ANGALIA LIVE NEWS

Monday, October 6, 2014

ANKO TENGA, TAFADHARI RUDI, KAKA MALINZI AMEFELI

Na Saleh Ally
USISHANGAZWE nami kuamua kujaribu kumshawishi aliyekuwa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Leodegar Chilla Tenga arejee tena ili kusaidia kuyatoa kwenye matope magurudumu ya shirikisho hilo.
TFF imekwama, rais wake Jamal Emily Malinzi, amefeli na hali inaonyesha wazi kuwa tuendako kuna hatari zaidi ya kutumbukia kabisa shimoni.
Kuna mengi ya kuonyesha kwamba Malinzi amefeli na kwa kuwa watu wanaona haya kuelezana ukweli, wanachukia kukosolewa, huenda kilichofanywa na TFF ya Tenga kwa mihula miwili, kitaporomoka na kupotea kabisa ndani ya nusu mhula wa Malinzi, nitafafanua.


Yamepita mengi kama ambayo tumeona, ile Taifa Stars maboresho iliyopotelea kusikojulikana na hakuna faida ya kusema ilikuwa imewekwa kwa malengo zaidi ya kuwasikia viongozi wakisema kuna wachezaji wa timu hiyo wamesajiliwa timu fulani tena asilimia 5 tu ya wachezaji hao, wengine hawajulikani walipo.


Matumizi mabaya na kuhama ofisi zao kwenye kupanga kwa mamilioni lukuki ni jambo jingine. Lakini kufeli kwa Taifa Stars ambayo iliwekewa ahadi kibao na sasa zinaanzishwa kamati tu eti za kutafuta walioihujumu ikionyesha wazi ni janja ya kutaka kuwaziba 
Watanzania macho na masikio.


TFF ya Malinzi ni ile inayokwenda na mtindo wa ‘unfinished business’. Hakuna ilichokianza, ikikimaliza na kila ilichofanya kimefeli, huenda kipo, basi watanikumbusha.
Sijui kama kuna yule anayeweza kukataa kuwa TFF ya sasa imejaa ubabe, inayoangalia itapata vipi fedha bila ya kujali wengine wataathirika vipi.


Mfano mzuri ni sakata la TFF sasa kuagiza klabu zianze kukatwa udhamini wao wa Vodacom na Azam TV ili ziende kwenye Mfuko wa Maendeleo ya Soka (FDF) eti ina mpango wa kusaidia vijana.
Ni maajabu saba kusikia eti kuna watu wanaona TFF iko sawasawa, inajenga hisia katika masuala yanayotakiwa kufanyiwa kazi kuusaidia mpira wetu, wako wanaofanya ushabiki kwa kuwa tu wanaweza kusaidiwa kurahisisha maisha yao!


Mpira huu ni kwa faida ya sisi tuliopo, wadogo na watoto wetu, pia vizazi vijavyo. TFF inafeli kwa kuwa inataka kuyapeleka mambo kiswahiba, kwa kubahatisha na viongozi kuangalia watapata nini, si mpira utapata kipi kwa ajili ya leo na baadaye.
Kichekesho cha kwanza ni kwamba TFF ndiyo inachukua fedha nyingi zaidi kwenye udhamini wa Azam TV na Vodacom kuliko hata klabu moja, hii ni kwa kila msimu. Lakini sasa inataka zaidi.
Kichekesho zaidi, klabu zinakatwa tayari fedha asilimia 6 katika mapato na zinakwenda kwenye mfuko huo.
Kukata mapato ni jasho lao, sawa hilo limekubalika, kukata hizo wanazopewa na wadhamini ndiyo juhudi na morali, ni sawa na kuwaua kisoka. Hofu yangu, TFF isije ikaagiza hata asilimia 5 za mishahara ya wachezaji na makocha nayo ianze kukatwa ili kusaidia soka.


Vodacom:
Udhamini wa Vodacom uko hivi, nitaufafanua kidogo; mkataba huo wa Vodacom uliosainiwa Septemba 11, 2012 ni wa miaka mitatu na kila msimu unatofautiana.
Msimu wa 2012-13, klabu zote 14 zilipewa Sh milioni 882 kwa ajili ya usafiri na zikigawanywa kila moja inapata Sh milioni 63. Msimu wa 2013-14, zinatolewa Sh milioni 952 (kila klabu Sh milioni 68) na msimu wa mwisho wa 2014-15 Vodacom wanatoa Sh bilioni 1.1 (kila timu Sh milioni 72).
Mgawo wa TFF kwa fedha kutoka Vodacom katika misimu hiyo mitatu uko hivi; 2012-13 (Sh milioni 160), 2013-14 (Sh milioni 172) na 2014-15 (Sh milioni 183).
Ukichukua fedha za TFF kwa kila msimu, toa za klabu moja, utagundua TFF inapata zaidi ya kila klabu kama ifuatavyo. Msimu wa 2012-13 (TFF inapata zaidi Sh milioni 97), 2013-14 (zaidi Sh milioni 104) na 2014-15 ambao ndiyo msimu huu (TFF inachota zaidi ya Sh milioni 111).
Kila msimu fedha ya Vodacom imepanda kwa kila klabu, lakini pengo la kuchukua nyingi zaidi kwa TFF nalo linazidi kuwa kubwa!


Azam TV:
Mkataba wa Azam TV, una pande tatu, kampuni hiyo ya runinga, TFF na Bodi ya Ligi Kuu Bara (TPL). Kampuni hiyo inatoa fedha sawa kwa pande hizo mbili.
Ni wa misimu mitatu ukianza 2013-14, TFF na TPL kila moja inapewa Sh milioni 140, 2014-15 (kila mmoja Sh milioni 154) na 2015-16 (kila moja Sh milioni 169). Kwa misimu yote mitatu, wote wawili, kila mmoja anapata Sh milioni 463.4.
Mgawo wa Azam TV kwa kila klabu kwa misimu mitatu uko hivi, msimu wa 2013-14 (Sh milioni 100), 2014-15 (Sh milioni 110) na 2015-16 (Sh milioni 121). Jumla kwa misimu yote mitatu, kila klabu italamba Sh milioni 331.
Msimu wa kwanza TFF inazizidi klabu kwa Sh milioni 40, wa pili Sh milioni 44 na wa tatu Sh milioni 48, maana yake pengo la wingi kati ya TFF pia linazidi kuongezeka kila wadhamini wanavyoongezeka kama ilivyo kwenye ule mkataba wa Vodacom!
Kama umeona yote hayo, basi nitakuachia maswali zaidi utafakari na kujiuliza, vipi TFF hairidhiki? Vipi inataka kufanya dhuluma mchana na vipi haitaki kujibu hoja na inafanya lazima?
Jiulize TFF na klabu, ipi inalipa mshahara watu wengi, ipi inasafiri zaidi na ipi ina gharama nyingi za uendeshaji, lakini usisahau shirikisho hilo kila mwaka linapewa dola 250,000 (zaidi ya Sh milioni 400) kwa ajili ya maendeleo ya soka kutoka kwa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa).
Usisahau TFF inapata fedha za mfumo wa maendeleo ya soka kutoka kwenye makato ya viingilio vya klabu na haijawahi kusema hata mara moja kwa mwaka inaingiza kiasi gani na kinatumika vipi. Hakika inatakiwa kueleza hilo kwa kuwa fedha hizo ni za taasisi ya umma na si ya Malinzi au washauri wake!
Kutaka klabu ziwatangaze wadhamini, halafu fedha zitumike kuisaidia Taifa Stars, si sahihi. Hii inaonyesha mawili.
Moja, fedha inazopata TFF kutoka kwa wadhamini hazitumiki vizuri na wakati wa kuanika mahesabu hadharani umefika sasa.
Pili, unaweza kusema ukosefu wa ubunifu kwa kuwa TFF ina kitengo cha masoko ambacho kingefanya kazi ya kusaka wadhamini ambao watakubali kuzidhamini timu za vijana na watoto kama ambavyo uongozi wa Malinzi ulivyoingia madarakani na kuikuta Taifa Stars tayari inadhaminiwa na Kilimanjaro, uongozi wa Tenga ulifanya ubunifu ndiyo maana haukuingia kwenye mzozo na klabu kwa kutaka fedha zao za udhamini ambazo zilikuwepo tokea wakati ule, ndiyo maana nasema uongozi wa sasa wa Malinzi, umefeli. Nitarudi.

1 comment:

Anonymous said...

Kelele za mlango hazimzuii mwenye usingizi kulala. Malinzi Kula kama wanavyokula wengine tuache alfu ulela ulela.