Wednesday, October 15, 2014

Habari kamili ya Ajali ya tenki la mafuta Dar- yaua, yajeruhi 20

Watu 20 wameungua vibaya na mmoja kufariki dunia baada ya kulipukiwa na petroli wakati kundi la vijana walipokuwa wakijaribu kupora mafuta hayo kwenye lori hilo lililopinduka eneo la Mbagala Rangi tatu jijini Dar es Salaam.

NIPASHE ilifika jana katika eneo na kushuhudia umati wa watu wakishangaa tukio, huku maduka sita, bar moja na nyumba ya kulala wageni vimeungua.

Mmoja wa mashuhuda hao, Shabani Mlawa alisema Majira ya saa 5:30 usiku, gari lilikuwa likitoka kujaza mafuta.

Alisema mara lilipofika katika eneo hilo likapinduka na kutumbukia kwenye mtaro ndipo dereva na utingo waliomba msaada kwa wananchi.

Alisema wananchi waliwasaidia kwa kubomoa hicho kioo, lakini baada ya dereva kutoka alitoa tahadhari kwa wananchi wasivamie gari hilo kwa kuwaeleza kuwa lilikuwa limebeba petroli.

Alisema cha kushangaza wananchi hao walifuata ndoo na kuanza kuchukua mafuta hayo na kwamba wakati wakiendelea kuna mtu aliyegusa betri ya gari hilo na kulipuka moto.
Alisema wengi waliiba mafuta hayo na kukimbia ovyo.


Muuguzi wa zamu wa Hospitali ya wilaya ya Temeke, Rolester Kinunda, alithibitisha kupokea maiti moja ya mwanaume na wengine 20 waliojeruhiwa vibaya.
Kati ya hao 19 walikuwa wanaume na mmoja alikuwa mwanamke na baada ya kuwapokea, majeruhi 15 walihamishiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kutokana na hali zao kuwa mbaya.

“Tulianza kupokea majeruhi majira ya saa 6:15 usiku wa kuamkia leo (jana) na maiti ya mtu mmoja akiwa ameungua vibaya,” alisema Kabelege.

Mmoja wa majeruhi, Mukiza Baltazar, alisema alikuwa akitembea kwa miguu jirani na eneo la ajali, na aliona lori la mafuta likipinda kona kwenye mzunguko likielekea Mbagala Charambe na ghafla akajitokeza dereva wa pikipiki, wakati dereva anajaribu kumkwepa lori likaingia mtaroni na kupinduka.

“Ghafla watu wakakimbilia kwenye lori hilo wakijaribu kuiba mafuta na betri na hapo ndipo mlipuko ulipotokea na mimi nikajikuta naungua miguu,” alifafanua.

Baltazar alisema, awali aliona kijana mmoja akichota mafuta na kukimbilia kwenye jirani na eneo la tukio na alipojaribu kukaribia kwenye kibanda cha kuchoma chipsi, moto ulimlipukia. “Ilikuwa balaa, eneo loto lilikuwa linawaka moto kama vile kuna milipuko ya mabomu,” alisema.

Majeruhi huyo ambaye aliungua miguu yake yote miwili, alisema, hakuwa miongoni mwa watu waliokuwa wakipora mafuta bali alikuwa anapita njia na haelewi ni jinsi gani alijikuta akiwaka moto.

Kinunda alisema majeruhi waliofikishwa hospitalini hapo 20 walikuwa ni wanaume wenye umri kati ya miaka 18 na 40 mmoja alikuwa na ni mwanamke.

Aliwataja majeruhi hao na miaka yao kwenye mabano kuwa ni Ibrahim Hamisi (36), Hamisi Ally (35), Nurdin Salum 24), Rajabu Selemani (28), Abass Uganga (20), Shabati Martin (40), Hassan Mohammed (40), Moses Israeli (40), Maganga Mgombela (38) na Ramadhan Khalfan (26).

Wengine ni Hamisi Benale (25), Mkiza Baltazar (31), Hamad Salehe (30), Abass Mohammed (30), Selemani Kassim (33), Iddi Saidi (28), Mathayo Daniel(21), Mohammed Ismail (19) na mwanamke pekee Jane Mathayo (25).

Hata hivyo, Kinunda, alisema, Jane Mathayo alitoroka hospitali usiku wa manane bila ya ruhusa ya daktari.

NIPASHE ilipomtafuta Kamanda wa polisi Temeke, Kihenye Kihenye alisema yupo nje ya mkoa wa Dar es Salaam na kuelekeza atafutwe kaimu wake, ambaye naye alisema taarifa zote zitatolewa na Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova.

Hata hivyo, Kova alisema hawezi kuzungumzia tatizo dogo kama hilo bali Kamanda wa Teneke alipaswa kulitolea taarifa.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake