Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ambaye pia ni Mganga Mkuu wa Serikali, Dk. Donald Mmbando
Serikali imewatoa hofu wa wananchi kuhusu ugonjwa mpya wa Marburg ambao umelipuka nchini Uganda huku dalili z\ake zikifanana na za Ebola.
Aidha Wizara imewataka wananchi kupuuzia taarifa zinazosambazwa na watu wachache kuwa ugonjwa wa ebola umeingia nchini wakati siyo kweli kwa kuwa Wizara ndio inatakiwa kutoa taarifa hizo.
Hayo yalisemwa jijini Dar es Salaam jana na Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ambaye pia ni Mganga Mkuu wa Serikali, Dk. Donald Mmbando, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kampeni shirikishi ya chanjo ya Surua na Rubella kuanzia kesho hadi Oktoba 24, mwaka huu.
Alisema Serikali imejipanga kufanya vipimo katika mipaka yote pamoja na sehemu nyingine ili kukabiliana na kusambaa kwa Ebola pamoja na marburg.
“Ugonjwa ulioko Uganda unafanana dalili zake na ugonjwa wa ebola Serikali ya huko tayari imeudhibiti na usisambae na sisi huku tumejipanga kukabiliana na hali yoyote itakayo jitokeza,” alisema Mmbando.
Alisema tayari zaidi ya watu 4,000 wameambukizwa na ugonjwa wa ebola Afrika Magharibi huku nusu yake wakiwa wameshafariki.
Dk. Mmbando alisema nchi zimetakiwa kuweka mikakati ya kujikinga na ugonjwa huo kwa kutoa elimu.
Aidha alisema kuwa Serikali imeandaa kamati ya kitaifa inayoongozwa na Mganga Mkuu wa Serikali ili kufatilia kuenea kwa ebola.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment