Advertisements

Saturday, October 18, 2014

Urais 2015:Rushwa yajikita Nec CCM

  Takukuru yazungumza, yaahidi kufuatilia
  Nape asema inachangia kukichafua chama
Rushwa iliyokithiri inadaiwa kutolewa kwa baadhi ya wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanaoshiriki kikao kilichomalizika jana, mjini Dodoma.

Vitendo hivyo vinadaiwa kuanza mwanzoni mwa wiki hii, vikiwahusisha pia baadhi ya Makatibu wa CCM waliokutana mjini hapa kutoka mikoa yote nchini.

Rushwa hiyo inadaiwa kufanywa na waratibu wa baadhi ya mitandao ya wanaotajwa kutaka kuwania Urais katika Uchaguzi Mkuu, mwakani.

Hata hivyo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, amesema bado hajazipata taarifa hizo, ingawa alithibitisha kuwa uwapo wake unaweza kuchangia kukichafua chama hicho.

Nape, alisema katika mazingira kunapofanyika kikao cha Nec, si rahisi kuwapo vitendo hivyo isipokuwa kama vinatendeka nje ya mazingira ya kikao, ni vigumu kwake kuzungumzia.

“Sasa hivi ninashughulikia kikao cha Nec kinachofanyika humo ndani (ukumbini) na ni vigumu rushwa kuwapo huko”, alisema. Labda kama wanafanyia kwenye hoteli walizofikia, tena wakati wa usiku tukiwa tumelala, hatuwezi kujua”, aliongeza kusema.

Nape, alisema CCM inahitaji ushirikiano katika kupata taarifa zinazohusu vitendo hivyo kwa maelezo kuwa vinakichafua chama hicho.

Uchunguzi uliofanywa na NIPASHE umebaini kuwapo waratibu hao wakiwamo wa ‘mgombea’ mmoja anayetajwa kuwa na nguvu kubwa ndani ya chama hicho.

Waratibu hao ambao hawakupatikana kuthibitisha au kukanusha madai hayo, kutokana na kushiriki kikao cha Nec, ni waziri mwanamke, wabunge wawili mmoja akiwa ni mhamasishaji wa CCM na mwingine anayetokea mkoani Kigoma.

Pia kiongozi mmoja wa CCM aliyewahi kuhudumu mkoani Dar es Salaam, anaelezwa kuwajibika katika kuwapeleka wajumbe wa Nec ili wakalipwe na ‘mratibu’ ambaye ni waziri.

Kwa mujibu wa utafiti huo, wajumbe waliolengwa zaidi ni wale walioonyesha nia ya kuhamia kwenye mtandao unaomuunga mkono Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.

Mgawo wa rushwa katika kashfa hiyo unaelezwa kufanywa kwa makundi yenye wahusika tofauti, ambao wanasimamia utekelezaji wake kwa siri.

Makundi hayo ni lile linaloongozwa na Waziri mwanamke, Mbunge ambaye pia ni mhamasishaji wa CCM na aliyewahi kuwa Mbunge wa moja ya majimbo ya mkoani Shinyanga.

Hata hivyo, wahusika (majina yanahifadhiwa) wa kadhia hiyo hawakupatikana kuzungumzia madai hayo.

Kashfa hiyo inaelezwa kuwa wajumbe wa mikoa ya kusini mwa nchi ikiwamo Ruvuma, walipokea rushwa hiyo kupitia kwa Mbunge aliyemhamasishaji wa chama huku wale wa kanda ya ziwa walipewa na aliyewahi kuwa Mbunge mkoani Shinyanga.

Taarifa zinaeleza kuwa kiasi cha Shilingi milioni moja (1,000,000) kilitolewa kwa kila mjumbe mlengwa ili kumuwezesha ‘mgombea’ wao kuwa na uhakika wa kupata kura zaidi ya 190 kati ya wajumbe 370 wa Nec huku ikielezwa kuwa lengo kuu la mpango huo lilikuwa kupata wajumbe 230.

Hata hivyo, baadhi ya wajumbe waliopokea rushwa hiyo kutoka kwa mbunge muhamasishaji walielezwa kulalamika kupunjwa kwa kupewa Sh. 700,000 hali inayodaiwa kutia dosari mchakato huo haramu.

Mbali na mtandao huo, inaelezwa kuwa ‘mgombea’ mmoja ambaye pia ni mbunge wa majimbo ya kanda ya ziwa, mwanzoni mwa wiki hii, alikutana na makundi ya makatibu wa CCM kwenye hoteli ya Dodoma.

“Huyu jamaa amekutana na makatibu wa CCM mara nyingi katika kile kinachoeleza kuwa ni ‘kuwakamata’ ili wasijiunge na kambi ya Pinda,” kilieleza chanzo chetu.

Tangu alipotangaza nia ya kuwania urais, Pinda amebadili upepo wa mbio za kuelekea Ikulu ikisadikiwa amesambaratisha mitandao mingine ya wanaoutaka wadhifa huo.

Hali hiyo inadaiwa kuwa kichocheo kwa mitandao inayowaunga mkono wanaotaka kuwania urais kupitia CCM, ni matumizi makubwa ya rushwa tofauti na Pinda ambaye makundi ya kumuunga mkono yalianza kuundwa hata bila yeye kufahamu, wakati wa vikao vya Bunge Maalum la Katiba, vikiendelea.

Makundi hayo yaliyohusisha baadhi ya Wabunge wa Bunge la Muungano na wale wasiokuwa wabunge ambao walikuwa wajumbe wa BMK, yalijipanga kikanda katika kilichoelezwa kuwa ni kuhakikisha jina la Pinda linapitishwa na vikao vya maamuzi vya chama hicho, kupeperusha bendera yao kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Ilielezwa na mmoja wa wanamtandao huo ambaye ni mbunge wa moja ya majimbo ya kanda ya ziwa kuwa, Pinda ni jina lisilo na mazonge mengi ambalo halitawatoa jasho kulinadi kwa Watanzania ili kukipatia ridhaa chama chao kuongoza nchi kwa awamu nyingine.

Akizungumzia madai ya rushwa miongoni mwa wana CCM, Mkuu wa Taasisi ya Kudhibiti na Kupambana na Rushwa (Takukuru) wa mkoa wa Dodoma, Emma Kuhanga, alisema hakuwa na taarifa hizo lakini aliahidi kulifanyia kazi suala hilo.

“Hatujapa madai hayo lakini kutokana na swali lako tunalichukulia kama taarifa ya kuanza kufanyia kazi, mapema iwezekanavyo” alisema Kuhanga.

NEC yaagiza serikali kununua mahindi ya wakulima
WAKATI Huo huo, Waandishi Jacqueline Massano na Paul Mabeja kutoka Dodoma wanaripoti kuwa, Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (NEC), imeiagiza serikali kununua mahindi yote ya wakulima badala ya kuwaachia mawakala ambao wanaonekana kuwanyonya wakulima nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini hapa mara baada ya kumalizika kwa kikao cha siku mbili cha NEC, Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alisema halmashauri hiyo iliiagiza serikali kuongeza juhudi za ununuzi wa mahindi na mazao mengine ambayo wananchi wamezalisha kwa wingi.

“Tulijadili tatizo la soko la mahindi, wananchi wamejitahidi na CCM inawapongeza wamelima mahindi mengi sana, lakini maeneo mengi hasa ambayo Katibu Mkuu, Abdulrahman Kinana alipita kufanya ziara wameripoti wananchi wakilalamika kutokuwepo kwa soko zuri la mazao.

“Ili wananchi wasipate hasara katika mahindi, NEC imeagiza serikali kuangalia suala hili na kuchukua hatua badala ya kuwaachia mawakala ambao kwa sehemu kubwa wamekuwa wakilalia wakulima kwa kuwapa bei ambao inawanyonya,” alisema.

Kuhusu uchaguzi wa serikali za mitaa, alisema NEC imejadili na kuweka mikakati ya namna ambavyo CCM kitashiriki katika uchaguzi huo.

“Tumejadili, mikakati, mbinu na kujiweka tayari kwa ajili ya kushinda… tunaingia katika uchaguzi huu tukiwa na uhakika wa ushindi wa asilimia 91 hivi, tunaamini safari hii pia katika uchaguzi wananchi watatuamini na watatupa kura nyingi za kutosha,”alisema.

Alisema CCM ipo tayari kwa ajili ya uchaguzi huo na wana uhakika wa kushinda kwa asilimia kubwa kama walivyokuwa wakifanya kwenye chaguzi mbalimbali.

Kwa upande mwingine, alisema NEC imepitisha sera na mikakati ya kudumu ya kuhakikisha chama hicho kinajitegemea katika ngazi zote bila ya ruzuku ya serikali.

“Mwenyekiti wa CCM aliahidi kuwa chama kitahakikisha kinatengeneza sera na mikakati ya kujitegemea, ili kupunguza na kuachana kabisa na kukiendesha chama kwa kutumia ruzuku,” alisema. Aliongeza kuwa NEC ilijadili na kupitisha kanuni za Shirikisho la wanafunzi wa vyuo vikuu nchini.
CHANZO: NIPASHE

No comments: