Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa akizungumza kwenye mkutano na waandishi Dar es Salaam jana. Kushoto ni Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu na Makamu Mwenyekiti (Zanzibar), Said Issa Mohamed. Picha na Venance Nestory
Dar es Salaam. Kamati Kuu ya Chadema imeazimia kuendesha kampeni ya kupinga Katiba Inayopendekezwa kwa viongozi wake wakuu pamoja na wale wa mabaraza yake kufanya ziara katika mikoa mbalimbali nchini.
Hatua hiyo imekuja siku tatu, tangu Rais Kikwete autangazie umma wa Watanzania alipokuwa akihutubia kilele cha Mbio za Mwenge mkoani Tabora kwamba Katiba Inayopendekezwa inafaa hivyo kuwataka Watanzania waipigie kura wakati wa mchakato wa kura ya maoni.
Ziara ya Chadema itaanzia katika mikoa ya Kanda ya Ziwa ambako itachukua siku 20 ikiongozwa na Baraza la Wanawake (Bawacha), linaloongozwa na Mbunge wa Kawe, Halima Mdee na baada ya kumaliza, itaanza ziara nyingine ya siku 20 itakayofanywa na Baraza la Vijana (Bavicha).
Dk Slaa alisema CCM wameanza kazi ya kuwataka wananchi kupiga kura ya ‘ndiyo’ na Chadema wanaanza mikutano ya kuwashawishi wananchi kuikataa kwa kuipigia kura ya ‘hapana’.
Alisema kuanzia Novemba 5 mwaka huu, viongozi wa ngazi za juu wa chama hicho nao wataanza ziara katika mikoa mbalimbali nchini.
“Bawacha ndiyo itakuwa timu ya kwanza. Itakwenda Mwanza mjini, Ukerewe, Magu, Sengerema, Geita, Busanda, Bukombe, Biharamulo, Muleba, Karagwe, Bukoba Mjini, Chato, Shinyanga Mjini na Maswa Mashariki,” alisema Dk Slaa.
Alisema uchakachuaji uliofanyika katika Bunge la Katiba umezaa Katiba isiyotokana na maoni ya wananchi, kwamba kazi iliyopo sasa ni kuipigia kura ya ‘hapana’ kwa sababu inabeba kundi fulani la watu wachache.
“Itakayopatikana si Katiba ya Tanzania ni Katiba ya CCM. Chama hiki kiliandaa rasimu yake na kuhakikisha kuwa inaingizwa katika Katiba Inayopendekezwa. Mwaka 2011 Halmashauri Kuu ya CCM (Nec) iliagiza viongozi wa CCM kuhakikisha kuwa mambo yote yanayopigiwa debe na chama hicho yaingizwe katika Katiba na hilo limefanikiwa,” alisema na kuongeza:
“Tunapenda kuwaeleza Watanzania, asasi mbalimbali na taasisi za dini kuwa wakati umefika. Sasa tuache kulialia, kulalamika na kunung’unika.”
Tafsiri ya Katiba
Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu alieleza hatua mbalimbali zinazotoa tafsiri ya wazi jinsi Katiba Inayopendekezwa inavyokosa uhalali wa kupigiwa kura ya ‘ndiyo’ katika kura ya maoni.
“Kwanza Bunge Maalumu la Katiba lilijigeuza Tume ya Katiba na kuanza kukusanya upya maoni ya makundi mbalimbali. Wajumbe waliokuwa nje ya Bunge hilo kuruhusiwa kupiga kura na wale waliopiga baadhi ya Ibara kuhesabiwa kuwa wamepiga kura ya ‘ndiyo’,” alisema Lissu.
Alisema hata baadhi ya wajumbe wa Bunge hilo walioelezwa kuwa wangepiga kura katika balozi za Tanzania katika nchi mbalimbali, haijaelezwa walipigia kura hizo wapi.
“Wajumbe wa Bunge la Katiba, Mohamed Raza na Salim Turky wote kutoka Zanzibar waliharibu kura zao, lakini zilizoharibika zilihesabiwa kura halali.
Hata hivyo Raza na Turky walipotafutwa jana kupitia simu zao za mkononi kuzungumzia suala hilo hawakupatikana.
Alisema hata wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kutoka Zanzibar na wengine waliosusia vikao vya Bunge hilo na ambao hawajulikani majina yao hadi sasa, zilihesabiwa kura halali za ‘ndiyo’.
“Maulida Komu alikuwa Ukawa, katika Gazeti la Serikali alitangazwa anatokea Zanzibar, aligeuzwa na kuonekana kuwa anatokea Tanzania Bara. Mjumbe mwingine, Zakhia Meghji wa CCM anatokea Tanzania Bara lakini tumeelezwa kuwa anatokea Zanzibar,” alisema.
Katika hatua nyingine, wakati Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa akidai kuwapo kwa mpango wa ununuzi wa helikopta tatu za Serikali kwa malengo ya kuzitumia kuisaidia CCM kwenye Uchaguzi Mkuu ujao, Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue amesema madai hayo siyo ya kweli.
Jana, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maazimio ya kikao cha Kamati Kuu ya Chadema, Dk Slaa alidai kwamba kuna mpango wa ununuzi wa helikopta tatu za Serikali ambao unapangwa kufanywa bila kufuata taratibu za ununuzi na kwamba Rais Jakaya Kikwete akienda ziarani China ataiona mojawapo.
Alidai kwamba helikopta hizo zitakazonunuliwa kwa mkopo kutoka Serikali ya Ujerumani, zitanunuliwa Ufaransa lakini wakala anayetumika kuzinunua anatuhumiwa nchini kwa ufisadi, alisema wakati ukifika atataja jina la wakala huyo.
Mbali na helikopta hizo, Dk Slaa pia alidai kuwapo kwa mpango wa kununua mitambo maalumu ya kunasia sauti za viongozi wa Chadema.
Hata hivyo, Balozi Sefue katika maelezo yake alisema: “Ni kweli kwamba Rais atakwenda China kwa mwaliko wa Rais wa nchi hiyo, lakini haendi kuangalia chopa”.
Katibu Mkuu Kiongozi aliweka wazi kuwa yapo mawazo ya kununua helikopta hizo kwa ajili ya matumizi ya jeshi lakini uamuzi bado haujafanyika.
“Hata kama uamuzi utafanyika kwamba zinunuliwe kwa ajili ya kuliwezesha jeshi letu (nasisitiza, bado uamuzi haujafanyika sasa) haiwezekani kusafirisha helikopta kwenda China kwa sababu ziara ya Rais haihusiani kabisa na suala hilo,” alisema.
Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu alisema kauli ya Dk Slaa ni uzushi na uongo na kwamba ajifunze kusema kweli... “Ni kiongozi na tunamheshimu kwa hiyo lazima ajifunze kusema kweli. Haiingii akilini kusema kwamba helikopta inaweza kusafiri kilometa zote hizo kwenda kumfuata Rais China eti akaione, kwani Rais ni injinia au ni nani?
Halafu technically (kiufundi) ni jambo lisilowezekana”. Umbali kutoka Paris Ufaransa hadi Beijing, China ni kilometa 8,022.
Uchaguzi Mkuu
Akigusia ununuzi wa mitambo ya usalama itakayotumiwa na Jeshi la Polisi, huku akionyesha nyaraka ya serikali yenye maelezo ya ununuzi huo iliyoandikwa na Ofisa wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa (jina limehifadhiwa) alisema:
“Rais ameomba kwenda Beijing kwa ajili ya kuona mitambo ya kiusalama ya polisi. Cha kushtusha zaidi katika nyaraka hii inaeleza mitambo hiyo lazima iwe imefika haraka iwezekanavyo kabla ya Uchaguzi Mkuu kwa sababu tunaogopa kuna vurugu zitatokea. Hayo yamesemwa kwenye maandishi wa Serikali,” alisema.
Alisema aliyeandikiwa nyaraka hiyo ni Waziri wa Mambo ya Nje na kufafanua kuwa nyaraka hiyo iliandikwa Oktoba7, 2014 na mawasiliano kati ofisa huyo na Waziri yalifanyika saa 11 jioni.
Katika mkutano wake Dk Slaa pia alisema: “Rais anaambiwa kwamba ndege ya Jeshi anayotaka kununua ipo kwenye mji mwingine, mji huo haupo katika eneo la ziara yake, lakini wanawaambia wahusika kule China, ndege irushwe na iletwe mpaka Rais atakapokuwa ili aione mwenyewe. Hivi Rais ni ofisa mnunuzi au!” alihoji.
Akizungumzia hilo safari hiyo, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, Mkumbwa Ally alisema: “Hatuna taarifa kama Rais anakwenda Beijing.”
Kuhusu madai ya Rais kukagua vifaa vya kiusalama vya polisi na helikopta zinazodaiwa kuwa zitanunuliwa Mkumbwa alisema: “Hayo ni madai ya kufikirika kwa kuwa Rais siyo ofisa ununuzi.”
Mwananchi
No comments:
Post a Comment