Advertisements

Friday, October 24, 2014

NINI CHA KUFANYA MUMEO ANAPOZAA NJE YA NDOA?-2


Ni wiki nyingine tunapokutana tena katika ukurasa wetu huu. Mada ambayo tulianza kuijadili wiki iliyopita, ilikuwa ni nini cha kufanya unapogundua kuwa mumeo amezaa mtoto nje ya ndoa.

Tuliangalia mfano wa dada yetu mmoja ambaye alieleza kisa chake jinsi mumewe alivyozaa mtoto nje ya ndoa kiasi cha kumfanya ashindwe cha kuamua. Maoni yalikuwa mengi mno, nikushukuru msomaji wangu uliyeshiriki kutoa maoni yako.

Nilichojifunza na ambacho nataka na wewe msomaji wangu, ambaye una tatizo kama hili ujifunze, ni kwamba matukio ya wanaume kuzaa nje ya ndoa ni mengi mno huko mitaani. Hata hivyo, ni wanaume wachache ndiyo huwa na ujasiri wa kuwaeleza wake zao ukweli na wengine huendelea kuficha siri mpaka wanapofikwa na mauti.

Matokeo yake, baba akitangulia mbele za haki ndiyo wanaanza kujitokeza watoto wengine wa nje na mama zao ambao wanakuwa na uthibitisho wote kwamba kweli walikuwa watoto wa nje wa mumeo, tatizo linakuwa kubwa zaidi.

INAWEZEKANA KUSAMEHE?
“Wanaume ndivyo walivyo, wote wana matatizo yanayofanana. Ukisema uachane na mumeo kwa sababu amezaa nje, siyo sahihi, cha msingi ni kuwaita watu wa heshima na kukaa wewe na mumeo kujadili suala hilo.

“Inawezekana kabisa ukasamehe na maisha yakasonga mbele,” msomaji wangu ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini, alichangia na kueleza kwamba hata yeye imemtokea kwa mumewe.
Sishabikii kwamba wanaume waendelee kuzaa nje ya ndoa kwa sababu watasamehewa na wake zao lakini ninachotaka kukijengea hoja hapa ni kwamba kama tayari mtoto ameshazaliwa, ni sawa na maji yameshamwagika. Huwezi kuyazoa tena, kinachotakiwa kama alivyoshauri msomaji hapo juu, ni kutafuta suluhu.

Watafute watu ambao unawaheshimu, waeleze tatizo lako na ikiwezekana, wawakalishe nyote wawili pamoja. Bila shaka mumeo atakiri makosa yake na kwa pamoja mtakubaliana kusonga mbele. Huna haja ya kumchukia mtoto aliyezaliwa kwani yeye ni malaika tu asiyejua chochote.

Cha msingi ni kuhakikisha hakuna mawasiliano ya moja kwa moja kati ya mumeo na mwizi wako. Mnaweza kukubaliana kwamba fedha za matumizi ziwe zinapitia wapi ili kuzuia mawasiliano ya moja kwa moja ambayo yanaweza kuwafanya wawili hao wakarudi tena kwenye usaliti.

HAKUNA HAJA YA KUFANYA SIRI
Kwa mwanaume, kama unajua umeshateleza na kusababisha mtoto nje ya ndoa, ni jambo la muhimu sana kama wewe mwenyewe utaamua kumwambia mkeo ukweli kabla hajaujua mwenyewe. Unaweza kutafuta muda muafaka ambapo utamueleza kwa upole kilichotokea na kuonesha unavyojutia kosa lako.

Japokuwa bado ataumia, kidogo itasaidia kwa sababu atakuwa ameujua ukweli kupitia kwako mwenyewe kuliko kama angeujua mwenyewe. Kitu kibaya ni kuuficha ukweli kwa kipindi kirefu kwani kuna leo na kesho, inaweza kutokea wewe baba ukapoteza maisha huku nyuma ukaacha bomu kubwa la watoto kuanza kugombea mali za urithi.

Kama kweli unajutia kosa lako, mweleze mwenyewe mkeo na muombe radhi, usiishie hapo tu, hakikisha kosa kama hilo halijitokezi tena.

JAMBO LA MSINGI
Kila mmoja anapokuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi, ni muhimu kuishi vizuri na mwenzako ili kuepusha matatizo ya usaliti kwa sababu usaliti huwa hauji tu, lazima kuna tatizo ambalo linasababisha.
Kuwa karibu na mwenzi wako, mpende, mtunze na mfanyie mambo mazuri yatakayomfanya asifikirie kukusaliti na kuleta matatizo mengine kama haya ya watoto wa nje ya ndoa.

Ni matumaini yangu kwamba kwa haya machache, tutakuwa tumeelewana vizuri. Tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri. Kwa maoni, ushauri, au kama una mada ungependa tuizungumzie, nicheki kwa namba za hapo juu.

GPL

2 comments:

Anonymous said...

Picha ni za wazungu tu? Nauliza tu.

Anonymous said...

Asante kwa maoni mazuri. japo si rahisi kwa wanaume kuwa majasiri kiasi hicho ni ngumu sana, kusuhu eti kusiwe na mawasiliana na mwizi hapo itakuwa ni shida kabisa kwa sababu wakisha zaa nje kuna mtoto mawasiliano yatakuwepo tu hata kama kwa njia ya wizi. la msingi kama umeshaoa ni kuwa mwaminifu kwa mke wako.

kwa tatizo hilo ni kumwomba Mungu atusaidie ila wanaume wawe waaminifu kwenye ndoa zao.