ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, October 16, 2014

SHOGA, HUKUSHIBA TONGE, UTASHIBA KUJILAMBA?


Haya jamani kama kawaida yangu siku ya leo ikifika mtambaji huwa mmoja, hili si geni kwa vile miluzi mingi humpoteza mbwa. Jamani hivi nitumie mdomo na lugha gani ili wanawake wenzangu mnielewe?
Kwa nini lakini tumekuwa mzigo wa miba hatubebeki, ni kweli mwalimu wetu ni kipofu?

Jamaniii! Mbona tunatia aibu tunafanya mambo hata watoto wana afadhali, ukishaharibu unakimbilia kwa waganga sasa mchawi nani kama siyo mwenyewe.
Kwa kweli nazungumza kwa uchungu, ungekuwa karibu yangu ungeona machozi yanavyonitoka. Juzi nililetewa malalamiko na mwanaume mmoja mtu mzima kwamba mkewe amekuwa mung’unya kaharibika ukubwani.

Kisa na mkasa? Katika miaka zaidi ya thelathini ya ndoa yao, sasa hivi ndo kaliona penzi la nje tamu na kuifanya nyumba iyumbe.

Mtu aliyenieleza namjua ana watoto watu wazima na wajukuu, bwana yule alinieleza kwa uchungu.
“Hivi Anti Naa, nimuache mke wangu uzeeni watu si watasema nina hila?”
Mmh! Hilo nalo neno! Au kama watoto wa sasa watasema ni sheeda. Kwa kweli sikutaka kumjibu mwenyewe, nilifunga safari hadi kwake na kumkuta mwanamke kajaa tele. Kwa vile nammudu nilifungua kesi mbele yao.

Nilimweleza mwanaume ayaseme yote aliyosema kwangu. Naye alirudia yote huku akiongeza na mambo yaliyokuwa ya siri ya mkewe kuondoka bila kuaga au kumpa unyumba siku anayotaka.
“Yanayosemwa juu yako ni kweli?”
“Hata yakiwa kweli wewe yanakuhusu nini?”

Majibu yake yalinichefua na kumweleza maneno ya shombo.
“Shoga kwa vile unakula dona na kushiba ndiyo maana unakuwa na jeuri ya popo kujipaka kinyesi lakini akiachika hakuna wa kukupa hata salamu. Siku zote ukiona kobe juu ya mti ujue kapandishwa acha kujitoa akili na kuzihamishia chini. Nani alikuambia hamu zinaisha kwa kutoka nje ya ndoa?

Shoga ndoa mbaya kwa vile unayo lakini ukiachika utaadhirika na dunia. Kila kitu kina wakati wake kama hukushiba kwenye sahani, utashiba kwa kujilamba? Ujana wote umeswampa hukuridhika utaridhika uzeeni?

Hebu acha kujitoa akili, utu uzima dawa, watoto na wajukuu wanakutegemea wewe, leo hii wanakuona umefumaniwa na mtoto mdogo aibu iliyoje.Acha jeuri ya nazi kushindana na jiwe, heshimu ndoa yako, heshimu umri wako siku zote ukijiheshimu utaheshimiwa, tunza heshima ya mumeo ili kila mmoja mtaani ajifunze kupitia ndoa yako.

Hebu basi jamani wanawake tubadilike, tujifunze kutokana na matukio ya wenzetu, kwa hali inayoendelea nakiri kabisa mwalimu wetu kipofu amefariki, sasa tuna mwalimu mwendawazimu.
Haiingii akilini mwanamke mtu mzima kutoka nje ya ndoa na kutembea na kijana mdogo. Mwingine nilishuhudia akifukuzwa kama mbwa baada ya kufumaniwa na mumewe kwa kuleta mwanaume ndani, jamani hii ni dharau kiasi gani kama nyumba huitaki kwa nini usiondoke kimyakimya kuliko kuondoka kwa aibu?

Narudia, mwanamke anayezipeleka akili zake chini hana tofauti na mnyama anayefanya mapenzi hadharani bila aibu. Jamani hebu tubadilike kwani nani alikufa kwa kukosa kufanya mapenzi na wanaume wengi?

Hebu tutulie ili kuimarisha ndoa zetu, starehe ya siku moja inaweza kuwa aibu ya miaka mia. Nina imani nimeeleweka, kwa leo inatosha tukutane wiki ijayo, ni mimi Anti Nasra Shangingi Mstaafu.

GPL

3 comments:

Anonymous said...

It goes both ways. Wanaume nao ni walaghai sana. Hutafuta nyumba ndogo na kusahau familia zao. Au wengine ni boyfriend and girlfriend then mwanaume anatafuta msichana mwingine name kumdanganya wa kwanza tena anadiriki kutoa maneno ya kashfa kuhusu first girlfriend kwa yule mpya. So wote wake kwa waume tuheshimiane, turpentine name kama tumechokana to call it quit.

Anonymous said...

We mwandishi una maneno matam kweli. Lakini waathirika yanawakolea haya? unawafunda kweli kweli. Naomba uendelee hivi hivi na somo hili kwa jinsia zote. Ni aibu kwa bibie kusoma gazeti tunapokula chakula cha usiku. Inakatisha tamaa sana. Kuchoka gani huko mke wa mtu. Mzee anatengewa chakula na kuambiwa ajihudumie. Kawa nafunua mwenyewe, chumvi,najiwekea nayo. Makubwa haya mkunga wetu. Mabibi tubadilike sana katika faragha

Anonymous said...

Wee muandishi hebu toa na hii story kwa wale wanawake walio athirika kwa wsume zao, wapo kwenye ndoa hawskubahatika mtoto ndani ya miaka 5, mwanaume ana amua kutoka nje ya ndoa na ku bahati ka kupata mtoto, halafu ana mnyanyasa mke wake wa ndoa na kuruhusu hawara amtanbie mke wsje, swala hili una msaidiaje mwanamke anaepitia shida kama hii.