Mwanamuziki mkongwe wa muziki wa dansi nchini, Kasimu Mapili (kulia), akiimba wakati Rais wa Shirikisho la Muziki Tanzania (TMF), Addo Novembar (kushoto), alipozungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, wakati akilipongeza Bunge la Katiba kwa kuingiza katika katiba vipengele vitatu vinavyolinda maslahi ya wanamuziki.
Shirikisho la Muziki Tanzania (TMF), limeunga mkono rasimu ya mabadiliko ya katiba kwa kile walichodai kuwa kimegusa maslahi yao hivyo wataipigania kwa nguvu zote kuhakikisha inapita.
"Wasanii wamekuwa wakifanya kazi kubwa lakini hawanufaiki na kazi zao, wasanii wa zamani ukiangalia walifanya makubwa kwenye tasnia hii ya sanaa lakini baadhi yao wamekufa ni maskini wa kutupwa, na wengine mpaka sasa wanaishi maisha ya dhiki hayalingani na thamani ya kazi waliyokuwa wanafanya.
"Nchi za wenzetu wasanii wamekuwa wakiishi maisha ya mazuri na kuendesha magari ya kifahari, lakini kwa Tanzania ni tofauti magari ya kifahari yanaendeshwa na wanasiasa, wasanii wananyonywa, tunashukuru katiba hii imetambua haki za wasanii kwa kuingiza vipengele vitatu ambavyo vitalinda maslahi ya wasanii na kuwainua kiuchumi.
Novemba alivitaja vipengele hivyo ni ibara ya 15 (1.e) ambayo inasema kuweka mazingira kwa wasanii kunufaika na kazi zao, ibara ya 38 (iii) inayosema kufanya ugunduzi, ubunifu na utafiti wa sanaa, sayansi na mapokeo ya asili.
"Ibara ya 56 (1) inasema kila mtu atakuwa na uhuru wa kushiriki kwenye mambo yanayoendeleza na kukuza sanaa, taaluma, ubunifu na ugunduzi.
"Kipengele cha (iii) Serikali itakuza na kuendelza utafiti, ubunifu na ugunduzi katika sanaa, sayansi na teknolojia kwa kutunga sheria ambazo zitalinda hakimiliki na haki za wabunifu, watafiti na wasanii.
Novemba alisema Wasanii kutambuliwa kama kundi maalum, sababu zikiwa ukubwa wa kundi hili, ambalo liko katika kila kijiji nchini, na machango wa pato la Taifa la kundi hili ambao kwa mujibu wa ripoti ya WIPO ya 2010, wasanii walichangia asilimia nne ya GDP, na walichangia asilimia tano ya ajira nchini.
"Kitendo cha rasimu hii kuweka wazi katika Katiba umuhimu wa ulinzi wa mali itokanayo na ubunifu 'Intellectual property' sheria ambayo italinda maslahi ya wasanii, tutaipigania kwa nguvu zote tupo tayari kufanya kampeni nchini nzima kuipigania ili ipite, tunaiunga mkono kwa asilimia 100 na kesho (leo) viongozi wenzetu watamsindikiza Rais kuipokea rasimu hiyo.
Aliwataja viongozi wa Shirikisho ambao watamsindikiza Rais Jakaya Kikwete kupokea rasimu hiyo kuwa ni katibu Abdul Salvador, Makamu Mwenyekiti Samweli Mbwana na Mweka Azina Mwinyi Ally.
No comments:
Post a Comment