Advertisements

Friday, October 10, 2014

AMEKUSALITI, LAKINI BADO UNAMPENDA?-2

Ni wiki nyingine tena tunapokutana katika uwanja wetu huu mzuri wa kuzungumzia ishu za uhusiano wa kimapenzi. Wiki iliyopita niliiweka mada mezani juu ya nini cha kufanya inapotokea mwenzi wako amekusaliti ingawa ndani ya moyo wako bado unampenda sana.

Inaonekana mada imewagusa wengi kwani nimepokea maoni kwa wingi, kila mmoja akieleza kwa uzoefu wake namna ya kushughulikia tatizo hili. Nakushukuru wewe uliyeshiriki kuchangia mada kwa kutuma ujumbe mfupi na kutoa mawazo yako kuhusu mada hii inayowatesa wengi.
Mawazo yalikuwa ya pande mbili, wapo ambao wameendelea kushikilia msimamo kwamba hakuna msamaha kwa mtu anayesaliti kwenye mapenzi.

Hata hivyo, wengi wameshauri kwamba inawezekana kabisa kuendelea na uhusiano hata baada ya mwenzi wako kukusaliti, cha msingi ni kuusikiliza moyo wako na kumpima mwenzi wako kama amelijua kosa lake na analijutia.

Nauheshimu mchango wa kila mmoja alioutoa na nawapa pole wote ambao wamenisimulia jinsi walivyoumia ndani ya mioyo yao baada ya kugundua kuwa wanasalitiwa na watu wanaowapenda sana. Tuendelee na mada yetu kuanzia pale tulipoishia wiki iliyopita.

NINI CHA KUFANYA UNAPOSALITIWA?

1. JIPE MUDA WA KUTAFAKARI
Sote tunakubaliana kwamba hakuna kipindi kigumu kwenye mapenzi kama unapogundua kuwa mwenzi wako amekusaliti. Ni katika kipindi hiki mtu anaweza kujidhuru mwenyewe, kumdhuru mwenzi wake au mwizi wake.

Hata hivyo, wataalamu wa mapenzi wanaeleza kwamba hatua ya kwanza na ya haraka ambayo unatakiwa kuichukua baada ya kugundua kuwa mwenzi wako amekusaliti, ni kujipa muda wa kutafakari kwa kina kuhusu kilichotokea.

Tafuta sehemu tulivu, kaa ukiwa peke yako na tafakari kwa kina juu ya kilichotokea. Anza kwa kujichunguza mwenyewe kwani yawezekana umesababisha mwenzi wako akusaliti.
Maamuzi ya busara hayafanywi ukiwa na hasira, ukijipa muda wa kutafakari utagundua kilichosababisha akusaliti.

2. USIKILIZE MOYO WAKO
Jiulize ndani ya moyo wako kwamba licha ya yote yaliyotokea, bado unamhitaji mwenzi wako na upo tayari kumsamehe? Uzuri wa mapenzi, moyo ndiyo huzungumza ukweli, kama humhitaji tena, chukua uamuzi wa kuachana naye lakini kama bado unampenda, mpe nafasi ya pili.
Epuka kuchukua uamuzi kwa hasira kwa sababu unaweza kuamua kumuacha wakati moyo wako bado unamhitaji baadaye ukaja kujuta. Yafikirie mambo mazuri mliyowahi kuyafanya pamoja kisha yapime.

3. ZUNGUMZA NAYE
Ukishakuwa umezifanyia kazi hatua hizo mbili za hapo juu, tafuta muda wa kuzungumza na mpenzi wako na muulize kwa upole kwa nini amekusaliti. Mpe muda wa kujieleza na msikilize kwa umakini.
Ikiwa anaonesha kujutia makosa aliyoyafanya na akakuomba msamaha kutoka ndani ya moyo wake na kuahidi kutorudia tena, mpe nafasi ya pili. Ukiamua kumsamehe, kweli umsamehe na usibaki na kinyongo ndani ya moyo wako.

4. WASHIRIKISHE WATU UNAOWAAMINI
Yawezekana ukahisi umekosewa sana kuliko mtu mwingine yeyote lakini ukijaribu kuzungumza na watu unaowaamini, ushuhuda wao utakusaidia kuona kila kilichotokea kuwa ni cha kawaida.
Kama ndoa yenu ni changa, jaribu kuzungumza na watu walioishi kwenye ndoa kwa muda mrefu na utashangaa kugundua kuwa wengi walishawahi kusalitiwa lakini wakawasamehe wenzi wao na maisha yakaendelea.

Ni matumaini yangu kuwa mbinu hizo zitakusaidia kukabiliana na hali hiyo ngumu na utampenda tena pengine zaidi ya ulivyokuwa unampenda mwanzo.

GPL

No comments: