1. Mtason Mtagwamba, mkazi wa Kijiji cha Nyantorotoro
Uliwaahidi wakazi wa Kijiji cha Nyantorotoro, Geita maji baada ya kuwaona wanateseka kwa kunywa maji ya chumvi na meupe kama maziwa, lakini mpaka leo bado wanateseka.
Jibu: Tulikuwa tumekubaliana na Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM) kusaidiana kuleta maji Geita.
GGM ilikamilisha sehemu yake ambayo ni ya kuvuta maji kutoka Ziwa Victoria lakini Serikali ikawa imekwama kusambaza maji kwa wananchi kama tulivyokuwa tumekubaliana.
Lakini tulikaa tukakubaliana na GGM ikamilishe programu hiyo ya kusambaza maji kwa wananchi na mpaka sasa taratibu ziko hatua ya mwisho hivyo wananchi wote wa Geita watapata maji kabla mwaka huu wa 2014 haujaisha.
2. Paulo Vicent.
Wananchi wa Geita wamebarikiwa kwa kuwa na madini lakini wanaishi kama wakimbizi, wananyan’ganywa ardhi wanapigwa virungu na kuitwa wezi. Ulituahidi kutatua tatizo la wachimbaji wadogo lakini mpaka leo wachimbaji wanakufa kwa kupigwa virungu wanapokwenda kuchimba kwenye maeneo ya wawekezaji na hata maeneo yao wanayochimba ikigundulika kuna dhahabu wanafukuzwa na kuambiwa eneo la mwekezaji utatueleza nini juu ya hili?
Jibu: Naomba niseme kuwa mbunge hajawadharau wachimbaji wadogo na suala la maeneo ya kuchimba wachimbaji wadogo linaendelea kushughulikiwa.
Lakini mpaka sasa kuna viwanja 18 vimetengwa kwa ajili yao maeneo ya Isamilo na Rwenge. Lakini suala la wachimbaji wa samina na Mpovu hilo eneo ni la mwekezaji na wachimbaji wadogo wanatakiwa kuondoka.
3 Wales Steaven, mkazi wa Kalangalala
Wakati unagombea ulituhahidi maji wakazi wa Kalangalala na Nyankumbu ndani ya miezi mitatu, ukasema kwa kinywa chako kama usipotekeleza ahadi hiyo kwa muda huo tukikuona tukukate kichwa.
lakini ulivyotuacha ndivyo tulivyo hadi leo. Kwa nini uligombea wakati ulijua huwezi kutekeleza ahadi?
Jibu: Kama nilivyokwishaeleza hapo awali kwamba maji yanakuja na mbunge licha ya kuwa anaumwa kwa kweli anajitahidi.
Ninachoweza kusema hapa ni kwamba hatujapata fedha kutoka Serikali kuu ambayo ni bajeti ya halmashauri.
Baadhi ya ahadi za mbunge zimechelewa kukamilika kwa wakati kutokana na ufinyu huo wa bajeti. Lakini tumeiomba GGM itusaidie kusambaza maji katika mji wa Geita.
Maji yanakuja wameshaanza kuchimba mitaro hivyo kabla ya uchaguzi maji yatakuwa yamefika, wananchi wawe na subira, wawe na imani na mbunge wao najua ahadi zote zitatekelezwa kwa asilimia 80 kabla uchaguzi.
4. Zawadi John, mkazi wa Nyakumbu
Wananchi wa kijiji cha Nyakumbu tuna tatizo la maji, kina mama tunatembea umbali mrefu na kupigania maji kwenye visima vya asili. Tunakunywa maji yenye mekyuri, ngozi zetu zinakakamaa kwa kuoga maji machafu. Ulituhahidi Nyankumbu itabubujika maji lakini hadi leo tunaelekea uchaguzi hakuna kitu unatueleza nini?
Jibu: Suala la maji nimeshalizungumza, nimesema yanakuja kabla ya mwaka huu kuisha. Niseme Mbunge hajawaahidi uongo, ahadi zake zote zinashughulikiwa na zitatekelezwa kama ilivyopangwa.
5. Jotham Mabula, mkazi wa Karangara
Nakumbuka wakati unaomba kura zetu katika Viwanja vya Nyankumbu na Karangara ukiwa amepiga Magoti uliahidi maji lakini mpaka leo tuko hivyohivyo. Kipi umetufanyia wananchi katika ahadi zote ulizotoa?
Jibu: Suala la maji nimeshalijibu, ninachoweza kusema hapa ni juu ya mambo aliyoyafanya mbunge.
Kabla hajaugua amefanya yafuatayo. Ameezeka kituo cha Polisi Nkome, ametoa mabati na kuezeka kituo cha Polisi Kakubilo.
Pia amejenga shule mbili kwa kata 19, pia amepeleka fedha za kutengeneza madawati kwa kila kata za Jimbo la Geita zaidi ya Sh69 milioni.
Wanafunzi wa shule hizo wanakaa vizuri kwenye madawati, pia amepeleka mabati 120 kwa kata 19 ya kuezeka shule za msingi na sekondari.
6. Erick Tarimo, mkazi wa Geita
Geita tuna tatizo la barabara, alituahidi wananchi wa Msalala Road kuwa tutakuwa na barabara baada ya kuoana ni mbovu na hatuna sehemu ya kupitisha magari ya kubeba wagonjwa, lakini mpaka leo hazijatengenezwa,kwa nini?
Jibu: Mpaka sasa barabara zinajengwa katika maeneo mbalimbali ya mji wa Geita ikiwamo Msalala Road.
Tumejenga barabara ya hapa mjini kwa kiwango cha lami na tunaendelea na ujenzi wa barabara za mkoa ikiwamo ya kutoka Geita kwenda Kasota na Nkome.
7. Baraka Enock, mkazi wa Geita
Nataka kujua kutoka kwako, wachimbaji wadogo wa Samina wametengewa maeneo gani? Wakati unagombea ulisema kila mchimbaji wa Geita atakuwa na eneo la kuchimba na hakuna wa kuwanyanyasa. Lakini leo wachimbaji wanateseka.
Jibu: Wachimbaji wadogo wametengewa maeneo ya Isamilo na Rwenge na bado tunaendelea kutafuta maeneo mengine.
Mbunge hajawasahau wachimbaji wadogo, anawakumbuka sana na ndiyo maana anahangaika kutafuta maeneo mengine kwa kuwatumia madiwani.
8. Elizabeth Msusa, mkazi wa Geita
Una mpago gani na maendeleo ya Mkoa wa Geita maana tangu tumekuchagua hatujaona chochote?
Jibu: Mbunge ana mipango mizuri tu ya maendeleo ya Geita na ndiyo maana mnaona sasa hivi Geita imebadilika haikuwa kama ilivyokuwa mwanzo.
Tumejenga barabara za lami, tumefanya ukarabati wa baadhi ya majengo ya Geita, bado tuna mipango mingi ya kuhakikisha Geita inakuwa na maendeleo.
9. Simon Nyanda, mkazi wa Nyankumbu
Tangu tukupe madaraka hujawahi kutufanyia chochote katika ahadi zote ulizotuahidi ikiwamo umeme katika Kijiji cha Nyankumbu. Mpaka leo wananchi wanatumia vibatali. Zahanati ya Nyankumbu kina mama wanajifungua kwa vibatali na tochi. Kwa muda huu uliobaki utatufanyia nini?
Jibu: Kwa muda huu ulliobaki mbunge analifanyia kazi suala hilo. Kuna mpango wa kusambaza umeme vijijini na vijiji 30 vya Jimbo la Geita vitanufaika kikiwamo Kijiji cha Nyankumbu na Zahanati ya Nyankumbu.
Mchakato wa kusambaza umeme katika Jimbo la Geita umeshaanza, nguzo zinasimikwa na kazi inafanyika kwa kasi hivyo muda si mrefu umeme utawala Nyankumbu na Tarafa nzima ya Busanda.
10. Edward Kuzenza, mkazi wa Geita
Ulituhaidi kwamba hadi kufikia Novemba, 2011 wananchi wa Wilaya ya Geita watakuwa na maji.
Lakini mpaka sasa wanahangaika . Je, una mkakati gani wa kutuletea maji wakazi wa Geita?
Jibu: Nimeshaeleza kwamba maji yatafika Geita muda ambao. Kama nilivyosema, bajeti ya mwaka huu ilibana kidogo kutokana na mambo ya kitaifa.
Hivyo kufikia Novemba mwaka huu, wakazi wa Geita watakuwa na maji kama mbunge alivyoahidi.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment