wawili. Na kila lenye mwanzo lina mwisho wake, kwanini uingie uchawi kwa jambo ambalo leo na kesho huyo asiye na macho hutoa hukumu bila kulaumu mwisho wa safari.

Unataka waachane unajua mwanao anapewa nini na mkewe kiasi cha kuchanganyikiwa, hebu tuziache ndoa za watoto wetu hata ninyi kama mngefuatiliwa hivyo sidhani kama mngefika mlipo.

Acheni kukumbatia kila kitu, yenuyenu ya wenzenu yenu lakini kwa hili la shuka moja, kazi kwenu huwezi kuitenganisha shuka moja kwa maneno tu. Kwa mtaji huo mtalia sana na laana zetu zitawarudia wenyewe.

Yangu nimemaliza mwenye kukasirika akasirike lakini ziacheni nyumba za watoto wenu, ndoa ina misukosuko mingi na si kuishi kwa umbea wa watu wote waliofuata umbea leo wanajuta.
Na ninyi mawifi mnataka mke wa kaka yenu aachike mkifanyiwa ninyi kwenye ndoa zenu mtafurahi? Tafakari kisha chukua hatua.

Yangu ni hayo ni mimi Anti yenu Nasra Shangingi Mstaafu.

GPL

No comments: