Advertisements

Friday, October 24, 2014

Tume ya Uchaguzi mtegoni

Balozi Ombeni Sefue.

Wakati Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) ikitarajiwa kuzungumza na vyombo vya habari jijini Dar es Salaam leo, inakabiliwa na mtihani mgumu juu ya muda wa kufanyika kwa kura ya maoni ya kupitisha au kukataa Katiba pendekezwa iliyokabidhiwa kwa Rais Jakaya Kikwete Oktoba 8, mwaka huu.

Ingawa kwa nyakati tofauti Nec imekuwa na msimamo kwamba kura ya maoni haitafanyika kabla ya kuboreshwa kwa daftari la wapiga kura, kauli ya Rais Kikwete aliyoitoa juzi akiwa nchini China kwamba kura hiyo itapigwa Aprili mwakani, imezidi kuiweka Nec mtegoni.

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Nec, Julius Malaba, alisema jana kwamba, leo tume hiyo itazungumza na waandishi wa habari na miongoni mwa mambo yatakayozungumzwa ni suala la kura ya maoni.

UTITIRI WA MITIHANI KWA TUME
Baadhi ya mambo yanayoonekana kukwamisha kura ya maoni ni utaratibu uliowekwa na sheria katika kuratibu zoezi zima ambao unataka mambo kadhaa yakamilike kabla ya kura yenyewe.

La kwanza, ni uboreshaji wa daftari la kudumu la wapigakura ambalo Nec kupitia Mwenyekiti wake, Jaji Mstaafu Damian Lubuva, imekaririwa ikieleza kuwa huenda likaanza kuboreshwa Januari mwakani kwa sababu haina fedha za kufanya kazi hiyo kwa sasa.

Sheria pia inaeleza kuwa siku saba baada ya Katiba pendekezwa kuchapishwa kwenye Gazeti la Serikali na Rais kuipa Nec kazi ya kuanza mchakato, itatunga swali ambalo litajibiwa na wapigakura.

Hatua hiyo itafuatiwa na elimu kwa umma, ambayo itaendeshwa na Nec kwa kushirikiana na asasi za kiraia, ambayo inatakiwa kutolewa kwa muda usiopungua miezi miwili na baadaye Nec kutangaza utaratibu wa kampeni.

Baada ya takribani miezi miwili ya elimu kwa umma, Nec itatakiwa kuunda kamati mbili za kitaifa na kwenye majimbo ambazo moja itakuwa inapinga Katiba pendekezwa na nyingine inaikubali; na zitatakiwa kufanya kampeni kwa mwezi mmoja.

Mbali ya kazi hiyo kubwa ya kuratibu kura ya maoni, Nec inakabiliwa na jukumu lingine la kuendesha uchaguzi wa serikali za mitaa uliopangwa kufanyika Desemba, mwaka huu nchi nzima.

Kadhalika, Aprili kuna Mkutano wa Bunge la Bajeti ya Serikali ambalo hufanyika hadi Juni, likifuatiwa na mchakato wa uteuzi wagombea wa nafasi mbalimbali ndani ya vyama vya siasa na kampeni kwa ajili ya uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba mwakani.

Hata hivyo, akizungumza na NIPASHE juzi, aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, alisema haoni uwezekano wa kuamua kura ya maoni sasa kwa kuwa hivi sasa Nec inakabiliwa na jukumu la kuandaa uchaguzi wa serikali za mitaa na kwamba haiwezi kufanya kazi nyingine kwa ufanisi.

Alisema kwa mazingira hayo, inategemewa itaanza kuandikisha wapigakura baada ya kumalizika uchaguzi huo na kwamba, hata ikianza Januari na Februari, mwakani, ikimaliza lazima kuwapo na kipindi cha kutosha kwa elimu kwa umma.

“Haiwezekani mwezi wa tatu kuwa na kura ya maoni. Kwa vyovyote hata ingekuwa hivyo, mwezi huo siyo mzuri wa kupiga kura. Ni wakati wa mvua. Wananchi wanashughulika na mashamba yao. Kwa kawaida upigaji kura unapangwa ili wananchi wapate nafasi. Ukiwapangia kipindi cha mvua, wana shughuli nyingi. Itakuwa vigumu kwa wananchi wote kushiriki. Kwa hali tuliyonayo, lazima tuangalie sheria, ifanyiwe marekebisho ili shughuli zote, hasa elimu kwa umma ipate nafasi ya kutosha.”

Badala yake, Jaji Warioba alisema ni vizuri serikali ikafanya jitihada kubwa ya kusambaza katiba inayopendekezwa ili wananchi wapate nafasi ya kuisoma kwa kina.
Jaji Warioba alisema Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilipewa miezi 18 na kuongezewa miwili, BMK lilipewa siku 70 na kuongeza siku 70 na nyongeza ya siku 20 na lilitumia mara mbili ya muda uliotengwa katika Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.

“Kwa wananchi ni muhimu zaidi kupata nafasi. Tusilifanye jambo hilo kwa kulipua. Ni jambo zito. Wananchi lazima wapewe nafasi ya kutosha kuelewa nini wanakipigia kura,” alisema Jaji Warioba. Alisema hata kama ni mapema, ifanyike Juni au Julai, mwaka 2015, muda ambao maandalizi yamekamilika na wananchi hawana shughuli za shamba.

“Lakini tujue mwakani ni uchaguzi mkuu. Ukiwa na mlolongo wa uchaguzi, Desemba, Juni na Oktoba, lazima wananchi watachoka,” alisema Jaji Warioba.

Aidha, wananchi wengi wameilalamikia Nec kwamba haina sifa kwa sasa kusimamia kura ya maoni kwa kuwa haiko huru; hivyo ilitegemewa kwamba ingefanyiwa marekebisho kabla ya zoezi hilo.
Hata Mwenyekiti wake, Jaji Lubuva, amekuwa akikiri kwamba tume yake siyo huru kuweza kusimamia chaguzi nchini.

MAKUBALIANO YA JK NA TCD
Mbali ya msururu wa majukumu yanayoikabili Nec hivi sasa, msimamo wa kutaka kura ipigwe Aprili mwakani unakiuka makubaliano kati ya Rais Kikwete na viongozi wa vyama vya siasa waliokutana mjini Dodoma Septemba 8, mwaka huu chini ya mwavuli wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD).

Miongoni mwa makubaliano hayo ni Katiba ya sasa ya mwaka 1977 kufanyiwa marekebisho ili kuweka mazingira mazuri ya kuufanya uchaguzi mkuu wa mwakani uwe huru na haki.

Mambo yaliyokubaliwa kufanyiwa marekebisho ni kuudwa kwa tume huru ya uchaguzi, mshindi wa uchaguzi wa Rais ashinde kwa zaidi ya asilimia 50, matokeo ya uchaguzi wa Rais yaruhusiwe kupingwa mahakamani na kuruhusu mgombea binafsi katika uchaguzi mkuu ujao.

Kwa mujibu wa makubaliano hayo kati ya TCD na Rais Kikwete, Rais ajaye ndiye atakayehitimisha mchakato wa Katipa pendekezwa.

Mwenyekiti wa TCD, John Cheyo, alieleza kuwa kutokana na makubaliano hayo, marekebisho ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 yatalazimika kufanyika kwenye Mkutano wa Bunge wa Novemba, mwaka huu au wakichelewa ni Bunge la Februari 2015.

KAULI YA KATIBU MKUU KIONGOZI
Pamoja na changamoto hizo, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue (pichani), amesema serikali haihitaji muujiza kufanikisha kura ya maoni kuhusu Katiba pendekezwa Aprili, mwakani kwa kuwa inajipanga vilivyo kuhakikisha kazi hiyo inafanikiwa.

Akizungumza na NIPASHE jana, Balozi Sefue alisema tayari Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imekwishatangaza Katiba pendekezwa kwenye Gazeti la Serikali kwa tangazo namba 382, la Oktoba 10, 2014.

Balozi Sefue alisema serikali inatambua kuna majukumu mengi na mazito yanayoikabili nchi hivi sasa ukiwamo uchaguzi wa serikali za mitaa uliopangwa kufanyika Desemba, uboreshaji wa daftari la wapigakura, elimu kwa umma na kampeni kuhusu Katiba pendekezwa, Mkutano wa Bunge la Bajeti wa Aprili na mchakato wa uchaguzi mkuu mwakani, lakini itajipanga kuhakikisha yote yanafanyika.

“Ni kweli mambo ni mengi, lakini tukijipanga vizuri itawezekana. Wala siyo muujiza; na sasa tupo katika kujipanga vizuri ili mambo yawezekane,” alisema Balozi Sefue.
CHANZO: NIPASHE

No comments: