ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, October 21, 2014

UNAMWACHA, UNADAI KILA ULICHOMNUNULIA!-2

WIKI iliyopita katika makala haya tuliishia kwenye wanawake wengi wanasema kuwa, mapenzi ya sasa, mwanaume hata akikununulia gari kuwa nalo makini kwani wengi wanaweza kukupa kadi feki, siku akikumwaga anachukua gari lake kiulaini kabisa.
Wiki hii tunaendelea

WANAUME NAO!
Nilibahatika kuzungumza na baadhi ya wanaume kuhusu madai hayo, wengi walisema ukikuta mwanaume anamnyang’anya vitu mwanamke kwa sababu wameachana, ujue mwanamke huyo kasaliti.

“Nataka niseme hivi! Mwanaume akimchoka mwanamke na akaamua kummwaga, hamnyang’anyi kitu chochote, kwanza hata mwanaume mwenyewe anaweza kutopenda kukutana na mwanamke huyo aliyemmwaga.

“Ila sasa, wengi wananyang’anywa kwa sababu kuu moja, usaliti! Utakuta mwanamke unamnunulia nguo, unampa pesa ya saluni, vipodozi, anapenda. Lakini siku ya siku unagundua kuna mwanaume mwenzako anakula sahani moja na wewe.

“Ndipo wanaume huamua kunyang’anya vitu vyake akiamini kule kumpendezesha kumemfanye wanaume wengine wamuone na kumtongoza.”

“Ile ni hasira kubwa inayoambatana na wivu, unampendezesha kumbe na yeye anatumia nafasi hiyo kuwakubali wanaume wengine. Tena unaweza kukuta kabla yako walikuwa wanampita tu.

“Wanaume hufanya tabia hiyo kwa wanawake wasaliti tu. Na dawa ya usaliti ni hiyo, kinyume cha hapo hakuna mwanaume anayeweza kumnyanga’anya vitu mwanamke. Hasa kama anamwacha yeye mwenyewe,” alisema Mackey, mkazi wa Mbagala ya Maji Matitu jijini Dar.

WANA HOJA?
Je, wanaume wanaodai wanafanya hivyo kwa sababu wanawake wamesaliti wana hoja?
Inawezekana wana hoja lakini dhaifu, kwa sababu mwanamke kusaliti hakuna uhusiano na vitu alivyonunuliwa na mwanaume. Unajitegemea. Kinachotakiwa kwa wanaume ni kuangalia, je wakati akiwa naye, yaani kabla hajagundua usaliti si alikuwa anamtumia?

NI BUSARA?
Katika hali ya kutofikiri sana, baadhi ya wanaume wanaweza kusema ni busara sana. Haiwezekani asumbuke kutafuta pesa, amnunulie mwanamke nguo siku ya kuachana amwachie, lazima achukue kila kilicho chake kwa kuwa mkataba umekwisha!

Lakini kwa upande mwingine, busara kama hizo ni ‘ziro’ kama siyo sifuri! Inawezekana vipi uchukue vitu kwa mwanamke kisa ulimununulia? Kwani wakati unamnunulia si alikutendea ya kukuvuta ndiyo maana ukawa huoni tabu ‘kulala ubavu’ na kuchomoa waleti ili kutoa mshiko na kumpa.

MTAZAMO WANGU
Namalizia kwa kusema kuwa, kwa wanawake au wanaume ni vyema kukaa chini wakati wa kuachana kuzungumza kwa undani ili kunusuru hatua ya kuachana hivyo kila mmoja kuwa na amani na mwenzake. Lakini ikifikia hatua ya kuachana, wanaume hawana budi kuachana na vitu pia, ulitoa kwa moyo viache kwa moyo ili isionekane ulitoa kwa mkopo ukataka kurejeshewa! Si poa!

GPL

No comments: