ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, November 5, 2014

MUWSA YASAMBAZA BOMBA LA MAJI KATIKA MRADI MKUBWA WA MAJI MTO KARANGA

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira mjini Moshi,MUWSA ,Mhandisi Cyprian Luhemeja akiwaonyesha wanahabari chanzo cha maji kilichopo Mto Karanga .
Wanahabari wakipita juu ya Bomba la kusambaza maji kutoka katika chanzo cha maji cha Mto Karanga.

TATIZO la upungufu wa maji katika Manispaa ya Moshi linaelekea kuwa historia ifikapo mwezi Desemba mwaka huu kufuatia kukamilika kwa utekelezaji wa mradi mkubwa wa maji uliopo katika chemchem ya Mto Karanga ambao umegharimu kiasi cha shilingi milioni 382.

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira ( MUWSA), Mhandisi Cyprian Luhemeja amefafanua kuwa, mradi huo utakapokamilika utahudumia maeneo ya Bomambuzi, Pasua , Matindigani na meneo ya katikati ya mji.

Mhandisi Luhemeja amesema maeneo hayo kwa sasa yana mgawo wa maji kutokana na uwepo wa maji kidogo ambapo pindi mradi huo utakapokamilika utawezesha kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa maji katika maeneo hayo kwa saa 24.

Amesema mradi huo utasaidia kuongeza kiwango cha upatikanaji wa maji kwa mita za ujazo zipatazo 2,592 kwa siku katika mfumo wa kusambazia maji ambapo kwa sasa umeshakamilika kwa asilimia 99.Amefafanua kuwa gharama za mradi huo ni kubwa lakini gharama za uendeshaji ni ndogo kutokana na chanzo cha maji hayo kutoka katika chemchem ya mto karanga ambapo itasaidia upatikanaji wa maji saa 24.

No comments: