ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, November 20, 2014

Mbinu za kuzuia mjadala kashfa IPTL zafichuliwa


Mkanganyiko mkubwa umeibuka mjini hapa kwamba serikali inafanya kila njia kuzuia taarifa ya sakata la IPTL la uchotwaji wa zaidi ya Sh. bilioni 300 katika akaunti ya Escrow iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kujadiliwa bungeni.

Habari za mkakati huo zilitangazwa jana na wabunge watatu wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), James Mbatia (NCCR-Mageuzi), Tundu Lissu (Chadema) na Mohamed Habib Mnyaa (Cuf), walipozungumza na waandishi wa habari wakidai kuwa Mahakama Kuu ya Tanzania imeandika barua kwenda ofisi za Bunge ikizuia mjadala wa sakata hilo.

Wabunge wa Ukawa waliionya Mahakama Kuu ya Tanzania, kutotumika kuzuia Bunge kujadili ufisadi kwenye akaunti ya Escrow.

Mbatia ambaye pia ni Mbunge wa Kuteuliwa na Rais, aliwaambia waandishi wa habari kuwa wamebaini mbinu za kuchelewesha au kuzuia Bunge kujadili kashfa hiyo.

Alisema hata danadana zinazoendelea katika ratiba ya shughuli za kila siku za Bunge, ikiwamo kuahirishwa kikao cha jana, kuwa ni moja ya njama za kupoteza muda ili mwishoni isemekane muda hautoshi.

Kwa msingi huo wanataka kila Mbunge apewe nakala ya ripoti hiyo, angalau kati ya siku tatu hadi nne, kabla ya Jumatano ijayo, suala hilo litakapopelekwa bungeni na PAC.

Mbatia alisema hatua hiyo itatoa nafasi kwa wabunge, kuisoma na kuielewa ili kuijadili kwa upana na kutoa uamuzi utakaofaa kwa maslahi ya taifa.

“Hii kashfa inahusisha viongozi waandamizi serikalini na tumepata taarifa za uhakika, kuna kila aina ya mbinu zinafanywa kuhujumu Bunge lisisimamie serikali katika kudhibiti matumizi ya kodi hizi za wananchi,” alieleza Mbatia.

Alisema kwa uchunguzi uliyofanyika mpaka sasa, wabunge hao wameazimia kila atakayethibitika kuhusika kisiasa, kisheria au kimaadili, achukuliwe hatua stahiki sambamba na kurejesha fedha alizochukua.

Alitaka umma kufahamu kuwa kashfa hiyo iliibuliwa bungeni kabla haijaondolewa kwa ahadi iliyotolewa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kwamba ingerudishwa baada ya kuchunguzwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Taasisi ya Kudhibiti na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

Mbatia alisisitiza kuwa pamoja na ripoti ya uchunguzi kuelezea fedha zilizochotwa kwenye akaunti ya Escrow kuwa zilizotokana na kodi za wananchi, kuna zaidi ya Sh. bilioni 21 ambazo zilitakiwa zilipwe serikalini kama kodi, lakini hazikulipwa.

“Hata Katibu Mkuu Kiongozi (Balozi Ombeni Sefue) mlimsikia akikemea Bunge lisishughulikie suala hili, akituita wanasiasa, tunasema hii ni kodi ya wananchi ni lazima tuhakikishe inatumika sawasawa, ndilo jukumu letu hilo,” alieleza.

Kwa mujibu wa Mbatia, watuhumiwa hao katika kashfa ya Escrow wamefika mbali zaidi kwa kufikia hatua ya kuingiza mahakama ili kuitumia kama kigingi cha kuzuia au kucheleweza mjadala huo usifanyike kama ilivyopangwa.

Aliwaonya wahusika hao, akiwataka kusoma alama za nyakati kwamba kwa sasa utulivu umekosekana bungeni, nje ya Bunge na hata serikalini na hivyo waone umuhimu wa kuacha kashfa hiyo ijadiliwe ili hatima yake ijulikane.

“Hauwezi kuacha watu kati ya watatu hadi saba hivi, wakatesa vichwa vya watu na walipa kodi wa Tanzania, hakuna uwezekano wa mahakama kuingilia mchakato wa kazi za kibunge dhidi ya kashifa ya IPTL,” alieleza Mbatia.

Pia alisema kwamba wanazo taarifa kuwa serikali inajaribu kusema haina fedha, ili muda wa Bunge ufupishwe kashifa hiyo ijadiliwe kwenye vikao vya Bunge vijavyo na kwamba Ukawa haiko tayari kwa hilo kutokea.

Lengo la mpango huo lilielezwa na Mbatia kuwa ni kutaka kuchakachua ripoti hizo zilizotokana na uchunguzi wa vyombo viwili vya serikali.

“Ukawa hatuna haja ya kumkandamiza mtu, tunachotaka ni haki itendeke kwa pande zote, waliohusika kuiba na walioaibisha taifa kwa kashfa hizi wawajibike kwa mujibu wa sheria, lakini pia fedha za walipa kodi zirudishwe,” alisema.

Naye Mbunge wa Iramba (Mashariki- Chadema) ambaye pia ni Mshauri wa Masuala ya kisheria wa Ukawa, Tundu Lissu, alisema hakuna kipengele cha sheria yoyote anayoifahamu kinachoruhusu mahakama kuingilia shughuli za Bunge na kwamba, kesi ya wizi huo katika akaunti ya Escrow ilikwisha kufanyiwa uamuzi katika Mahakama Kuu, Saa 6:00 usiku.

Alitaka mahakama ikiwa bado ina hata chembe ya kuhitaji kusitiri hadhi yake, isikubali kutumika mithili ya karatasi ya chooni.

Alisema kashfa hiyo ni kubwa na pengine kuliko ya Richmond, ambayo ilijadiliwa bungeni na uamuzi ukafikiwa kabla ya waliohusika kwa namna tofauti kuwajibika tena bungeni.

“Tumesikia kuna barua imetoka mahakamani, kwa Jaji Mkuu au Jaji Kiongozi, hatujapata hakika, lakini tumeambiwa kwamba, kuna barua imekuja kutoka mahakama ya Tanzania ikisema jambo hili liko mahakamani na kwa sababu hiyo lisijadiliwe na Bunge,” alisema Lissu.

Alisema kwa mujibu wa kanuni za Bunge, hakuna mahakama au jaji, au kiongozi yeyote wa mahakama mwenye mamlaka ya kuliandikia Bunge barua, kulipangia kitu gani kifanyike au kisifanyike.

Vilevile Lissu alisema utaratibu wa aina hiyo haupo hata kwa mujibu wa Katiba ya nchi wala sheria yoyote anayoifahamu, iliyowahi kutungwa na Bunge na kwamba itawashangaza ikitokea barua ya aina hiyo iingizwe kwenye ukumbi wa Bunge kama inavyosemekana imekusudiwa.

Alitoa wito kwa wabunge wa CCM wanaochukia maovu, kushirikiana nao dhidi ya vikwazo vinavyoundwa kuzuia mkakati wa kushughulikia wezi bungeni kutekelezwa.

Hata hivyo, Lissu alisema ikitokea wakafanikiwa kuzima jitihada hizo bungeni, wana hakika hawatafaulu kuzizuia nje ya Bunge kwa kuwa dunia ni pana, watatembea kwa lengo la kuhakikisha kodi ya Watanzania inatendewa haki.

Naye Mbunge wa Mkanyageni (CUF), Mohammed Habib Mnyaa, alisema pamoja na maelezo ya Mbatia, mwenendo wa serikali unaoshuhudiwa kwa sasa, ukiwamo kuunganisha vikao viwili vya Bunge; cha 16 na 17 ni dhahiri haina nia njema ya kuridhia kashfa ya Escrow kujadiliwa bungeni.

“Tulitakiwa kukaa kwenye kamati wiki nne, tumekaa wiki mbili ikisema haina fedha tuahirishe Bunge kwa ajili hiyo, basi ni dhahiri serikali hii imeshindwa kujiendesha, kiasi cha kukosa uwezo wa kuhudumia muhimili wake wa Bunge,” alieleza Mnyaa.

Msemaji wa Mahakama ya Tanzania, Mery Gwela, alipoulizwa kuhusiana na barua hiyo, alisema hana taarifa na kwa wakati huo yupo nyumbani na kushauri aulizwe Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Amir Msumi, ambaye naye hakupatikana baada ya simu yake ya kiganjani kuita bila kupokelewa. Nao viongozi wakuu wa Bunge hawakupatikana kuthibitisha kama wameipokea barua hiyo.

Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashillilah, alipotafutwa simu yake haikupokelewa kwa maelezo kutoka Kitengo cha Habari cha Bunge kuwa alikuwa kwenye kikao sambamba na Ndugai.

Hata walipotumiwa ujumbe mfupi wa maandishi (sms) hawakujibu hadi tunakwenda mitamboni.
CHANZO: NIPASHE

1 comment:

Anonymous said...

Asanteni wadau na Mr Mbatia na wafuasi wote hili sio jambo la kuanchia au kufanyiwa mzaha tuliona ya Mheshimiwa Aliyekuwa waziri Mkuu JAPO wanamwita msataafu!!! sio mstaafu. hili swala lazima lijulikane kiuhakika kabla ya uchaguzi ujao tusidanganyane hapa!!! This is tooomuchh wana Tanzania, au Tanganyika!!!