Dar es Salaam. Mwenyekiti wa lililokuwa Bunge la Katiba, Samuel Sitta amesema hakuwahi kukaa na kuuahidi upinzani serikali tatu.
Sitta alisema hayo jana ikiwa ni siku moja baada ya Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ kukaririwa na gazeti hili akisema kuwa, Sitta aliwasaliti wapinzani baada ya kuwafuata kuomba kura za uenyekiti wa Bunge la Katiba ili atetee serikali tatu lakini baadaye akawageuka.
Katika mchakato wa kumpata mwenyekiti wa Bunge hilo, Sitta ambaye pia alikuwa Spika wa Bunge la Tisa, alionekana kukubalika na pande zote; chama chake cha CCM na wapinzani jambo lililomfanya kushinda kiti hicho kirahisi kwa kupata asilimia 86.5 dhidi ya mpinzani wake Hashim Rungwe aliyepata asilimia 12.3.
Sugu alisema Sitta alimfuata na kumwomba ampigie debe kwa vijana ili akishinda atekeleze pamoja na mambo mengine, madai ya serikali tatu yaliyotolewa na wajumbe wa upinzani.
Akizungumzia suala hilo Sitta alihoji, “Sugu ni mtu gani kwangu mimi hata nimtafute? Nikitaka kuongea na Chadema nitamtafuta (Freeman) Mbowe au (John) Mnyika na si Sugu, hata sijui tulikutana wapi na yeye,” alisema Sitta.
Sitta ambaye pia ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki alisema hakuwahi kumwahidi mtu yeyote kitu chochote wakati wa kampeni zake ya kuwania uenyekiti wa Bunge hilo la Katiba.
“Mimi ni mtu wa kujitegemea na kusimamia haki na ndicho nilichofanya, sasa hayo anayosema huyo sijui katoa wapi,” alisema Sitta na kuongeza: “Nakanusha vikali kuhusu suala hilo analosema Sugu.”
Alisema kuna wabunge kama (Joshua) Nassari ambao walikuwa wanakubali sera zake na hivyo kumpigia kampeni za kuwania nafasi hiyo ya kuongoza Bunge la Katiba lakini si kama anavyosema Sugu hivi sasa.
Sitta alisema ni muhimu wapinzani wakaacha kupiga kelele na badala yake wasubiri Kura za Maoni ya Katiba Inayopendekezwa.
“Tusubiri Kura ya Maoni ndiyo waseme huko na si kupindisha mambo kwa kuwa wanaongea tu vitu ambavyo havipo,” alisema Sitta.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment