Advertisements

Saturday, November 8, 2014

KASHFA YA ESCROW:Ripoti ya CAG yaiva

 Sasa itawasilishwa Bungeni wiki ijayo
Ripoti ya uchunguzi uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhusu kashfa ya kuchota fedha kwenye Akaunti Maalumu ya Tegeta Escrow Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imekamilika na sasa itawasilishwa bungeni wiki ijayo.

Wakati ripoti hiyo ikisubiriwa, wabunge wameitaka serikali kufunga akaunti za kampuni ya VIP Engineering zilizopo katika Benki ya Mkombozi ili kupisha uchunguzi kwa kuwa kwenye akaunti hiyo kuna baadhi ya wabunge, mawaziri na majaji wamepata mgawo wa fedha za Tegeta Escrow.

Pia wametaka serikali izuie malipo ya zaidi ya Sh. bilioni 12, ambayo Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) huwalipa watu, ambao wanachunguzwa kuhusiana na kashfa hiyo kila mwezi ili kupisha uchunguzi huo.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, alisema bungeni jana kuwa ripoti hiyo ya CAG inatarajiwa kukabidhiwa kwa ofisi ya Bunge wiki ijayo na kwamba, wanataraji itatoa mwanga wa mambo yalivyo kimahesabu.

Alisema hayo alipokuwa akitoa taarifa kufuatia mwongozo wa Spika ulioombwa bungeni jana na Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila, akitaka serikali ifunge akaunti ya kampuni hiyo iliyopo katika benki hiyo.

Kafulila alisema serikali inapaswa kuchukua hatua hiyo kwa kuwa hata Jumuiya ya Ulaya (EU) baada ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitisha azimio la kuamuru uchunguzi ufanywe kuhusiana na kashfa hiyo, iliamua kufunga akaunti ya kampuni hiyo kwenye benki iliyopo nchini Uholanzi.

Alisema EU ilichukua hatua hiyo kuitikia mwito huo wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

"Sasa mheshimiwa naibu spika, nilitaka nipate mwongozo wako, kwamba wakati VIP ina akaunti Mkombozi Bank Tanzania na akaunti ile Tanzania kwa maana serikali hawajaamuru akaunti ile iwe suspended (isitishwe) kwanza, kusubiri uchunguzi. Kama ambavyo benki ya Ulaya imeamua kule kuitikia uamuzi wa Bunge lako tukufu," alisema Kafulila.

Aliongeza: "Kwa hiyo, ningependa mwongozo wako katika jambo hili, kwa sababu taarifa zilizopo kwenye akaunti hiyo ya Mkombozi kuna baadhi ya wabunge, mawaziri na majaji wamepata mgawo wa fedha za Escrow kupitia akaunti hiyo."

"Sasa katika utawala bora, kwa kuwa Bunge lako liliamuru uchunguzi, kwanini serikali haikuona haja ya kusitisha ile akaunti kusubiri uchunguzi ukamilike ndiyo iendelee kama ambavyo benki ya Ulaya iliamuru kusitisha akaunti hiyo kule nchini Uholanzi. Naomba mwongozo wako katika hilo."

Akijibu hoja hiyo ya Kafulila, Waziri Lukuvi kwanza alisema taatifa kuhusu EU hajaisoma na kwamba, kwa mujibu wa sheria zinazotumika Tanzania na maelekezo ya Bunge, suala la kampuni ya kufua umeme ya IPTL na akaunti ya Escrow linashughulikiwa na CAG kwa maagizo ya Bunge.

Pia alisema Bunge lilikwisha kusema kuwa uchunguzi utafanywa na vyombo vinavyohusika kwa mujibu wa sheria za Tanzania na kwamba, kazi hizo zimepewa taasisi mbili, ikiwamo Takukuru.

"Kazi hiyo ya uchunguzi pamoja na hayo (Kafulila) unayoyasema na mengine (Takukuru) ameshaanza kuyafanya," alisema Lukuvi.

"Ninachotaka kusema ni kwamba, kwa sasa uchunguzi wa mambo yote hayo yanayosemekana, yanayosikika, yanayosemwa kuhusiana na hilo, yanafanywa hivi sasa na taasisi hizo mbili kwa mujibu wa maelekezo ya bunge lako na kwa mujibu wa sheria za nchi hii."

Mbunge wa Chakechake (CUF), Mussa Haji Kombo, alisema kwa heshima ya nchi na serikali amesikitishwa kusikia Lukuvi, ambaye ana jukumu la kusimamia shughuli za serikali bungeni, anashindwa kujua 'data' ndogo inayohusu akaunti hiyo kufungwa Uholanzi na EU kwa sababu ya fedha za Escrow.

Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe, alisema wakati uchunguzi wa kashfa ya Escrow unaendelea, Tanesco bado inawalipa watu, ambao wanachunguzwa kiasi hicho cha fedha na kuhoji: "Ni kwanini malipo hayo yasizuiwe mpaka uchunguzi utakapokwisha."

Aliunga mkono hoja ya Kafulila na kuhoji: "...ni kwanini mamlaka zetu za ndani hapa Tanzania, hazijachukua hatua kama hiyo pending(iliyoachwa kiporo), uchunguzi ukiisha mambo yakiwa safi murua wanarudishiwa hela zao. Uchunguzi ukionekana kwamba kuna makosa, tutakuwa tumeweza kuokoa fedha zaidi hata kama uchunguzi utaonyesha kuna matatizo, kutakuwa na ugumu sana wa kurejesha fedha, ambazo tayari zimelipwa."

"Kwa hiyo, nilikuwa ninaomba waziri wa nchi aweze kutoa kauli ya serikali kwamba, je, mamlaka husika, hasa benki kuu, mamlaka husika, hasa serikali, itazuia malipo hayo hivi sasa. Taarifa inakuja, inawezekana imeingia leo, wiki ijayo tukaanza kuishughulikia. Kwa hiyo, baada ya hapo, tutaweza kujua kama kuna tatizo au hakuna tatizo."

Mbunge wa Kasulu Mjini (NCCR-Mageuzi), Moses Machali, alisimama ili kumpa taarifa Waziri Lukuvi na kusema ni dhambi mbaya sana kwa mtu kuzungumzia jambo, ambalo hulijui.

Alisema kilichofanywa na Lukuvi ni kuzungumza kitu kingine, ambacho hakihusiani na muktadha, hivyo, akamtaka kuepuka kuzungumzia mambo ambayo hayajui.

"Hayo ni mambo ya ubabaishaji, hili ni jambo zito. Leteni taarifa tukate mzizi wa fitina na siyo blah blah mahali hapa," alisema Machali.

Kauli hiyo ya Machali ilimfanya Ndugai (pichani) kusimama na kumtaka kutumia lugha zinazopendeza bungeni.

Ndugai alisema hoja za Kafulila, Zitto na Machali, zimelenga kuwahisha kufanyika shughuli husika kwa kuwa tayari wameshakubaliana mwanzoni mwa wiki hii bungeni kuwa serikali na vyombo vinavyohusika vilifanyie kazi suala hilo, ikiwa ni pamoja na kupeleka ripoti bungeni.

"Tumepewa taarifa na mheshimiwa waziri ametuambia kuna uwezekano mkubwa kabisa ripoti ikaja wiki ijayo. Na kwenye ratiba yetu ya Bunge tumeorodhesha kwamba mambo haya tutayajadili tarehe 27 ikiwezekana tarehe 28 mwezi huu, kwa sababu baada ya taarifa hizo kuja, lazima zipewe kwanza taarifa ya bwana Zitto ya PAC wapitie, baadaye tuje tuone namna gani tunafanya," alisema Ndugai.

Tayari nchi wahisani zimetangaza kuikatia misaada serikali ya zaidi ya Sh. trilioni 1 kutokana na kashfa hiyo.

Akaunti ya Tegeta Escrow ilifunguliwa kutokana na kutoelewana kuhusu gharama halisi na halali za umeme unaozalishwa na IPTL na kuuziwa Tanesco.

Mahakama ya Usuluhishi ya Kimataifa (ICSID), katika uamuzi wake wa Februari 2014, ilitoa hukumu kuonyesha kwamba Tanesco walitozwa kiwango cha juu zaidi ya kilichopaswa kulipwa kwa IPTL.

Kwa uamuzi huo, ni dhahiri fedha zilizokuwa zimehifadhiwa kwenye akaunti ya Escrow zilipaswa kugawanywa kwa IPTL na Tanesco baada ya hesabu kufanyiwa marekebisho upya kwa viwango halali, lakini badala yake fedha hizo zilitoweka ghafla kwenye akaunti hiyo.

CHANZO: NIPASHE

1 comment:

Anonymous said...

Asante, Kwa Kweli tupu Tanzania tumejawa na upumbavu wa hali ya juu!! Hii sio taarifa ya kujadiliwa bungeni hata kidogo na kama itapokelewa na bunge basi halijui kazi ya kufanya!. Kumbe hii ni fedha aliyokopa na sio amechukua kiholela!! Na isitoshe ni fdha kidogo saana kulinganisaha na fedha iliyokuwa inalipwa kwa hawa wachakachuaji wa bunge la katiba!! Je mlikuwa mnataka asimtibie mama yake/ na kama kulikuwa kuna uwezekanao wa kukopa hiyo fedha na akastahili kwanini asipewe?? Ninyi mliofutatilia haya mambo hamna kazi ya kufanya ana haki mbona waziri mkuu Sitamtaja jina aichota fungu kibao kwa yasiyojiri na haikurudishwa! tuacheni maneno ya kupotosha jamii
>>......