ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, October 21, 2014

Serikali yakalia trilioni 8.4/- za PSPF, NSSF, PPF

Mkurugenzi wa SSRA, Irene Isaka

Madeni sugu ya serikali yanatishia uhai wa mifuko ya hifadhi ya jamii nchini huku Mamlaka ya Usimamizi ya Mifuko hiyo ( SSRA) ikitoa angalizo kwa serikali kuhusiana na hali hiyo kufuatia kuidai Sh. trilioni 8.43.

Hali hiyo inaweza kukwamisha mifuko hiyo kuwalipa mafao wanachama wake, kujiendesha yenyewe na kuwekeza katika miradi mbali mbali.

Deni hilo linatokana na serikali na taasisi zake kukopa kwenye mifuko hiyo na kutopeleka michango ya wanachama.

Mkurugenzi wa SSRA, Irene Isaka, alisema deni hilo ni pamoja na lililotokana na ahadi ya serikali kulipa malipo ya pensheni kwa wafanyakazi ambao walikuwa hawachangii kwenye Mfuko kabla ya 1999.

Isaka aliyekuwa akizungumza katika mkutano ulioitishwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) na kuwakutanisha wakurugenzi wa kifumo ya hifadhi ya jamii, Wizara ya Fedha, Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Mkuu wa Hesabu za Serikali, SSRA na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), alisema deni jingine ni dhima ya mifuko ambayo ni kifurushi cha ahadi ambacho mwanachama ameahidiwa hadi siku anafariki na kwamba mifuko isipokuwa na hazina ya kutosha inabadilika kuwa kuwa deni.

Isaka alisema iwapo serikali itaendelea kukopa na kutopeleka michango ya wanachama wake, mifuko hiyo itaathirika kiasi cha kushindwa kulipa mafao kwa wanachama wake.

”Athari tuliyonayo, mifuko yetu ni ya pensheni, hasara ni ya mifuko. Mwanachama hatamsamehe mwenye mfuko kwa kushindwa kumlipia, kadri deni linavyoongezeka ndivyo Mfuko unaumia na baadaye kushindwa kulipa mafao yanayotakiwa,” alifafanua Isaka.

Alisema kwa madeni hayo Mfuko ambao unanunua kifurushi cha ahadi kwa mwanachama na unatakiwa kutimiza anapostaafu, utaendelea kuharibika kadri muda unavyozidi iwapo utashindwa kulipa madeni.

Awali, Kaimu CAG, Athumani Selemani, akizungumza alisema zaidi ya Sh. Trilioni 1. 37 ni deni la serikali na taasisi zake walikopa kutoka kwenye mifuko hiyo kwa shughuli mbalimbali.

Alisema zaidi ya Sh. trilioni 7.9 ni deni la PSPF la kuanzia 1999 ikiwa ni fedha za kuwalipa mafao wanachama ambao walikuwa hawachangii kwenye Mfuko lakini kwa mujibu wa sheria walioaswa kulipwa.

Selemani alibainisha deni hilo kwa kila mfuko inavyoonekana kwenye mabano ni PPF ( bilioni 192), NHIF ( bilioni 107), NSSF ( bilioni 467), PSPF ( bilioni 4.29), LAPF ( bilioni 170) na GEPF (bilioni 6.86).

Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dk. Servacius Likwelile, alithibitisha serikali kulitambua deni hilo na kwamba ni lazima ilipe ikiwa ni pamoja na deni ya PSPF kabla ya mwaka 1999.

Pamoja ka kukiri na kuahidi kulilipa madeni hayo, Dk. Likwelile hakueleza ni lini serikali italipa wala utaratibu utakaotumika kuyapunguza.

Akizungumza na waandishi wa habari kabla ya kuanza kikao hicho, Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe, alisema waliwaita BoT, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, CAG, SSRA, Wenyeviti wa bodi na Wakurugenzi wa mifuko ya hifadhi ya jamii kwa ajili ya kulijadili suala hilo.
Alisema lengo ni kujadili namna ya serikali kulipa deni hilo ili kuiwezesha mifuko hiyo kusonga mbele kwa kulipa mafao wanachama wake na kuwekeza.

Kabwe alisema serikali zote duniani zinakopa kwenye mifuko hiyo, lakini tatizo kubwa kwa serikali ya Tanzania ni kutolipa, jambo ambalo alisema ni hatari kwa uendeshaji endelevu wa mifuko hiyo.

”Tuna tatizo la serikali kukopa kwenye mifuko kwa ajili ya miradi mbalimbali na kutolipa, ni kawaida kwa nchi nyingine duniani kukopa na kurudisha tofauti kwa serikali ya Tanzania hairudishi,” alisema Kabwe.

Aliyataja baadhi ya madeni kuwa ni fedha za ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma Sh. milioni 800 na deni la PSPF la kabla ya 1999.

Alisema hali hiyo ikiachwa kuwa kama ilivyo sasa mifuko itashindwa kuwekeza katika miradi mbalimbali, hivyo ni muhimu madeni yalipwe ili mifuko iendelee kulipa madeni na kwamba itafika wakati itauza samani zake na kushindwa kufanyakazi.

Deni hilo ni takribani nusu ya bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2014/15 ambayo ni Sh. trilioni 19.8.

Wakati serikali ikidaiwa na mifuko hiyo, kiasi hicho cha fedha, Deni la taifa hadi Machi mwaka huu, lilifikia Shilingi trilioni 30 ikilinganishwa na Shilingi trilioni 23.6 Machi mwaka uliopita 2013.
CHANZO: NIPASHE

No comments: