Amri hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Janeth Kaluyenda, baada ya upande wa Jamhuri kueleza kuwa mshtakiwa wa kwanza Mdee, wa tatu Renina Leafyagila na wa sita Sophia Fanuel hawajafika mahakamani kama ilivyokuwa imepangwa.
Wakili wa Serikali Mohamed Salum alieleza kuwa, upande wa Jamhuri uko tayari kuendelea kusikiliza maelezo ya awali lakini hauna taarifa za washtakiwa hao.
Kwa upande wake, Wakili wa Utetezi, Peter Kibatala, alieleza kuwa wadhamini wa washtakiwa wana taarifa za washtakiwa hao.
Mdhamini wa Mdee alidai kuwa mshitakiwa huyo alikuwa kwenye ziara za kichama Kanda ya Ziwa na kwamba alipanga kurejea jijini juzi lakini ilishindikana baada ya ndege kuahirisha safari.
Naye Mdhamini wa mshtakiwa wa tatu, alidai kuwa mshtakiwa huyo amefiwa na baba yake mzazi na kwamba jana walikuwa wanafanya maziko.
Halikadhalika, mdhamini wa mshtakiwa wa sita, alidai kuwa mshtakiwa huyo yuko kwenye msafara wa ziara ya chama na Mdee na kwamba walikosa usafiri wa ndege kurejea Dar es Salaam.
Baada ya maelezo hayo, upande wa Jamhuri ulikubaliana na sababu ya mshtakiwa wa tatu kuwa ni ya msingi kwa sababu kufa hakuna taarifa.
“Mheshimiwa hakimu sababu ya mshtakiwa wa kwanza na wa sita hazina msingi na mahakama isipokemea tabia hii itakuwa changamoto ya kuruhusu kila mtu kufanya anavyotaka na kuchelewesha usikilizwaji wa kesi… suala la kufika mahakamani washtakiwa kusikiliza kesi yao ni la msingi na ziara za kichama hazina uhusiano na mahakama hii” alieleza Salum.
Akizungumza baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Hakimu Kaluyenda aliwataka wadhamini hao wahakikishe washtakiwa wanazingatia umuhimu wa kuhudhuria mahakamani na kwamba siku mbili kabla ya kesi wanatakiwa kufanya mawasiliano nao ili kuzuia ucheleweshaji wa kusikilizwa kesi hiyo.
Alisisitiza washtakiwa wanatakiwa kuwapo mahakamani kila kesi yao inapopangwa.Kesi hiyo imepangwa kusikilizwa maelezo ya awali Novemba 5, mwaka huu na dhamana ya washtakiwa inaendelea.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment