ANGALIA LIVE NEWS

Monday, October 6, 2014

WANANCHI WAASI, WAWASHAMBULIA WATENDAJI, VIONGOZI

Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue

Takribani wiki moja baada ya Ikulu kukana Rais Jakaya Kikwete, kuagiza watumishi wa serikali kuchangishwa fedha na Chama cha Walimu Tanzania (CWT) na watumishi wengine wa serikali kupinga walimu kukatwa mishahara kuchangia ujenzi wa maabara za shule za sekondari nchini, baadhi ya wananchi mkoani Singida wameasi na kuwashambulia na kuwajeruhi viongozi wa serikali waliokuwa wakitekeleza mpango huo.

Wananchi hao wanadaiwa kuwashambulia na kuwajeruhi maofisa watendaji wa serikali akiwamo ofisa mtendaji wa kata na mtendaji wa kijiji, katika Wilaya ya Mkalama, mkoani Singida waliokuwa wakikusanya michango hiyo ikiwa ni hatua ya kupinga utekelezaji wa mpango huo.

Michango hiyo ilikusudiwa kuelekezwa kwa Shule ya Sekondari Kata ya Mwangeza mkoani humo.Kutokana na kipigo hicho, viongozi hao wanadaiwa kulazwa katika Hospitali ya Haydom inayomilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Mbulu, mkoani Manayara kwa matibabu zaidi.

Imeelezwa kuwa viongozi hao walishambuliwa na baadhi ya wananchi wa Kitongoji cha Matere, Kijiji cha Dominiki, kilichopo Kata ya Mwangeza, Tarafa ya Kirumi.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, James Mkwega, alisema wakusanya michango hao waliongozwa na Ofisa Mtendaji Kata ya Mwangeza, Halfa Mrisho, ambaye naye amelazwa katika hospitali hiyo.

Tukio hilo lilitokea Oktoba Mosi, mwaka huu, majira ya mchana.Aliwataja wengine waliojeruhiwa kwenye sakata hilo kuwa ni Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Dominiki, Juma Saidi, Ofisa Mifugo wa kata hiyo, Joseph Doto, Mratibu wa Elimu kata hiyo, Saidi Nyika, na askari mgambo, Koyo Maduhu.

Alisema baada ya watendaji hao kujeruhiwa kwa silaha za jadi, walikimbizwa katika Hospitali ya Misheni ya Hydomu, iliyoko mkoani Manyara, ambako wanaendelea kupatiwa matibabu hadi sasa.

Akifafanua zaidi kuhusiana na tukio hilo, Mkwega alisema siku hiyo watendaji hao wakiwa kazini kwa ajili ya kukusanya michango ya ujenzi wa vyumba vitatu vya maabara ili kuitikia agizo la Rais Jakaya Kikwete, ghafla walivamiwa na watu ambao inaonyesha kwamba waliandaliwa kwa ajili ya kuwadhuru.

“Pamoja na kupigwa vibaya, pia walinyang’anywa fedha walizokuwa tayari wamekusanya, stakabadhi halali za kukusanyia michango na pikipiki zao zimeharibiwa vibaya.,” alisema Mkwega.

Hata hivyo, alisema Jeshi la Polisi tayari linamshikilia Diwani wa Kata ya Mwangeza, Petro Mlinga (Chadema) na baadhi ya wananchi wa Kitongoji cha Matere kuhusiana na tuhuma za kujeruhiwa kwa watendaji hao.

Kwa upande wake, Jeshi la Polisi Mkoa wa Singida limethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuahidi kuwa litatoa taarifa zaidi baada ya kukamilika kwa upelelezi.

Septemba 30, mwaka huu, CWT ilitoa tamko kupitia kwa wakurugenzi wa halmashauri zote nchini kujiandaa kukabiliana na mkono wa sheria wasipositisha zoezi la kuwakata walimu mishahara yao kwa ajili hiyo na kuwataka kurejesha mara moja fedha zote walizozikata kabla hawajadaiwa kuzirejesha na faida.

Naibu Katibu Mkuu wa CWT, Ezekiah Oluoch, alisema hayo alipozungumza na NIPASHE baada ya kuulizwa msimamo wa chama chao kufuatia taarifa ya baadhi ya halmashauri kuwakata fedha walimu kwa ajili ya ujenzi wa maabara.

Alisema kwa mujibu wa Sheria ya Mahusiano Kazini ya Mwaka 2008, mwajiri haruhusiwi kukata mshahara wa mwajiriwa. “Isipokuwa kwa ridhaa ya mwajiriwa au kwa matakwa ya kisheria kama vile amri ya mahakama,” alisema.

Alisema anatoa salamu hizo kwa wakurugenzi wote baada ya kuwa amepata barua iliyoandikwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa, mkoani Dodoma, ikiwaeleza kukata mishahara ya walimu.

WAZIRI MAJALIWA
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa-Tamisemi (Elimu), Kassim Majaliwa, alisema hana taarifa za kusambazwa kwa barua kwa waratibu elimu wa kata, zinazowataka wakusanye michango ya ujenzi wa maabara maeneo mbalimbali nchini na kwamba iwapo kuna michango kama hiyo, suala hilo ni la hiyari na siyo lazima.

BARUA YATHIBITISHA
Hata hivyo, suala hilo linathibitishwa na barua kutoka moja ya halmashauri nchini iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii kwenda kwa waratibu elimu wa kata yenye kichwa cha habari cha “Michango ya maendeleo kuchangia ujenzi wa maabara” ikiwataka waratibu hao kukusanya michango hiyo.

Barua hiyo, ambayo NIPASHE imeona nakala yake inaeleza kuwa kulingana na agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania juu ya ukamilishwaji wa maabara katika shule zote za sekondari nchini, uongozi wa halmashauri umeridhia uchangiaji huo.

Barua hiyo imeainisha viwango vya uchangiaji kuwa ni Sh. 60,000 (waratibu elimu kata), 60,000 ( walimu ngazi ya mshahara TGTS (F-G), Sh. 30,000 (ngazi ya mshahara TGTS D-E) na Sh. 20,000 ( TGTS B-C).

Barua hiyo ya Septemba 15, mwaka huu, imetaka michango hiyo kutolewa kwa awamu mbili; Septemba na Oktoba, mwaka huu na kuagiza walimu wakuu kusimamia michango hiyo kwa shule zao na kuwasilisha fedha hizo halmashauri.

Rais wa CWT, Gratian Mukoba, alithibitisha kupokea malalamiko kutoka kwa walimu juu ya michango hiyo na kusema inapaswa kuwa ya hiari na siyo lazima.

Alisema hiyo ni kutokana na makato ya kisheria kuwa wazi na kwamba, wamewaagiza viongozi wa chama hicho kwenye wilaya kufuatilia na kuhakikisha walimu wanafanya kwa hiari yao.

IKULU
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, alisema Rais hajawahi kutoa agizo lolote kwamba watumishi wa serikali wawe wanachangishwa fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

“Mimi sijui kama kweli kuna taarifa kwamba, Rais alishawahi kutoa agizo kwamba, watumishi wawe wanachangishwa fedha. Kama kuna watu wanasema hayo, waeleze Rais alitoa agizo hilo wapi,” alisema.
CHANZO: NIPASHE

No comments: