Dodoma. Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), Jaji Damian Lubuva amesema mpango wa vyama vya siasa vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) wa kusimamisha mgombea mmoja katika Uchaguzi Mkuu mwakani ni halali kisheria.
Vyama vinavyounda Ukawa ni NCCR-Mageuzi, CUF, Chadema na NLD.
Jaji Lubuva alisema hayo jana mjini Dodoma katika semina ya siku mbili ya Baraza la Vyama vya Siasa Tanzania ya kuwahamasisha wadau wa siasa kudumisha amani na utulivu ambayo ilihudhuriwa na vyama vyote vyenye usajili wa kudumu nchini isipokuwa Chadema na CUF.
“Wanaposema katika wilaya fulani wanasimamisha mgombea wa chama fulani hawaundi chama, ni kwamba pale wanaachia chama fulani, wanakiunga mkono kwa hivyo hapo sheria inaruhusu kabisa,” alisema Jaji Lubuva na kuongeza:
“Nadhani huo ndiyo ukweli wao siyo lazima waende wakaandikishe chama. Wanasema chama X kule Iringa tunamsimamisha fulani na wengine wanamuunga mkono, hilo si tatizo.”
Jaji Lubuva alisema hayo baada ya Mwenyekiti wa Baraza hilo, Peter Mziray kusema sheria hairuhusu Ukawa kuungana.
“Hawa wanataka kuvunja sheria... wanawaambia uongo Watanzania kwamba watasimamisha mgombea mmoja katika uchaguzi,” alisema Mziray ambaye pia ni Rais Mtendaji wa Chama cha APPT Maendeleo na kuwataka wanasiasa kufuata sheria za nchi ili kuepuka machafuko nchini.
Akichangia katika mkutano huo, Katibu Mkuu wa NCCR- Mageuzi, Mosena Nyambabe alisema kitabu cha maadili ya vyama katika uchaguzi kinaruhusu vyama kushirikiana na ndiyo sababu walipokuwa wanazunguka nchini, chama kimoja katika umoja huo ndicho kilikuwa kikiomba kibali cha kufanya mkutano.
Amani na Utulivu
Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Philip Mangula alisema uvunjifu wa amani katika uchaguzi unachangiwa na tofauti kubwa za kimapato. Alisema jinsi pengo kati ya maskini na tajiri linavyozidi kuwepo, amani haiwezi kuwepo.
Akifungua semina hiyo, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Asha - Rose Migiro, alivitaka vyama vya siasa nchini kufahamu kuwa kujenga amani na utulivu ni lengo lao la kudumu.
Profesa wa Chuo Kikuu cha Ruaha, Gaudence Mpangala alisema yapo mambo matatu; ujenzi wa demokrasia kitaifa, ushiriki wa jamii katika siasa, uchumi na maendeleo ya jamii ambayo yanatakiwa kufuatwa ili kudumisha amani na utulivu.
Mwanasiasa mkongwe, Getrude Mongella alisema nchi imefika mahali mtu anatoa matamshi ya uvunjifu wa amani lakini hachukuliwi hatua.
Makamu Mwenyekiti wa UDP, Issack Cheyo alivishutumu vyama vikubwa vya siasa kwa kuwa vyanzo kuvunja makubaliano ya maadili ya uchaguzi... “Tulikubaliana kuwepo kwa nafasi sawa katika kutangaza sera kwenye vyombo vya habari lakini chama kimoja kinapewa nafasi kubwa katika vyombo vya habari.”
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment