Dar/Siha. Suala la Mahakama ya Kadhi jana liliibuka wakati wa maadhimisho ya Sikukuu ya Idd el Haji wakati naibu Imamu wa Msikiti wa Shafii, Sheikh Othman Amani aliposema kuwa ahadi ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuhusu Mahakama ya Kadhi ndiyo itakayoamua kura za Waislamu dhidi ya Chama cha Mapinduzi (CCM).
Katika kutuliza mvutano baina ya pande mbili zilizokuwa zikibishana juu ya kuingiza Mahakama ya Kadhi kwenye Katiba wakati wa kikao cha Bunge Maalumu la Katiba wiki iliyopita, Waziri Pinda alisimama na kuahidi kuwa Serikali itawasilisha muswada wa kutaka chombo hicho kitambuliwe kwenye Bunge la Februari.
Akihutubia baada ya Swala ya Idd al Haji kwenye Viwanja vya Msikiti wa Taqwa, Ilala jijini Dar es Salaam jana, Sheikh Amani alisema Waislamu wanasubiri Mahakama ya Kadhi iliyopo itambuliwe kimfumo na iwepo ndani ya Katiba.
Alisema kila mmoja miongoni mwa Waislamu ametia akilini na kwamba wanamfuatilia Waziri Mkuu ili Februari muswada uende bungeni na Mahakama ya Kadhi ikae sawasawa.
“Tunachotaka, iwe ndani ya Katiba na kikubwa tunafanya hivyo kwa busara na hekima. Tusitumie mabavu mpaka viongozi watakapotuambia sasa jamani tusiipigie kura CCM... Hayo maelezo yatakuja baadaye. Kwa sasa tunakwenda polepole, kuna mwelekeo wa kuelewana,” alisema.
Alisema wanachokitaka Katiba ndiyo itaje Mahakama ya Kadhi kwa sababu Waislamu ni sehemu ya walipa kodi wa nchi hii na hivyo wana haki hiyo.
“Kwamba upelekwe muswada ukafikiriwe wengine wakubali, wengine wakatae... Ni muswada moja kwa moja unatakiwa upite, kwa sababu sisi nasi ni wahusika katika nchi hii,” alisema Sheikh Amani.
Vijana na maendeleo
Mkoani Kilimanjaro, vijana wa Kiislamu wametakiwa kuwa wamoja na kufahamu umuhimu wao katika maendeleo ya mkoa wao na nchi kwa ujumla ili watumie ujuzi na nguvu walizonazo kwa manufaa ya Taifa.
Imamu wa Msikiti wa Majengo, Hashimu Muhamed alisema hayo jana katika hotuba ya swala ya Iddi iliyofanyika kwenye Uwanja wa CCM Sanya Juu.
Aliwataka vijana kuzingatia elimu kwa kuwa kuikosa ni jambo la hatari ambalo litasababisha kuyumbishwa kimaisha.
Sheikh Muhamed aliwataka vijana hao kutambua kwamba wao ndiyo muhimili wa maendeleo ya Taifa la leo na amani ya nchi kwa jumla
“Ni lazima muwe tayari kufanya kazi kwa bidii na kujenga Taifa na katika kufanikisha malengo hayo tunatambua kwamba vijana wanapaswa kulelewa na kukuzwa katika maadili mema ya ucha Mungu,” alisema Muhamed.
Pia alikemea vikali tabia ya watoto wa Kiislamu kuvaa nguo fupi kwa kuwa wanakwenda kinyume na maadili ya dini.
“Inasikitisha kuona watoto wa Kiislamu wakitembea suruali chini ya makalio. Inatia aibu kwa mtoto wa kike anatoka nyumbani akiwa nusu uchi kwa mavazi yake lakini mama anamwangalia bila kuchukua hatua zozote za kukemea na kukataza tabia hiyo,” alisema.
Alisema hiyo si msingi na miongozo ya Mtume Muhammad (S.W.A) na kufanya hivyo ni sawa na kuudhalilisha Uislamu, hivyo aliwataka wazazi kwa pamoja kukemea tabia zisizofaa kwa watoto wao.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment