ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, October 9, 2014

Wanafunzi Njombe wateketeza bweni

Mkuu wa Shule ya Sekondari Njombe, Bernard William akimwonyesha bweni lililoungua moto Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Fulgence Ngonyani.Picha na Shaban Lupimo

Njombe. Shule ya Sekondari ya Wavulana Njombe (Njoss) iliyoko mjini hapa, imefungwa kuanzia jana hadi Novemba 8, mwaka huu, baada ya wanafunzi kuchoma moto bweni, karakana na kuharibu mali mbalimbali za shule na walimu.
Wanafunzi hao wanadaiwa pia kuharibu majengo ya Shule ya Msingi Kilimani iliyo karibu na shule hiyo.
Uamuzi wa kuifunga shule ulitolewa jana na Ofisa Elimu wa Mkoa wa Njombe, Said Nyasiro baada ya kufika katika eneo la tukio akiwa ameambatana na Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Sarah Dumba na Ofisa Elimu wa Shule za Sekondari wa Halmashauri ya Mji wa Njombe, Venance Msungu na kufanya kikao cha ndani na walimu.
Nyasiro aliagiza kila mwanafunzi arudipo shuleni hapo, aende na Sh 150,000 kwa ajili ya kufidia hasara iliyopatikana na wanafunzi wote 1,000, waambatane na wazazi wao. Tukio hilo lilitokea saa 5 usiku wa kuamkia jana.
Polisi walilazimika kutumia mabomu ya machozi kwa zaidi ya saa mbili ili kuwatuliza, huku wakazi wanaoishi jirani na shule wakiwa wamejawa hofu kutokana na milio ya mabomu iliyokuwa ikirindima.
Polisi waliokuwa katika eneo la tukio, walisema hali ingekuwa mbaya zaidi kama wasingewahi kufika.
Mbali ya kuchoma moto bweni na karakana, walianza kuvamia nyumba za walimu na kuharibu mali zao.
Inadaiwa kuwa walichoma pia gari la mwalimu wa taaluma ambaye jina lake halikufahamika mara moja na kisha kuvunja duka lake na kuharibu vitu mbalimbali kabla ya kuvamia nyumba ya mkuu wa shule, Bernard William na kuvunja vioo vya madirisha.
Inadaiwa wanafunzi hao walifikia hatua hiyo kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kutaka kuushinikiza uongozi wa shule uwarudishe wenzao 30 waliosimamishwa masomo kutokana na utovu wa nidhamu.
Mkuu wa shule hiyo, William alisema bweni hilo lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 102, limeteketea lote na mali zilizokuwamo ndani. Alisema uharibifu huo unawaongezea gharama nyingine ya ukarabati kwani wakati tukio hilo linatokea, shule ilikuwa inafanya ukarabati wa bweni lingine lililoungua moto hivi karibuni.
Alisema chanzo cha wanafunzi kufikia uamuzi huo ni kudai kuonewa kwa wenzao 30 waliosimamishwa masomo kutokana na utovu wa nidhamu, ambapo 29 kati ya hao wanakabiliwa na kosa la kutoroka na kwenda kufanya fujo kwenye disko lililokuwa likipigwa Chuo cha Maendeleo, Njombe.
Mwalimu William alisema mwanafunzi mmoja amesimamishwa kwa kosa la kukutwa na simu darasani wakati sheria za shule haziruhusu.
“Huu ni utukutu wa watoto ambao unakatisha tamaa, madai wanayolalamikia hayana msingi, na kuna mmoja wao alijeruhiwa vibaya huko kwenye disko na mpaka sasa anatembelea magongo.
“Sasa tumewasimamisha wanadai ni uonevu. Kuna uonevu gani hapa mpaka wafanye uharibifu mkubwa hivi? Alihoji mwalimu huyo.
Mwenyekiti wa Bodi ya shule hiyo, Maria Mdete alisema wanafunzi wanaowatetea hawajafukuzwa shule bali walisimamishwa tu na juzi walikutana na wazazi wa wanafunzi hao.
Alisema athari ya tukio hilo itakuwa kubwa hasa kwa wanafunzi wa kidato cha sita wanaojiandaa na mtihani wa Taifa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Fulgence Ngonyani naye alifika katika eneo la tukio na kujionea uharifu uliofanyika na kufanya kikao cha ndani na mkuu wa shule hiyo.
Ngonyani aliwaambia waandishi wa habari kuwa atalizungumzia suala hilo baada ya kufanya tathmini ya hasara iliyopatikana.
MWANANCHI

1 comment:

Anonymous said...

Nafikiri muda umefikia wa kufikiri kabla hujaamua kutenda kitu. Nikiangalia hapo hawakutatua tatizo bali wamejiongezea matatizo.
kuna wazazi ambao hata kuwalipia watoto wao ada, wamejinyima kupita kiasi au kupunguza hata huduma kwa watoto wadogo nyumbani. Sasa hiyo gahrama ya 150,000/+ nauli ya watu wawili wakati huo mmoja wao atahitaji nauli ya kurudia pengine hata malazi na chakula! Kundi jingine ni la wale ambao hawakujihusisha na chochote, masomo yao yamesimama kwa muda! Vijana wakumbuke tu yakuwa kuna wazee wanaotamani kurudi shule maana hawakuzingatia shule Enzi zao/ walikoswa ada na wafadhiri! Acheni jamani kuharibu miundo mbinu mnaongeza umasikini!