ANGALIA LIVE NEWS

Friday, October 17, 2014

UHISPANIA NA UTURUKI WACHUANA VIKALI NAFASI YA UJUMBE USIO WA KUDUMU WA BARAZA KUU LA USALAMA LA UMOJA WA MATAIFA

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uhispania, Bw. Jose Manuel Garcia Margallo akifuatillia duru ya tatu ya Uchaguzi wa wajumbe wasio wakudumu wa Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa katika uchaguzi uliofanyika siku ya Alhamisi ambapo nchi yake ilichuana vikali na Uturuki ambapo hatimaye Uhispania iliibuka kidedea kwa kupata kura 132 dhiti ya Uturuki na hivyo kuungana na Angola, Venezuela, New Zealand na Malayasia watakaokuwa wajumbe wasio wa kudumu wa Baraza hilo kuanzia Januari Mosi 2015 wakichukua nafasi za wajumbe wanaomaliza muda wao wa miaka miwili ambao ni Rwanda, Jamhuri ya Korea ya Kusini, Argentina, Australia na Luxembourg. Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa ndiyo lenye dhamana ya kusimamia masuala ya amani na usalama wa Jumuiya ya Kimataifa kwa mujibu wa Katiba ya Umoja wa Mataifa. Baraza linakuwa na wajumbe 15 ambapo watano ni wakudumu na wenye kura ya veto na kumi wasio wakudumu na ambao huchaguliwa kwa mgawanyo wa kikanda

Na Mwandishi Maalum, New  York
Wajumbe wa Baraza Kuu la  Umoja wa  Mataifa ,  jana  Alhamisi waliwapigia kura ya siri wajumbe  watano wasio wa kudumu watakaojiunga na  Baraza  Kuu la Usalama la  Umoja wa Mataifa   kuanzia  January Mosi 2015.
Mataifa yaliyokuwa yanawania  nafasi hizo kwa kuzingatia  mgawanyo wa Kikanda ni nafasi moja kutoka nchi za Afrika,  ambayo kwa  sasa inashikiliwa na Rwanda, nafasi moja kwa kundi la nchi za Asia na Pacific ambayo   kwa sasa inashikiliwa na  Jamhuri ya Korea ya Kusini, nafasi moja   kwa kundi  la nchi za Latini ya Amerika na Visiwa  vya Karibian nafasi ambayo kwa sasa inashikiliwa na Argentina na viti viwili kwaajili ya nchi za Ulaya ya  Magharibi na nchi nyinginezo, nafasi ambayo kwa sasa inashikiliwa na  Luxembourg na Lithuania mbayo inatarajiwa kuachia nafasi hiyo mwakani ikiwa ni nafasi ya  kundi la nchi za Ulaya Mashariki.
Katika  duru ya kwanza  ya uchaguzi huo  Angola,   New  Zealand, Malaysia   na Venezuela ziliibuka  kidedea  kwa kupita bila kupingwa  huku mchuano mkali  ukibakia kwa  Uhispania na Uturuki.
Kila muwania  nafasi hiyo alihitaji ushindi wa theluthi  mbili za wingi wa kura zilizohitajika, kura ambazo katika duru ya kwanza  na ya pili ya uchaguzi kura za  Uturuki na Uhispania  hazikutosha na hivyo kuwalazimu kurudia kwa mara ya tatu duru ambayo  Uhispania iliibuka kidedea kwa kupata kura 132.
Wajumbe hao wataungana na wajumbe wengine watano   wa kudumu wenye kura ya veto ambao ni Marekani,  Urusi, Uchina,  Uingereza na Ufarasa. Pamoja na wajumbe hao watano wa kudumu wajumbe wengine watakaoendelea   hadi mwishoni mwa  2015 ni Chad,  Chile, Jordan na  Nigeria na hivyo kufanya idadi ya wajumbe  wa Baraza  Kuu la  Usalama kuwa 15. Kumi kati yao wakiwa hawana dhamana ya kura ya Veto.
Baraza  Kuu la  Usalama la Umoja wa  Mataifa ndilo limekasimiwa jukumu la masuala yote yanayohusu Amani na  Usalama wa Kimataifa kwa Mujibu wa    Katiba  ya Umoja wa  Mataifa

No comments: