ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, October 21, 2014

Dk. Slaa: Tukishinda elimu itakuwa bure

Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk.Willibrod Slaa (pichani), amesema chama hicho kimejiwekea ajenda nne na kuwa ifikapo 2015 kikishika dola, kazi yao ni kutoa elimu bure na bora kwa watanzania.

Hata hivyo, amesema Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeichakachua sera hiyo ya Chadema iliyowekwa katika Ilani yake ya uchaguzi wa mwaka 2010 na kusema elimu ya bure inawezekana, ingawa hadi leo chama tawala kimeshindwa kutekeleza ahadi hiyo.

Alitoa kauli hiyo alipokuwa akihutubia wananchi katika mkutano wa hadhara mjini Iringa.
Alisema ajenda ya pili ya Chadema katika uchaguzi mkuu uliopita ambayo pia wataitekeleza ni vifaa vya ujenzi kushushwa bei ili kila Mtanzania awe na uwezo wa kujenga nyumba ya saruji na bati.

Alisema kuwa wazee wote, wafugaji, wakulima, mama lishe na makundi mengine watapewa pensheni kwa sababu wote wamechangia uchumi wa nchi na kwamba haiwezekani kuona wazee wanakufa hivihivi wakati wamechangia.

Ajenda ya nne alisema ni huduma bora za maji na afya ambazo ni jukumu la serikali na siyo la mtu mmoja mmoja, lakini serikali ya CCM imewatupia wananchi badala ya kuhakikisha wanapata huduma hiyo.

Hata hivyo, alimkosoa Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, kwamba anazunguka nchi nzima na kuwadanganya vijana kuwa atawapatia ajira, lakini hazungumzii kuimarisha na kujengwa viwanda.

“Kinana alisema kuwa atawapa vijana bodaboda, lakini Chadema kinasema msigawe bodaboda, tengenezeni viwanda hapa nchini ili vijana wapate ajira na ziuzwe kwa bei ya chini, lakini siyo wagawe bodaboda ambazo zitawafanya wawe vilema na kusababisha nguvu kazi ya nchi kushuka,” alisema.

Kuhusu katiba inayopendekezwa, Dk. Slaa alisema vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vitazunguka nchi nzima mtaa kwa mtaa na kijiji kwa kijiji katiba hiyo itakapopelekwa kwa wananchi kwa ajili ya kupigiwa kura na kuwataka wananchi waikatae.

Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Profesa Abdallah Safari, alisema maendeleo ya Tanzania yamedumazwa na serikali kuingia katika mikataba mibovu ambayo haijali maslahi ya wananchi na kwamba umaskini wa wananchi umetokana na CCM huku akitolea mfano kwa sekta ya madini kuingiza mapato madogo.
SOURCE: NIPASHE

2 comments:

Anonymous said...

HUU NI UWONGO MTUKUFU KWANI DUNIA NZIMA ELIMU NI YAKULIPIA TUMUULIZE ATAITOA BURE KI VIPI

Anonymous said...

Wanasiasa huwa hawasemi uongo