ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, October 7, 2014

MAAJANU YA AKIDI BUNGE MAALUMU LA LATIBA

UKIACHILIA MBALI, tabasamu lenye mashaka la baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, ukiacha na jina iliyopewa kuwa ni Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 2014, Ukiacha kuzingatia ukataji viuno uliofanywa na wabunge, ukiacha na kejeli, vijembe, ukiangalia na kukumbatiana kwao, bila kujali kauli ya “tumepitisha liwalo na liwe”, akidi ya Bunge Maalumu la Katiba imeacha maswali mengi ya ajabu.
Ajabu ya kwanza, idadi iliyotajwa kabla ya kupiga kura, na idadi iliyotajwa baada ya kupiga kura ni tofauti. Tuliambiwa wakati wa kuanza zoezi la kupiga kura wajumbe wa Zanzibar walikuwa 210, lakini wakati wa kusoma matokeo tukaambiwa wapo 219, haijajulikana wazi walioongezeka ni wapiga kura au kura zenyewe, bado kitendawili.
SamuelAjabu ya pili, kwa idadi zote, ya kwanza na ya pili, zote akidi imeleta utata. Kama idadi ya kwanza ni sahihi, yaani 210, theluthi mbili ilikuwa ni kura 140. Katika Idadi hiyo, inajulikana wazi kuwa wajumbe wa kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ilikuwa ni 67, waliopiga kura za hapana wazi wazi mbele ya Televisheni wananchi wakiwa wanaona ni 8, ukijumlisha waliotoka na waliopiga kura za hapana ni 75.
Kwa idadi hiyo bila kuhesabu wengine ambao hawakupiga, wapiga kura waliotoka Zanzibar walibaki 135, hata kama wangepiga kura wote za ndio. Akidi ya theluthi mbili ilikuwa 140 kama wangekuwa 210, je, hizo kura 5 hadi 6 zilipatikanaje? Zilipatikana toka wapi?.
Ajabu ya tatu, kama kura zote za Zanzibar zilikuwa ni 219 kama tulivyotangaziwa maana yake theluthi mbili ya 219 ni 146, Sasa 219 ukitoa wajumbe 67 wa Ukawa, na 8 waliopiga kura za hapana, 219 -75 inabaki 144, je, kura mbili zilitoka wapi kufikisha akidi?
Ajabu ya Nne, Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta aliwatangazia watanzania kuwa kuna wajumbe wawili wa Ukawa wamepiga kura za ndiyo na wapo tayari kufukuzwa kwenye Chama chao, hakutaja Chama.
Kisheria, ili uwe mpiga kura halali unapaswa kusajiliwa. Wajumbe wa Ukawa kutoka Zanzibar hawakusajiliwa katika Bunge Maalumu la Katiba la awamu ya pili kwa sababu hawakurejea Bungeni Agosti, mwaka huu. Maana yake kama walipiga kura walikuwa sio wapiga kura halali waliosajiliwa.
Hata kama walipiga, kanuni za Bunge hilo ziliweka utaratibu kuwa wote watakaopata fursa ya kupiga kura wakiwa nje ya bunge wanapata kibali maalumu cha Mwenyekiti kutokana na sababu maalumu zikiwemo Hija, Mitihani au Matibabu, Je, wabunge wa Ukawa walipewa kibali na Sitta?
Je, anatambua sababu za Ukawa kuwa nje zilikuwa ni halali kwa mujibu wa kanuni mpaka awapatie kibali kupiga kura? Kuna udanganyifu katika hili, watu ambao hawajajisajili, hawawezi kupewa kibali maalumu kupiga kura, hizi mbili zilitoka wapi?
Ajabu ya Tano, Idadi ya Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba tuliyoambiwa ni 619, tunaambiwa waliotoka Zanzibar ni 210, na waliotoka Tanganyika ni 419 ili kupata jumla kuu.
Jumla kuu iliyotangazwa na Rais Jakaya Kikwete wakati wa uteuzi, na jumla kuu iliyotangazwa na Sitta ni ile ile, maana yake walikuwa na hofu ya kuchakachua, ndio maana hawakupunguza kura wakahesabu ya Marehemu Shida Salumu aliyekuwa mjumbe wa Bunge hilo. Walihesabia na kura ya marehemu (Mungu amrehemu).
Je aibu gani hii, wabunge wote, vikokotozi vyote (Calculator), washauri wote, na Usalama wa Taifa wote hakuna aliyekumbuka kuondoa kura mmoja ya mjumbe aliyefariki, akili zote zilielekezwa kwenye kupata akidi ya Zanzibar na ambayo kimsingi inaonekana haikupatikana kwa maelezo yeyote yale.
Ajabu ya Sita, wajumbe wote wa Bunge hilo baada ya kupatikana kile kilichoitwa akidi, walikuwa na wimbo na stahili moja ya kucheza. Wimbo ulitungwa lini? Ulitungwa na nani? Kwa makusudi yapi? Walifanya mazoezi wapi, kwa muda gani na hadi kile walichosema ni akidi kilipotajwa wakaanza kuimba?
Hivyo basi ili Rasimu ikwame kwa upande wa Zanzibar ilihitaji kura 74 au zaidi za kuikataa. Yaani idadi yoyote ambayo itazidi 73 (theluthi moja) ingekwamisha Rasimu.
Turudie kidogo somo la hesabu pamoja na wajumbe wa CCM waliopitisha Katiba inayopendekezwa. Kama Ukawa walioikataa Rasimu ni 65 kama Sitta alivyotangaza tunaongeza na 8 ikiwemo ya Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar hapo tutapata kura 73. Kuna mpiga kura anaitwa Abdallah Abbas ambaye aliondoka Bunge la Katiba na hakupiga kura jumla ni 74 kwa idadi hiyo tayari kura hizo zimezidi theluthi moja, ambayo ni 73 Lakini cha ajabu tunaambiwa Rasimu imepita. Imepitaje?
Kama waliokataa wamezidi theluthi moja, inakuaje tena waliokubali nao wazidi theluthi mbili? Hesabu za aina hii ngumu kama mtu unasahihisha mtihani, unaweza kupuuza daftari la mwanafunzi huyu na kuandika “seen”, “nimeona” au kupiga mstari tu kuthibitisha kuwa Mwalimu ameliona daftari la Mwanafunzi mzembe asiyefikiri sawasawa.
Sitta ametekeleza wajibu wake kuwasulubu watanzania ili kutekeleza mapenzi ya chama chake, ni kama mfano uliotokea kwa Pilato aliyemhukumu Yesu akiwa hana hatia. Watanzania wamenyang’anywa haki ya kushiriki katiba yao bila hatia. Pilato aliogopa Wakuu wa makuhani na Sitta amewaogopa CCM akajiondoa ufahamu kaanza hata kutukana viongozi wa dini.
Pilato hakuona hatia kwa Yesu akaanza kutafuta njia ya kumwachia lakini kwa kuwa Wakuu wa Makuhani walikusudia, waliona heri Yesu asulubiwe lakini Muuaji anayeitwa Baraba awe huru. Pilato aliwauliza wakuu wa Makuhani, Basi, nimtendeje Yesu aitwaye Kristo? Wakasema wote, Asulibiwe.
Akawauliza tena Kwani? Ni ubaya gani alioutenda? Wakazidi sana kupiga kelele, wakisema, Na asulubiwe. Hawakutaja kosa lake, sisi watanzania hatujatajiwa makosa yetu sharia zimechakachuliwa na akidi ikachakachuliwa
Pilato aliogopa ghasia iliyozidi akatwaa maji, akanawa mikono yake mbele ya mkutano, akasema, Mimi sina hatia katika damu ya mtu huyu mwenye haki; yaangalieni haya ninyi wenyewe. Watu wote wakajibu wakasema, Damu yake na iwe juu yetu, na juu ya watoto wetu.
Kazi kubwa iliyopo kwa Rais Kikwete, Sitta amejitoa ufahamu, anakuletea kinachoitwa Katiba inayopendekezwa chenye kulalamikiwa kila kona ya nchi, wanakileta kwa mbwembwe sare wameshona kwa pesa za walipa kodi masikini ambao mawazo yao yalipuuzwa.
Kusaini hicho kinachoitwa Katiba inayopendekezwa ni kuliingiza taifa machafukoni, damu ya watanzania imewekwa rehani mikononi mwako, ni juu yako Rais Kikwete kuamua ili damu ya watanzania iwe juu yako na juu ya watoto wako kama walivyojipiza wakuu wa makuhani ili waafiki uamuzi wa kumuua Yesu ingawa hakupatika na hatia. Kazi kwako
CHANZO: TanzaniaDaima

No comments: