
Kwa mujibu wa habari zilizopatikana kutoka ndani ya uongozi wa Simba, kambi hiyo ya siku 10 imelenga kukiimarisha kikosi cha timu hiyo ili kiweze kufanya vizuri katika mechi dhidi ya Yanga na nyingine za Ligi Kuu ya Soka ya Tanzania Bara ambayo itaendelea tena mwishoni mwa wiki.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa maamuzi ya kuipeleka Simba Afrika Kusini yalifanywa na viongozi wa klabu hiyo kwa kushirikiana na Kundi maarufu la Friends of Simba ambalo mwenyekiti wake ni Zacharia Hanspoppe.
"Katika kuhakikisha timu inarejesha kiwango chake, uongozi na Friends of Simba haukuangalia gharama za kambi," alisema mmoja wa viongozi wa juu wa klabu hiyo yenye makao makuu yake Mtaa wa Msimbazi, Kariakoo jijini Dar es Salaam.
Alisema Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mzambia Patrick Phiri, amefurahishwa na maamuzi ya viongozi kwa kuandaa kambi hiyo ambayo inawabadilisha wachezaji na kuwapa jukumu la kuhakikisha wanapambana kulida 'deni' la ushindi.
"Kikubwa Phiri amefurahia kupata mechi kubwa za kirafiki na timu zinazocheza Ligi Kuu ya Afrika Kusini ambayo ni ligi bora barani Afrika. Tunaamini ushindi utapatikana na tutasahau machungu ya nyuma," alisema kiongozi huyo.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa kipa Hussein Shariff 'Casillas' aliumia mguu juzi wakati wa mechi ya kirafiki dhidi ya Orlando Pirates ambayo ilimalizika kwa sare ya bila kufungana.
Hata hivyo, taarifa za awali zilieleza kuwa kipa huyo atarejea katika hali yake hivi karibuni na ana nafasi kubwa ya kudaka Jumamosi.
RATIBA YA SIMBA
Jana Jumapili timu imefanya mazoezi asubuhi saa tatu (saa nne kwa saa za Tanzania ) mpaka saa saa sita mchana na jioni saa 10 mpaka saa moja usiku.
Leo Jumatatu saa tisa mchana ya Afrika Kusini itaikabili Bidvest Wits United 'The Clever Boys' katika mechi ya kirafiki ya kimataifa itakayofanyika kwenye Uwanja wa timu hiyo iliyoko katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Afrika Kusini.
Kesho Jumanne asubuhi- timu haitafanya mazoezi ya uwanjani lakini wachezaji watafanyiwa 'massage' maalumu kwa ajili ya kunyoosha viungo vyao.
Jumanne mchana- timu itashuka tena dimbani kucheza mechi nyingine ya kirafiki dhidi ya Jomos Cosmos.
"Pia Jumatano tunatarajia kucheza mechi ya mwisho ya kirafiki, kila mechi mwalimu anajaribu kutumia wachezaji wote," kilisema chanzo chetu.
Aliongeza kuwa, wachezaji wa timu hiyo walioko katika timu ya Taifa (Taifa Stars) wataungana na wenzao jijini Johannesburg mapema leo asubuhi.
"Wale walioko Stars watatua huku kesho (leo) saa tatu asubuhi na ndege ya Shirika la Ndege la Afrika Kusini," aliongeza.
Wekundu wa Msimbazi ambao wana pointi tatu mkononi baada ya kucheza mechi tatu na zote kutoka sare, wanatarajia kurejea nchini Ijumaa tayari kuwavaa Yanga wenye pointi sita kutokana na kupoteza mchezo mmoja na kushinda miwili.
CHANZO: NIPASHE
1 comment:
I am a Simba fan, but all those residential training are a waste of money. Mara Pemba and now SA and you end up with draw with a team coached by a local coach. We have imported coaches and players and all we manage is draw and draw and draw. Good luck!
Post a Comment