Advertisements

Tuesday, October 21, 2014

ANASWA AKIMTEKA MTOTO WA SHULE

Denti wa Shule ya Msingi Mwalimu Nyerere, Magomeni (mwenye sare za shule) aliyenusurika kutekwa na njemba inayotambuliwa kwa jina moja la Omar.

Stori: Waandishi Wetu
HALI bado tete! Polisi wa Kituo cha Magomeni jijini Dar, wamemkamata baba mmoja aliyetambuliwa kwa jina moja la Omar baada ya kupokea kipigo ‘hevi’ kutoka kwa raia wenye hasira kali akihusishwa na utekaji wa denti wa Shule ya Msingi Mwalimu Nyerere iliyopo maeneo hayo.

Tukio hilo lililokusanya kadamnasi lilijiri wikiendi iliyopita, Magomeni-Kagera, Dar wakati mwanafunzi huyo akitokea shuleni.Kwa mujibu wa mashuhuda, denti huyo alipofika eneo hilo, baba huyo alimsalimia na baada ya kujibiwa salamu yake alianza kumchombeza kwa maneno matamu-tamu

Akizungumza na Uwazi lililofika eneo la tukio ndani ya ‘dakika sifuri’, denti huyo aitwaye Laila alisema licha ya kuitikia salamu ya jibaba huyo na kumuamkia bado aliendelea kumchombeza na kila alipojaribu kumkwepa ilishindikana.

Njemba huyo alivuka mipaka na kumshika mkono na kutaka kumvutia ndani ya gari lililokuwa karibu yake ndipo Laila alipoamua kupiga mayowe ya kuomba msaada na hatimaye kuokolewa na wasamaria wema waliokuwa wakipita njia.”

Mwanafunzi huyo aliendelea kusema: “Alianza kunifuatilia tangu kule, akanisalimia hujambo nikamjibu sijambo, akaniambia tena kwenu hawajambo, nikamjibu hawajambo, akaendelea kuniambia eti, nimfuate akanipe lambalamba, mimi nikakataa kwa sababu mama alinikataza kukubali kupewa lifti na vitu vingine kutoka kwa watu nisiowajua tangu aliposikia habari za watoto kutekwa na Noah nyeusi.

“Kila kitu nilimkatalia lakini yeye akawa anaendelea kuniambia maneno yake na kuanza kunivuta ndipo nikaona sasa naenda kufa hivyo ikanibidi nipige kelele ndiyo watu wakatokea na kumkamata kisha kuanza kumpiga mpaka walipofika polisi.”

Gazeti hili lilizungumza na mtuhumiwa aliyekuwa amehifadhiwa ndani ya gari, alipoulizwa kuhusiana na tuhuma hizo alimuomba paparazi wetu kabla ya yote kwanza amuokoe na kifo kutoka kwa wananchi wenye hasira kali.

“Chondechonde ndugu yangu, naomba kwanza mnilindie usalama wangu, hao jamaa wanataka kuniua bila sababu, mimi wala sikuwa na nia mbaya na huyo binti wananizushia tu, nilikuwa namsalimia tu,” alisema Omar kupitia upenyo mdogo wa juu ya dirisha la gari alilohifadhiwa.

Imeandaliwa: Richard Bukos, Deogratius Mongela na Chande Abdallah wa GPL

No comments: