Sunday, October 26, 2014

Polisi wakamata mabomu ya kivita Z’bar

Kamishna wa Jeshi la Polisi Zanzibar, Hamdan Omar Makame, akiwaonyesha mabomu manne ya kivita yaliyokamatwa katika eneo la Daraja Bovu, Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja. Picha na Mwinyi Sadallah

Zanzibar. Mabomu manne ya kivita yamekamatwa yikiwa yamehifadhiwa chini ya ardhi huko katika mji mdogo wa Daraja Bobu Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja na bomu moja likihusishwa kutumika katika mlipuko uliosababisha kifo cha mtu mmoja Juni 13 mwaka huu katika Manispaa ya Unguja.
Kamishna wa Polisi Zanzibar, Hamdan Omar Makame alisema mabomu hayo yameingizwa Zanzibar kupitia mtandao maalumu ambao umekuwa ukifanya vitendo vya uhalifu kwa kutumia mabomu hayo
Akizungumza na waandishi wa habari Makao Makuu ya Polisi Zanzibar, alisema katika tukio hilo tayari mtu mmoja anashikiliwa akihusika ingawa alisema ni mapema kumtaja jina lake lakini uchunguzi wa Mwananchi umebaini mtuhumiwa huyo ni mkazi wa Daraja Bovu kisiwani Unguja.
Kamishna Hamdan alieleza kuwa mtu huyo amekuwa akijihusisha na vitendo vya kuagiza, kuingiza na kuhifadhi mabomu ya kivita ya kurushwa kwa mkono ambayo yamekuwa yakitumika katika matukio mbalimbali ya kihalifu.
Alisema miongoni mwa matukio ya milipuko iliyotokea na kuhusishwa na mtandao huo ni pamoja na tukio la Mwanza, Arusha, Dar es Salaam na tukio lililotokea katika shehia ya Pangawe kisiwani hapa.
Matukio mengine ni yale ya kulipuliwa kwa mgahawa wa Mwrcury Februari 24 mwaka huu, milipuko miwili mbele ya Kanisa la Anglikana lililopo Mkunazini na mlipuko wa Darajani wa Juni 13 mwaka huu ambapo ulisababisha kifo cha Khatib Mohamed Khatib Mkombalaguah na watu saba kujeruhiwa.
“Mtuhumiwa mmoja tunamshikilia ambaye amethibitisha kujihusisha katika mtandao wa kuigiza, kuingiza na kuhifadhi mabomu ya kivita ya kurushwa kwa mkono ambayo yamekuwa yakitumika kwa uhalifu na uvunjifu wa amani nchini,” alisema Kamishna Hamdan.
Hata hivyo, alisema polisi bado inaendelea kuchunguza ili kujua mabomu hayo yametengenezwa kiwanda gani na yameingizwa Zanzibar kutoka sehemu gani, malengo na madhumuni kwa watu wanaofanya vitendo hivyo.
Akizungumzia kuhusu watu kukamatwa Zanzibar na kushtakiwa Tanzania Bara, alisema kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania polisi ina haki ya kufanya kazi pande zote za Muungano na mtuhumiwa kufunguliwa mashtaka kulingana eneo lilikofanyika kosa kisheria.
Alisema washtakiwa waliofunguliwa mashtaka ya ugaidi wanatuhumiwa kula njama ya kutenda makosa hayo katika maeneo ya Tanzania Bara na Zanzibar.
Kamishna Hamdan alisema hali ya usalama Zanzibar ni shwari na kuwataka wananchi kuendeleza ushirikiano ya kuwafichua wahalifu popote walipo ili kujenga na kuendeleza mazingira ya amani na utulivu.
MWANANCHI

No comments: