Advertisements

Wednesday, October 22, 2014

Tanzania inahitaji walimu laki nne ifikapo mwaka 2030

Hii ni moja ya nyumba za Walimu wa shule ya Msingi Mihuga iliyopo Wilayani Bagamoyo. mazingira ya namna hii yanasababisha walimu wengi kuikimbia fani yao ya ualimu. Picha na Ibrahim Yamola.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, (UNESCO) hivi karibuni limetoa ripoti inayoonyesha Tanzania itahitaji angalau walimu 406,600, ifikapo mwaka 2030.
Wakati mahitaji ya walimu katika nchi mbalimbali yakizidi kuwa makubwa, shirika hilo linasema uhaba wa walimu wenye mafunzo unazidi kutamalaki katika nchi mbalimbali, ikiwamo Tanzania.
Kwa sasa na inawezekana na baadaye, Afrika ndiyo inayoongoza kwa kuwa na uhaba mkubwa wa walimu, jambo linalohatarisha mustakabali wa sekta ya elimu barani humu.
Ukiondoa Tanzania, ripoti hiyo inaonyesha mahitaji makubwa ya walimu pia yanazikabili nchi kadhaa za Afrika, zikiwamo Uganda, Nigeria na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Kwa ngazi ya dunia ripoti hiyo inasema hadi mwaka huo, walimu zaidi ya milioni 27 watahitajika kuziba mapengo ya walimu wanaostaafu na nafasi mpya za ajira.
Hata hivyo, taarifa nzuri ya ripoti hiyo inaonyesha kama Tanzania itajipanga vizuri, inaweza kuziba pengo la walimu , hasa katika shule za msingi ifikapo mwaka 2026. Hilo linawezekana ikiwa nchi hiyo itakuwa inaajiri angalau asilimia 10 ya walimu kila mwaka.
Hata hivyo, Unesco inasema mikakati ya kuziba mianya hiyo ya walimu katika nchi nyingi imegubikwa na dosari kubwa kwa vyombo husika kuajiri walimu wasio na mafunzo bora ya ualimu.
“Takwimu zinaonyesha kuwapo kwa tatizo sugu la walimu wasio na mafunzo katika nchi nyingi. Kama hatua hazitochukuliwa, itakuwa vigumu kwa watoto wote kwenda shule na kujifunza,” inasema taarifa ya Unesco iliyotolewa kwa umma.
Sababu za uhaba wa walimu
Takwimu za Unesco zimetolewa wakati ambao kila mdau anapozungumzia maendeleo ya elimu, hakosi kutaja uhaba wa walimu kama moja ya changamoto tete zinazoikabili sekta hiyo nchini.
Walimu na wakuu wa shule wanalia na uhaba wa walimu, wadau wanalalamika, Serikali nayo inakiri kuwa walimu ni tatizo nchini.
Kwa nini Tanzania iwe na uhaba mkubwa wa walimu? Mwalimu mstaafu, Bakari Kheri, anasema uhaba wa walimu ni jambo la kujitakia.
Anasema mosi, Serikali imekuwa ikibuni mipango inayolenga kuongeza wanafunzi na shule bila kuzingatia mahitaji ya walimu waliopo au itakayowaajiri.
“Jambo la pili, hao waliopo na wengine wakiwa wamesomeshwa na Serikali, wanakimbia kazi hiyo kwa sababu ya masilahi madogo na pia kufanya kazi katika mazingira magumu,” anasema na kuongeza:
“Viongozi wa Serikali wanasema ni jambo gumu kuwaridhisha walimu, eti kwa kuwa wako wengi, ukweli siyo wingi wa walimu bali kutumia rasilimali za nchi kwa kutozingatia maeneo ya vipaumbele kwa Taifa kama kuwahudumia walimu.
Kwa sababu ya fani hiyo kukabiliwa na matatizo mengi, kama masilahi madogo hasa mishahara, walimu wengi wamekuwa wakikimbia fani..
Ripoti ya HakiElimu kwa kushirikiana na chama cha walimu, inasema zaidi ya asilimia 45 ya walimu shuleni wako tayari kuacha ualimu na kwenda kufanya kazi nyingine.
“Walimu wengi wanahisi hadhi yao ni ndogo katika jamii kwa sababu wanalipwa mishahara midogo, mishahara hii midogo ndiyo inayowazuia wanafunzi wenye ufaulu mzuri kujiunga na taaluma ya ualimu.’’ inasema ripoti hiyo iitwayo ‘Hali ya kazi na maisha ya walimu Tanzania’.
Ripoti inaongeza kusema kuwa walimu wengi waliohojiwa wanasema ualimu ulikuwa chaguo la mwisho. Hii inamaanisha walisoma na kukubali kuwa walimu kwa kuwa shingo upande.
“Kwa jumla, kiasi cha theluthi moja ya walimu, walisema wangetafuta kazi nyingine kama kungekuwa na uwezekano wa kufanya hivyo. Asilimia 40 walisema hawangewashauri watoto wao kufanya kazi ya ualimu,’’ inabainisha zaidi.
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa anakiri kuwapo kwa uhaba wa walimu katika shule za msingi na sekondari.
Akisoma Hotuba ya Bajeti ya Wizara yake kwa mwaka wa fedha wa 2014/2015 mjini Dodoma, alisema baada ya jitihada za kuajiri walimu wapya, kwa sasa nchi inakabiliwa na uhaba wa walimu 30,949 wa shule za msingi na 24,596 kwa shule za sekondari.
“Wizara na wadau wake wataendelea kuwaandaa walimu kulingana na mikakati na kadri rasilimali zinazohitajika zinavyoendelea kupatikana,’’ alieleza.
Kwa mujibu wa Kawambwa, tatizo zaidi liko kwa walimu wa sayansi na hesabu. Anasema mahitaji halisi ya walimu wa masomo hayo ni 48,407, lakini waliopo ni walimu 21,409.
Mikakati kadhaa inatekelezwa na Serikali kuongeza idadi ya walimu na kuhakikisha waliopo hawakimbii vituo vya kazi au kuacha kabisa kazi ya ualimu.
Kwa mfano, kuhusu walimu wanaokimbia kwa sababu ya kupangiwa katika maeneo magumu na hatarishi, wizara imetoa ahadi ya kutoa motisha ya fedha kiasi cha Sh500,000 kwa kila mwalimu anayepangiwa katika maeneo hayo.
Ahadi hiyo aliitoa Dk Kawambwa alipozungumza bungeni Novemba 8 mwaka 2011, ikiwa ni utekelezaji wa awamu ya pili ya Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (MMES).
Kuhusu kuajiri walimu wenye mafunzo kama inavyopigiwa debe na Unesco, anasema Serikali inaimarisha vigezo vya ufaulu kwa waombaji wa masomo ya ualimu.
Anasema kwa sasa ili mwombaji ajiunge na mafunzo ya ualimu kwa ngazi yoyote, kigezo cha chini kitakuwa ni ufaulu wa daraja la tatu katika elimu ya sekondari.
Mkakati mwingine anautaja kuwa ni: “Kuweka utaratibu wa kuanza kutoa ruzuku na mikopo kwa wanachuo wenye sifa watakaojiunga na mafunzo ya stashahada ya ualimu wa sayansi na hisabati ili kuwavutia wale wenye ufaulu wa juu.”
MWANANCHI

1 comment:

Anonymous said...

CCM NA UONGOZI MZIMA MPO HAPO JAMANI?? BUNGENI MMECHAKACHUA KATIBA MKALA HELA KIBAO HAWA WAALIMU WANAISHI HIVI HAKI HIYO. JE HUU NI UUNGWANA?? NAULIZA!