Huduma zazidi kuzorota
Wagonjwa wakosa matumaini
Wagonjwa wakosa matumaini
Hali ya huduma za tiba katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) ni mbaya kutokana na tatizo kubwa la bajeti ya kuwezesha wagonjwa kutibiwa kwa wakati na kupata dawa na vifaa tiba, jambo ambalo hata uongozi wa hospitali hiyo umelithibitisha.
Kukosekana kwa fedha za kutosha za kuendesha hospitali hiyo huku ikielemewa na madeni mengi ya watoa huduma, kumefanya ubora wa huduma za kitabibu zinazotolewa kuwa duni kiasi cha kwamba mgonjwa asiye na fedha za kununua dawa kutoka mfukoni mwake hali yake inazidi kuwa mbaya siku hadi siku.
Kwa muda mrefu sasa wagonjwa wanaolazwa na wanaotibiwa na kuondoka, wamekuwa wakilazimika pia kununua dawa kwenye maduka ya dawa yaliyopo nje ya hospitali hiyo na kwingineko kwani kwenye maduka ya hospitali hiyo dawa hazipatikani.
Maelekezo ya dawa na matumizi yake vinaandikwa na daktari wa MHN, lakini
kutokana na kile kinachoelezwa kuwa ni upungufu, hata zile za msingi kama Panadol na Diclofenac, wagonjwa wamekuwa wakielekezwa kwenda kununua kwenye maduka nje ya hospitali hiyo.
Anne Joseph anayemuuguza mumewe hospitalini hapo alisema, “ukisikia ndugu yako yuko Muhimbili ogopa, hali ni mbaya na kama hauna fedha anakufa ukimuangalia tu.”
Anaongeza: “Tangu Januari mwaka huu sisi tuko hapa, mume wangu ana tatizo la kibofu cha mkojo na kila tunapokuja tunaandikiwa dawa. Lakini ukienda katika maduka yao unaambiwa hii hatuna, sasa tumeishiwa hela.” Anne alizungumza na NIPASHE Julai mwaka huu ilipoanza uchunguzi wa hali ya huduma katika hospitali hiyo kubwa kulizo zote nchini.
Anasema mumewe, Abia Joseph, anasumbuliwa na kibofu cha mkojo kwa muda mrefu, lakini kila wanapokwenda kumwona daktari na kuandikiwa dawa, wamekuwa wakilazimika kwenda kununua kwenye maduka binafsi yaliyoko nje ya MNH.
Naye Henry Ummy, anayemuuguza ndugu yake, John Jonathan, alisema tangu mgonjwa wao alazwe MNH Julai mwaka huu wamekuwa wakinunua dawa wanazoandikiwa na daktari na kwamba wagonjwa wanaodhihirika kutokuwa na uwezo wa kiuchumi, wanajaziwa fomu za msamaha na kupewa dawa.
Mama mzazi wa Kulwa Stephen (12), ambaye alipata ajali hivyo kuwekewa `njia’ ya kutolea haja ndogo maeneo ya tumboni licha ya kukosa huduma kwa wakati, alilalamikia ukosefu wa dawa alizoandikiwa hospitalini hapo kwa ajili ya mtoto huyo wakati akiwa hana fedha.
“Mtoto wangu amewekewa mipira ya kujisaidia haja ndogo baada ya kupata ajali ya gari. Siku zote nikimleta hapa Muhimbili naandikiwa dawa… lakini maduka haya ya Muhimbili (madirisha ya kutolea dawa Muhimbili) nimeambiwa hakuna dawa, sasa fedha tunazochangia sijui zinakwenda wapi,” alihoji.
Anaongeza: “Huyu mtoto naenda naye kupanda daladala kurudi nyumbani, sasa kama hajapata dawa mambo yanaweza kutuharibikia njiani na sina fedha za kununulia hizo dawa.”
Kwa mujibu wa uchunguzi wetu, kuna upungufu mkubwa wa vitanda na nafasi ni finyu kwenye wodi za hospitali hiyo, hali inayowalazimu wauguzi kuwalaza wagonjwa kwenye magodoro yaliyochakaa sakafuni; wengine kwenye viambaza vya wodi husika.
Hata hivyo, uchunguzi wa NIPASHE mwanzoni mwa wiki hii Muhimbili umeonyesha kuwa wagonjwa wamepungua sana kiasi cha baadhi ya vitanda kubakia wazi. Mwenendo huu mpya unaelezwa kuwa unachangiwa kwa kiasi kikubwa na gharama mpya za matibabu, hasa za kulipia kitanda Sh. 5,000 kwa siku. Gharama hizi zilianza kutumika mwezi uliopita.
Uchunguzi wa NIPASHE umebaini kuwa hali ya vyoo vya wodi mbalimbali kwenye hospitali hiyo ni mbaya.
Hakuna maji, hali inayosababisha baadhi ya ndugu na jamaa kununua maji kutoka nje na kuwapelekea wagonjwa wao.Vyoo vingine usiku haviingiliki kutokana na kukosa taa.
Baadhi ya ndugu na jamaa wa wagonjwa waliozungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti, walisema wanalazimika kupeleka maji kwa ajili ya wagonjwa wao kutokana na maji kwenye wodi hizo kutopatikana kwa uhakika.
Akizungumza kuhusu kuzorota kwa huduma katika hospitali hiyo, mmoja wa madaktari alisema serikali iliamua `kuyapa kisogo’ madai ya madaktari ambayo mengi yalikuwa yakitaka kuboreshwa kwa huduma hospitalini hapo.
Hivyo, alisema madaktari waliamua kukaa kimya na kufanya kazi katika mazingira hayo yanayowaathiri zaidi wagonjwa wasiokuwa na hali nzuri kiuchumi.
Daktari huyo ambaye hata hivyo hataki kutajwa jina lake, alisema wakati wa mgomo wa madaktari mwaka 2011 serikali ilijitahidi `kupindisha ukweli’ na kuwahadaa wananchi kwamba madaktari walikuwa wakitaka nyongeza ya mishahara.
Alisema, ukweli ni kwamba madaktari walikuwa wakilalamikia mazingira magumu ya kazi kama ukosefu wa vifaa tiba, dawa na vipimo hospitalini hapo na nyongeza ya mishahara ikiwa ni sehemu tu ya madai yao.
Daktari huyo alisema moja ya madai ya madaktari kwenye mgomo uliotikisa nchi mwaka 2011, ilikuwa ni kuboreshwa mazingira ya kazi, kuongeza vifaa tiba na upatikanaji wa dawa hospitalini, vipimo, nyongeza ya mishahara ya madaktari, kuwapo vitanda na wodi za kutosha.
“Ni kweli nyongeza ya mshahara ilikuwa moja ya madai yetu, lakini madai mengine yalikuwa kwa maslahi zaidi ya wagonjwa. Cha kushangaza miaka inapita, madai hayajafanyiwa kazi na hakuna chombo chochote kile kinachoyafanyia kazi,” alisema.
“Hivi sasa serikali isione madaktari wamekaa kimya ikadhani mambo yameisha, bali watu wameamua kufanya kazi katika mazingira yaliyopo... walioondoka wameondoka, waliobaki wanafanya kazi kama kusukuma muda tu ili waende kwenye shughuli zao binafsi za kuwaongezea kipato,” alisema.
Zipo taarifa kuwa baadhi ya madaktari walikwenda kufanya kazi nje ya nchi ikiwamo Botswana inaposemekana wanalipwa mshahara mizuri ya kati ya Sh. milioni 3.5 hadi sita kwa mwezi . “Hali iliyopo hapa Muhimbili ni kama serikali imefunika tatizo, ila isijidanganye kwamba limeisha, wasipochukua hatua kurekebisha, huko tuendako mambo yanaweza kuharibika zaidi ya hali iliyopo, sasa,” alisema.
Anaongeza: “madaktari wamekaa kimya sana lakini wana kinyongo moyoni kwa maana madai yao yamewekwa kapuni. Sasa ipo siku kunaweza kuibuka mgomo (mwingine) mkubwa hapa.”
Alisema viongozi wengi wa serikali wanafahamu matatizo ya Muhimbili, ila `wanayafumbia macho’ kwa vile wengi wao wakiugua wanapelekwa kutibiwa nje ya nchi, hata kwa maradhi yanayoweza kutibiwa nchini.
Alisema kuzorota kwa huduma katika hospitali hiyo kumesababisha ongezeko la malalamiko kutoka kwa wagonjwa dhidi ya watumishi na madaktari wa MNH huku ari ya kufanya kazi (kutibu) ikipungua na wengine kukiuka misingi na maadili ya udaktari.
Daktari huyo alisema serikali imekuwa ikiipa fedha kidogo MNH, hivyo kushindwa kufanya kazi zake kwa ufanisi ikiwamo ununuzi wa dawa kutoka kwenye Bohari Kuu (MSD).
“Muhimbili haina fedha za kununua dawa za kutosha, madaktari wanapowaambia wagonjwa wakanunue dawa wenyewe hawafanyi hivyo kwa makusudi bali hali halisi ya hapa (Muhimbili) ndivyo ilivyo,” alisema.
SEWAHAJI
Katika wodi zilizoko kwenye jengo la Sewahaji, wagonjwa wanaonekana wakiwa wamelazwa sakafuni kwenye viambaza vya wodi hiyo karibu kabisa na lango kuu la kuingilia ndani.
Julai, Agosti na mwanzoni mwa Septemba mwaka huu NIPASHE ilipopita hospitalini hapo ilishuhudia wagonjwa wakizwa wamelazwa sakafuni hadi karibu na lango kuu la kuingilia kwenye wadi namba 1, wakati hali mbaya zaidi ikidhirika kwenye wodi namba 3 na 4 zinazotumiwa na wanawake.
Hali hiyo imekuwa ikisababisha msongamano mkubwa wodini inapofika muda wa ndugu na jamaa kuona wagonjwa.
Hali ya usafi wa vyoo wodi ya Sewahaji ni mbaya, licha ya kuwapo taarifa kuwa uongozi wa hospitali hiyo umekuwa ukitoa zabuni kwa kampuni kadhaa kufanya usafi unaokidhi viwango na kanuni za afya bora.
Mwandishi aliingia ndani ya vyoo hivyo na kubaini havikuwa na maji na vifaa vya kusukuma maji (flashi) havikuwa vinafanya kazi. Ndivyo ilivyokuwa kwa mabomba ambayo mengine yalikuwa na kutu.
Kutokana na ukosefu wa maji, wagonjwa na watu wanaowatembelea, wanatumia maji yaliyopo kwenye mapipa nje ya vyoo. Maji yanapokosekana kwenye mapipa hayo mhusika anawajibika kutafuta mahali kwingine ikiwamo nje ya jengo hilo.
Gazeti hili lilishuhudia baadhi ya vyoo vikiwa vimejaa uchafu katika majengo ya Sewahaji, Kibasila na Mwaisela huku vingi vikiwa katika hali mbaya ya uchakavu kutokana na kutumika muda mrefu bila kufanyiwa ukarabati.
MADAKTARI WAPATA TAABU KUHUDUMIA
Gazeti hili lilishuhudia madaktari na watumishi katika wodi hiyo wakivuka kwa shida kutoka mgonjwa mmoja kwenda kwa mwingine kutokana na mrundikano wa wagonjwa uliopo.
Mmoja wa wauguzi ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini, alisema kuwalaza wagonjwa sakafuni si jambo la kushangaza hospitalini hapo, na kwamba ni utaratibu wa muda mrefu unaosababishwa na idadi kubwa ya wagonjwa wanaofikishwa hapo kutoka hospitali mbalimbali nchini.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi hospitali hiyo hupokea wagonjwa 1,000 kwa siku, kwa wiki wagonjwa 7,064, kwa mwezi wagonjwa 28,258 na kwa mwaka wagonjwa 339,096.
“Hilo linaweza kuwa jambo la ajabu kwako, lakini hali hii haikuanza jana wala leo, wagonjwa wanaoletwa hapa ni wengi kama unavyowaona sasa,” alisema muuguzi huyo wa wodi ya Sewahaji.
Hali kama hiyo ilibainika pia kwenye wodi zilizopo kwenye jengo la Kibasila, hususani namba 2 ambayo ni maalum kwa wanawake.
NDUGU WATUMIKA KUTOA HUDUMA
Wagonjwa wanaohamishwa kutoka sehemu moja kwenda nyingine kwa ajili ya mahitaji kama vipimo, wamekuwa wakipelekwa na kurudishwa na ndugu na jamaa zao badala ya watoa huduma ya afya kama ilivyokuwa awali.
Taarifa zinaeleza kuwa hatua hiyo inahatarisha afya na maisha ya wagonjwa kutokana na baadhi ya wagonjwa kuhitaji uangalizi wa karibu wa mtaalamu wa afya badala ya mtu asiyekuwa na taaluma hiyo.
Miongoni mwa matukio yaliyobainika ni ndugu na jamaa wa wagonjwa kusukuma vitanda ama viti vya magurudumu matatu vinavyotumiwa na wagonjwa kuwahamisha kutoka sehemu moja kwenda nyingine.
Wakati hali ikiwa hivyo kwenye wodi na majengo hayo, gazeti hili lilishuhudia vitanda vingi vikiwa `vimetelekezwa’ nje ya jengo la watoto hospitalini hapo, vikihitaji matengenezo ambayo yangewezesha vitumike na kupunguza tatizo la wagonjwa kulazwa sakafuni.
JENGO LA WAGONJWA WA NJE
Wagonjwa wa nje wanaofika na kuondoka wanakabiliwa na tatizo la kutoonana na madaktari, hali inayowafanya watumie muda mwingi kufika hospitalini hapo bila mafanikio.
Hali hiyo inaelezwa kusababishwa na wingi wa wagonjwa usiolingana na idadi ya madaktari na wataalamu waliopo.
Mmoja wa wagonjwa waliohojiwa, Aisha Hussein alisema alifika hospitalini hapo alfajiri Julai 26, mwaka huu akiwa ‘amebanwa’ na kifua akitokea Tegeta jijini Dar es Salaam, lakini hadi kufikia saa nane mchana alikuwa hajahudumiwa.
Mgonjwa mwingine, Mathias Lwenge, ambaye anasumbuliwa na maradhi ya tumbo, alisema huduma katika jengo la wagonjwa wa nje zinasuasua kutokana na wingi wa wagonjwa wanaopata rufaa kutoka hospitali za wilaya jijini Dar es Salaam.
“Tumepata rufaa kutoka Hospitali ya Amana. Mwenzangu ameshachukuliwa vipimo, anasubiri majibu. Lakini mimi hadi muda huu (saa 9:30 alasiri) naendelea kusubiri na kama unavyoona watu walivyo wengi, sina hakika kama nitapata huduma leo hii,” alisema mgonjwa ambaye hakutaka jina lake litajwe.
Madaktari wanaowahudumia wagonjwa wa nje, wanatoa siku nyingi kwa wagonjwa kurejea tena hospitalini kupata huduma tofauti zikiwamo ushauri wa kitabibu na vipimo.
Madaktari hao wamekuwa wakifanya hivyo kutokana na wingi wa wagonjwa usiolingana na vifaa, wauguzi na madaktari waliopo katika hospitali hiyo.
Mmoja wa wagonjwa aliyepata rufaa kutoka hospitali ya St. Francis Ifakara, Athanas Joseph (72), ambaye anasumbuliwa na kibofu cha mkojo, alisema tangu Julai mwaka huu, amekuwa akifika MNH kwa ajili ya matibabu bila mafanikio.
Alisema, alifika MNH kwa mara ya kwanza Julai 25 na kutakiwa kurudi Agosti 12 ambako alifanyiwa upasuaji na kuambiwa arudi Agosti 27 kwa ajili ya vipimo vingine ikiwamo damu.
“Leo (Agosti 27), wamechukua vipimo, lakini wanatuambia turudi baada ya wiki tatu ambayo itakuwa Septemba 20, sasa mimi kwa hali yangu hii ilivyo mbaya, naambiwa nirudi baada ya wiki tatu… muda wote huu niendelee kuumia,” alisema.
Aliongeza: “Daktari aliangalia orodha ya wagonjwa kwenye kompyuta yake akasema wako wengi na ndiyo sababu akanipanga tarehe ya mbali, lakini sijui nitafikaje huko kutokana na hali yangu kuwa mbaya.
“Sina fedha za kuendelea kuishi hapa Dar es Salaam, na nauli za kwenda Ifakara na kurudi huku ni kubwa. Nashindwa la kufanya…sijaamua nikae au niondoke.”
UPATIKANAJI WA DAWA
Daktari mmoja wa watoto katika hospitali hiyo ambaye hakutaka jina lake litajwe, alisema maduka ya dawa katika MNH yapo kama ‘mapambo’ kwa vile hata dawa za msingi hazipatikani, hivyo kuna sababu kwa ndugu na jamaa wa wagonjwa kutakiwa kupata huduma hizo nje ya hospitali.
Alisema hali hiyo imedumu kwa muda mrefu na ingawa madaktari wamekuwa wakiueleza uongozi wa hospitali hiyo kuhusu malalamiko wanayopata kutoka kwa wagonjwa kwa kukosa dawa, hakuna hatua zilizochukuliwa.
“Nenda kawaulize wagonjwa kama wanapata dawa, nakuhakikishia hata wale wenye bima mbalimbali wanalazimika kununua dawa katika maduka binafsi ya nje, tunalalamikiwa sana,” alisema daktari huyo na kuthibitisha kuwapo malalamiko ya baadhi ya wagonjwa kutokuwa na fedha za kununua dawa.
Daktari mwingine, ambaye ni mtaalamu wa maradhi ya wanawake, alisema kutokana na kuzorota kwa huduma katika hospitali nyingi za serikali ikiwamo MNH, wagonjwa wengi wameamua `kukimbilia’ kwenye tiba mbadala.
TIBA MBADALA KIMBILIO
Alisema waganga wa tiba mbadala wamegundua udhaifu wa serikali katika kuhudumia wananchi hususani kwa masuala ya afya na wametumia fursa hiyo `kuchuma’ fedha za wagonjwa huku wengi wao wakiwa ni `matapeli’ wasiokuwa na utaalamu wa kutibu.
“Hauwezi kuwalaumu wagonjwa kwa kwenda katika tiba mbadala. Wamechoka na huduma mbovu za hospitali za serikali kama Muhimbili, mtu anakuja mwezi huu anaambiwa uje uonane na daktari mwezi ujao, mwingine anachukuliwa vipimo leo anaambiwa njoo baada ya wiki mbili,” alisema daktari huyo.
Daktari huyo, alisema madaktari wamekuwa wakilazimika kuwapa tarehe za mbali wagonjwa si kwa kuwakomoa bali kutokana na wingi wao, kwani uwiano baina ya daktari na wagonjwa nchini unatufautiana na viwango vilivyowekwa na Shirika la Afya Duniani (WHO).
Kwa mujibu wa daktari huyo, WHO inatambua kuwa daktari mmoja anatibu wagonjwa 10,000 kwa mwaka wakati kwa Tanzania ni wagonjwa 28,000.
“Hapa Muhimbili ni kama hakuna kitu, madaktari wanafanya kazi kwa sababu wanalipwa mishahara, lakini hakuna vifaa tiba wala dawa, tumelisemea hili mara nyingi na wizara inafahamu… madaktari wanafanya kazi katika mazingira magumu sana ila hakuna anayejali,” alisema daktari huyo na kuongeza:
“Sheria inakataza vyombo vya habari kurusha matangazo ya tiba asili na mbadala. Sasa matapeli wameuona udhaifu wa huduma za afya kwenye hospitali za serikali ambazo zilitarajiwa ziwe mkombozi kwa mwananchi wa kawaida, wamejitangaza kwa nguvu na wagonjwa wengi wamekimbilia huko,” alisisitiza.
Pia alisema kumeibuka wimbi la madaktari bandia wanaojitangaza kwenye vyombo vya habari na kuwapata wateja kwa sababu wagonjwa wameongezeka, vifaa tiba na madaktari wa kweli hawatoshi.
Sheria ya Waganga wa Tiba Mbadala ya mwaka 2002 inawazuia kujiita madaktari na kujitangaza kwenye vyombo vya habari, lakini hivi sasa ukiukwaji wa sheria hiyo upo dhahiri katika maeneo tofauti ya nchi.
MAT: HAKUNA ANAYEJALI
Rais wa Chama Cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk. Primus Saidia, anaunga mkono kauli za madaktari kuhusu hitaji la serikali kuyashughulikia madai ya madaktari hao ili kuepusha mgomo unaoweza kutokea na kuiathiri jamii.
“Ukimya wa madaktari si kwamba wameridhika na hali iliyopo hapa Muhimbili, kudhani hivyo ni kujidanganya maana ukweli ni kwamba hali si nzuri na madaktari wanalazimika kufanya kazi katika mazingira hayo kwa kuwa hawana namna,” alisema na kuongeza:
“Madai yao ya wakati ule hayajafanyiwa kazi zaidi ya kuwafukuza kazi Mganga Mkuu na Katibu Mkuu wa Wizara husika.”
Dk. Saidia alisema miongoni mwa madai ya madaktari ambayo hayajafanyiwa kazi ni pamoja na kutaka bima ya afya, kwa vile wengi wao (madaktari) wanapougua wamekuwa wakipata shida ya matibabu licha ya kwamba wanafanya kazi kwenye Hospitali ya Taifa.
“Unaweza kushangaa wanakuja wagonjwa hapa wana bima kubwa, sisi tunawapatia matibabu ya daraja la kwanza, lakini sisi tukiugua hatupati huduma nzuri ya matibabu kama ile tunayowapa wagonjwa wenye bima kubwa,” alisema Dk. Saidia.
Pia alisema madaktari waliomba kupatiwa chanjo ya maradhi ya kuambukiza kama homa ya ini, lakini ombi lao `limetupwa’ na serikali.
“Kwa ujumla mazingira yaliyokuwa yakilalamikiwa wakati ule yako vile vile.
Vifaa tiba havitoshi, dawa shida na tatizo la wagonjwa kulazwa sakafuni wodini limekuwa maisha ya kawaida hapa Muhimbili, hakuna anayejali,” alisema Dk. Saidia.
Alisema awali madaktari walikuwa na haki ya kupata nyumba kama ilivyo kwa watumishi wengine wa serikali, lakini haki hiyo iliondolewa na hivi sasa wamekuwa wakiishi maisha ya `kuhangaika’ mitaani.
Alisema madaktari 700 wanahitimu kila mwaka, lakini ajira zao zimekuwa za kusuasua, zenye vikwazo na kusababisha wengi kuachana na fani hiyo na kufanya biashara ama kwenda kufanya kazi nje ya nchi.
KUCHELEWA KWA MALIPO YA WITO WA DHARURA
Madaktari hospitalini hapo walisema kuchelewa kwa malipo ya wito wa dharura si jambo la kushangaza kwani umeshakuwa utaratibu wa kawaida ambao wameuzoea miaka `nenda rudi’ na kwamba wakati mwingine unapita mwaka bila kulipwa posho hizo.
Mmoja wa madaktari hao (jina tunalihifadhi) alisema kuchelewa kwa malipo hayo kunashusha ari ya watumishi wa MNH hasa wanapoitwa kufanya kazi kwa dharura.
“Madaktari hatuishi hapa, wengine wanakaa mbali na mji na hawana magari binafsi.
Sasa unapoitwa kwa dharura hasa usiku, kwanza unajiuliza utafikaje Muhimbili kama si kukodi usafiri halafu fedha zako unalipwa baada ya miezi tisa,” alisema daktari huyo.
Gazeti hili lilifanikiwa kuona waraka uliobandikwa kwenye matangazo ya hospitali hiyo Septemba 2, mwaka huu, unaoonyesha kuwa hadi muda huo madaktari na wauguzi walikuwa hawajalipwa malipo ya kuitwa kazini kwa dharura tangu Machi mwaka huu, (sawa na miezi sita iliyopita).
Waraka huo uliosainiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Dk. Marina Njelekela, ulisema hospitali hiyo ilikuwa ikiendelea kufuatilia malipo hayo Hazina, kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.
Waraka ulisema kuwa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imepata malipo ya kuanzia Machi na June mwaka huu, hivyo malipo hayo yanaweza kuwasilishwa Muhimbili na kusambazwa kwa wanaodai kama watakuwa wamewasilisha madai yao kwenye idara ya fedha.
MGANGA MKUU: TUNAATHIRIWA NA MIUNDOMBINU
Aliyekuwa Mganga Mkuu wa Serikali, Dk. Donan Mmbando (hivi sasa ndiye Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii), alithibitisha kuwapo kwa `utitiri’ wa wagonjwa katika hospitali hiyo na kufafanua kuwa hali hiyo inatokana na huduma zake kutopatikana katika hospitali za mikoa na wilaya nchini, wakiwamo madaktari bingwa, na hivyo `kuwavutia’ wagonjwa wengi.
Alisema ni kweli hospitali hiyo imekuwa ikifurika wagonjwa kupita uwezo wake kiasi kwamba wengine wanalazwa sakafuni, sababu kubwa ikiwa ni miundombinu iliyopo kutokukidhi mahitaji ya sasa.
Hata hivyo, alisema serikali inafanya jitihada zinazolenga kukabiliana na hali hiyo, ikiwamo kuziimarisha hospitali za wilaya na mikoa.
“Muhimbili ni kilele cha huduma za afya hapa nchini na ndiyo sababu unaona idadi kubwa ya wagonjwa, pale hata ukiongeza majengo hali itabaki vile vile,” alisema na kuongeza:
“Tunachokifanya ni kuboresha huduma za hospitali za manispaa, mikoa na wilaya kwa kuziwezesha kuwa na majengo, vifaa tiba na wataalamu. Lakini kinachotukwamisha ni uhaba wa fedha,” alisema Dk. Mmbando.
Alisema mpango wa serikali ni kuongeza pia madaktari bingwa katika hospitali hizo katika nyanja za upasuaji, kina mama, mifupa na watoto ili huduma husika zitolewe huko badala ya wagonjwa wote kupelekwa Muhimbili.
“Tunataka kuondoa mrundikano Muhimbili, maana madaktari bingwa wa kutosha wakiwapo kwenye hospitali hizo (za wilaya na mikoa) wataweza kutoa huduma zinazohitaji utaalamu wa hali ya juu kama upasuaji ama huduma za kitaalamu zaidi ambazo wagonjwa walikuwa wakiletwa Muhimbili, hiyo itasaidia kupunguza msongamano,” alisema Mmbando ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Madaktari Tanzania.
UPUNGUFU WA DAWA
Dk. Mbando alisema ni kweli kumekuwa na upungufu mkubwa wa dawa katika hospitali ya Muhimbili, kwani wamekuwa wakipeleka bajeti katika Bohari Kuu ya Dawa (MSD), lakini wanakwamishwa kutokana na uhaba wa fedha.
Alisema asilimia 80 ya dawa zinazotumika nchini zinaagizwa kutoka nje ya nchi, hali inayosababisha gharama kuwa kubwa ikilinganishwa na uwezo wa kifedha wa serikali katika kuhimili mahitaji halisi.
Alisema, baada ya serikali kubaini tatizo hilo wameanzisha ‘bajeti mbadala’ ambapo fedha za Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF) na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) zimekuwa zikitumiwa kununua dawa kutoka MSD kwa makubaliano maalum na serikali.
“Zamani walikuwa wakitumia fedha hizo wanazopata kutoka mifuko hiyo kununua dawa wenyewe, lakini tulibaini kuwa hawanunui sasa tumeanzisha utaratibu mpya. Asilimia 50 ya madai yote ya hospitali za serikali kutoka CHF na NHIF yanapelekwa moja kwa moja MSD na hizi hospitali zinapatiwa dawa tu,” Dk Mmbando alisema na kuongeza:
“Kwa sababu zamani walikuwa hawanunui dawa za kutosha na hela zinabanwa, sasa tunadhani mfumo huu mpya utasaidia dawa zipatikane kwenye hospitali zetu ikiwamo Muhimbili,” alisema.
Alisema utaratibu huo mpya umeanzishwa miezi miwili iliyopita baada ya kubaini upungufu mkubwa wa dawa katika hospitali hizo na malalamiko ya wagonjwa kukosa dawa.
WIZI wa DAWA
Dk. Mmbando alisema ni kweli baadhi ya watumishi wamekuwa wakila njama na kuiba dawa za serikali, hivyo kusababisha wagonjwa kukosa baadhi ya dawa muhimu wanazoandikiwa na madaktari wanapokwenda kwenye hospitali za serikali ikiwamo MNH.
Alisema baada ya serikali kubaini wizi huo imeanzisha utaratibu mpya wa kuziweka `lebo’ dawa zote zinazotoka MSD ikiwa ni pamoja na kila kidonge, tofauti na ilivyo kuwa zamani ambapo `lebo’ ya MSD ilikuwa ikiwekwa kwenye kasha la kuhifadhia dawa tu.
“Dawa nyingi zimechepushwa na watu wasio waaminifu na hii inachangia sana uhaba wa dawa kwenye hospitali zetu… sasa badala ya kuweka alama ya MSD kwenye kopo la dawa hata vidonge vilivyomo ndani tumeamua kuvibandika alama na vyenyewe vimeandikwa TG/MSD tunaamini itasaidia kupunguza kama si kumaliza wizi uliokuwa ukifanywa,” alisema Dk. Mmbando.
Katika hatua nyingine ya kukabiliana na upungufu wa dawa, Dk. Mmbando alisema serikali imeanza mazungumzo na wawekezaji wanaotaka kuja kuwekeza kwenye kuzalisha dawa hapa nchini hali itakayosaidia kupunguza mzigo mkubwa wa kuagiza dawa nje ya nchi.
GHARAMA KUBWA ZA VIPIMO
Dk. Mmbando alikiri kuwa gharama za vipimo mbalimbali zimekuwa kubwa hali inayowatesa wananchi wa kawaida wanapokwenda kufuata huduma katika hospitali za serikali na za binafsi.
Aliyasema hayo alipoulizwa kuhusu gharama kubwa za vipimo mbalimbali vikiwamo vya MRI na CT SCAN vinavyofikia hadi Sh 450,000 katika hospitali ya Muhimbili ambayo imekuwa ikifurika wagonjwa wanaotoka tabaka la chini.
Alisema katika mkutano na waganga wakuu wa mikoa yote nchini uliofanyika mkoani Morogoro hivi karibuni, wamebaini tatizo hilo na wamejaribu kurekebisha gharama za dawa na vipimo mbalimbali ili kuleta usawa katika utoaji wa huduma za afya.
Alithibitisha kuwa ni kweli gharama za vipimo mbalimbali ni kubwa na kwamba watajitahidi kudhibiti gharama hizo hata kwenye hospitali binafsi ili kuwatendea haki wananchi wengi wanaokwenda kupata huduma za afya ambao wengi wao wana vipato vidogo.
“Wagonjwa hawapaswi kuadhibiwa kwa shida zao, tumepanga turekebishe gharama hizo ili tusiwaadhibu wananchi maana tumegundua gharama kubwa za vipimo kama MRI na CT SCAN, kuna hospitali zinatoza hadi Sh. 700,000, sasa mwananchi wa kawaida unamuumiza,” alisema Dk. Mmbando.
Uchunguzi ulibaini kuwa vipimo vya CT SCAN na MRI kwa hospitali ya Muhimbili vinaanzia Sh 250,000 hadi Sh 450,000 kulingana na maeneo ambayo mgonjwa anapaswa kupimwa, wakati kwenye baadhi ya hospitali binafsi hufikia hadi 700,000.
KUCHELEWESHWA POSHO ZA KUITWA KWA DHARURA
Kuhusu malalamiko ya madaktari ya kuchelewa kulipwa posho za kuitwa kwa dharura, Dk. Mmbando, alisema utaratibu wa zamani ulikuwa ukiruhusu hali hiyo kutokea, lakini mabadiliko yaliyofanyika posho hizo zitakuwa zikifika kwa wakati.
Alisema awali, fedha za malipo hayo zilikuwa zikichanganywa na za matumizi mengine, lakini kwa sasa zinawekwa pamoja na fedha za mishahara na malipo ya madaktari wanafunzi hivyo zinapohitajika inakuwa rahisi kuwafikia walengwa tofauti na utaratibu wa zamani.
Kuhusu posho ya nyumba kwa madaktari, Dk. Mmbando alisema walishapeleka mapendekezo ya kuziboresha kwenye Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma) na kurejeshwa kwa posho ya nyumba kwa madaktari iliyoondolewa, lakini hawajajibiwa.
“Kwa sasa madaktari wanaopata posho ya nyumba ni wale wanaofanya kazi za kiutawala, ila sasa tumependekeza ile posho ya nyumba kwa madaktari wengine iliyoondolewa miaka ya nyuma irejeshwe ili iongeze motisha na serikali haijatupa majibu bado, tunasubiri,” alisema.
MUHIMBILI IKO HOI KIUCHUMI
Mkurugenzi Mkuu wa Muhimbili, Dk. Njelekela alikataa kuzungumza na mwandishi wa habari hizi, licha ya kufuatwa ofisini kwake kwa zaidi ya mara tano.
Hata hivyo, chanzo cha habari hospitalini hapo kilisema mazingira yote yanayosababisha utoaji wa huduma kuwa mbovu hospitalini hapo ni kuwa hoi kiuchumi kutokana na kuhudumia wagonjwa wengi wa misamaha kama vile watu wazima wa umri unaoanzia miaka 60, watoto wa chini ya miaka mitano na wajawazito wanaokaribia kujifungua na wagonjwa wanaopelekwa hospitalini hapo ambao hawana ndugu na jamaa.
“Misamaha ya matibabu ni mingi, sasa chanzo cha mapato kiko wapi? Watu wasiojiweza, ama kaja mtu kagongwa na gari na hana ndugu, inabidi atibiwe tu maana huwezi kumwacha akafa. Sasa hayo yote yanasababisha hospitali inazidiwa na kukosa fedha za kununua dawa na vifaa tiba,” kilisema chanzo chetu kutoka Muhimbili.
Aidha, alisema pamoja na kuhudumia wagonjwa wengi bure, hospitali hiyo inapata mgawo kidogo kutoka serikali kuu, jambo linalokwamisha shughuli nyingi kufanikiwa.
“Mahitaji ya Muhimbili ni makubwa sana. Wanatakiwa kuwa na dawa za wagonjwa wa nje, waliolazwa, vifaa tiba kama x-ray, gloves na vingine vingi, lakini havipo kwa sababu serikali haitoi fedha zinazotengwa kwa ajili ya hospitali hii,” alisema na kuongeza hivi sasa MSD inaidai Muhimbili mabilioni ya fedha.
“Fedha zinazopatikana kutoka kwa wagonjwa binafsi ndizo zinatumika kununulia vifaa tiba, lakini dawa huwa siyo kipaumbele kwa sababu fedha hizo hazipo,” kilisema chanzo hicho.
Alisema kwa hali hiyo, madaktari huwataka wagonjwa kununua vifaa kama gauze ili kufanyiwa upasuaji au reagent kwa ajili ya vipimo vinavyotakiwa kuwapo hospitalini hapo.
Alisema hospitali hiyo imekuwa ikikopa dawa na vifaa tiba kutoka MSD hadi kukaribia hatua ya kuifilisi, kwani deni lake ni kubwa na linaongezeka siku hadi siku.
“Angalia hospitali kubwa kama Muhimbili ilivyotelekezwa, imekopa dawa na vifaa tiba MSD hadi sasa hivi Muhimbili haikopesheki tena maana hazina hawajawapa fedha kwa muda mrefu. Sasa dawa na vifaa tiba wananunua kwa fedha za nani?”alihoji.
MKAKATI WA KUDHIBITI WIZI WA DAWA
Mkurugenzi wa Manunuzi wa MSD, Heri Mchunga, alisema taasisi hiyo ilibaini dawa kutofika kama inavyokusudiwa kwenye hospitali mbalimbali ikiwamo Muhimbili, hivyo wakaanzisha utaratibu wa kuzisafirisha wenyewe (MSD) hadi kwenye hospitali husika.
Mchunga ambaye wakati anazungumza na gazeti hili alikuwa akikaimu nafasi ya Mkurugenzi Mkuu wa MSD, alisema awali wahusika walikuwa wakizifuata dawa na vifaa tiba kutoka ofisini hapo, lakini baada ya kubaini dawa nyingi `kuishia katikati’ walibadili mbinu.
“Tunapaswa kujiuliza dawa zinapotelea wapi maana zikitoka hapa zinakwenda hospitali ama kituo cha afya kisha zinakwenda kwa mgonjwa, sisi MSD tumedhibiti kwa asilimia 100 kwa kuhakikisha dawa zinafika kunakohusika kama zilivyotoka hapa na kupokelewa na kamati ya hospitali, sasa inaonyesha kuna baadhi ya watumishi katika hospitali husika wanakula njama za kutorosha dawa hizo,” alisema.
MAJIBU RASMI YA HOSPITALI YA MUHIMBILI
Uongozi wa hospitali hiyo ulikataa kuzungumza na mwandishi wa habari hii ukitaka upelekewe maswali, na ulipopelekewa maswali hayo majibu yalikuwa haya.
Kuhusu deni ambalo (MNH) inadaiwa na Bohari Kuu ya Dawa, uongozi wa hospitali hiyo katika majibu yake kwa mwandishi wa habari hizi ulisema deni limefikia Sh 3,539, 379,530 ambalo hadi leo Hazina haijalilipa Bohari Kuu ya Dawa.
Hata hivyo, kwa mujibu wa uchunguzi wa shirika lisilo la kiserikali la Sikika uliotangazwa Oktoba 26 na Mkurugenzi wa shirika hilo, Irenei Kiria, MSD inaidai Muhimbili Sh. bilioni 8 na deni hilo linatokana na malimbikizo ya gharama za dawa na vifaa tiba.
Aidha, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Seif Rashid alikiri mbele ya Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii kuwa serikali inadaiwa na MSD jumla ya Sh. bilioni 102 na kwamba, tayari imeanza kulipa deni hilo kwa kupeleka Sh. bilioni 10.7 kwa kipindi cha kuanzia Julai hadi Oktoba, 2014.
Kuhusu wagonjwa kulala chini wodini, uongozi huo ulisema ni kweli wagonjwa wanapozidi wanalala chini kwenye magodoro kwa sababu hakuna nafasi zaidi ya kuweka vitanda wodini na wagonjwa ni wengi sana kuliko vitanda vilivyopo. Ulisema tatizo hilo litatatuliwa hapo serikali itakapoongeza jengo lingine la wodi za wagonjwa.
Kuhusu malalamiko ya wagonjwa kukosa dawa, majibu ya Muhimbili yalisomeka hivi: ”Inategemea na aina ya mgonjwa…..kama ni mgonjwa wa binafsi (private) au wa Bima tatizo ni letu, ila Kama ni mgonjwa wa umma tatizo ni la MSD ambako serikali inapeleka hela yote ya madawa na vifaa tiba kwa ajili ya wagonjwa wa umma.
“Wagonjwa wa Bima wanalipiwa huduma za matibabu na Bima na wale wa binafsi wanalipa hela taslimu ya matibabu kwa hiyo wagonjwa wa aina hizi mbili tunatakiwa hospitali inunue dawa ili wao wanunue kwenye maduka yetu au wachukue dawa na bima zao zilipe.”
“Kwa sasa hospitali imejipanga na tumetenga akaunti maalum kwa ajili ya kununua dawa za wagonjwa wa makundi haya mawili. Pia tumeingia kwenye makubaliano na wauzaji mbalimbali wa madawa ambao wanatuletea dawa kwa wingi kuhakikisha kwamba dawa haziishi kwenye pharmacy za wagonjwa wa makundi haya mawili,” ilisema taarifa hiyo.
Aidha, sehemu ya taarifa hiyo ilisema kwa wagonjwa wa umma, kilichotokea ni kwamba serikali ilipeleka hela MSD na hospitali hiyo ikawa kwa mwaka mzima inachukua dawa nyingi MSD kupita hela waliyopelekewa na serikali na hadi sasa MSD wanaidai hospitali hiyo.
“Kwa hiyo MSD wamesema sasa hivi tukitaka dawa kwao inabidi tupeleke cheque ndipo watupe dawa. Na hali halisi sasa ya hospitali ni mbaya sana, hatuna pesa ya kupeleka MSD kununua dawa za wagonjwa wa public (umma) ambao huwa hawalipii kabisa dawa hapa hospitalini.
Wagonjwa wa public kwa hapa Muhimbili wanalipia Sh. 10,000 ya kufungua file, basi. Vipimo vyote na dawa wanapewa bure na kama ni wa kulazwa wodini huwa wanalipa Sh. 20,000 tu na vipimo na dawa wanapewa bure isipokuwa CT scan na MRI ndiyo wanachangia kidogo,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Kuhusu uchafu uliobainika vyooni hasa vile vya wodini, taarifa ilisema siyo vichafu ila vimechakaa kutokana na material iliyowekwa kuwa ni ya aluminium.
Kuhusu maji, ulisema yanakatika mara moja moja kama sehemu nyingine, hata hivyo hospitali inafanya juhudi ya kuchimba visima kwa ajili ya kuongeza maji.
Kuhusu kuchelewa kwa huduma na wagonjwa kupangiwa tarehe za mbali kwa ajili ya kuwaona madaktari, uongozi ulisema tatizo kubwa lililopo ni kwamba wagonjwa ni wengi kuliko idadi ya madaktari, hivyo inabidi madaktari wajigawe kadri wawezavyo ili kuhudumia wagonjwa wote waliopo.
Taarifa hiyo ilisema wagonjwa wanaopata chakula ni wale waliolazwa, waliopata rufaa kutoka mikoani na kuja kutibiwa hospitali ya taifa Muhimbili na hawana ndugu wa kuwahudumia kwa chakula hapa Dar es Salaam. Wengine ni wagonjwa wote wa akili na watoto.
Kuhusu malipo ya kuitwa kazini kwa dharura, ilisema zimeshalipwa hadi Juni mwaka huu na kwamba malipo hufanyika baada ya kupokea fedha kutoka wizarani.
Shuka za wagonjwa zinaonekana ni za mwaka 47, huwa zinaondolewa baada ya muda gani?
Uongozi ulisema mashuka ya wagonjwa yanabadilishwa kila siku na kupelekwa kufuliwa, kunyoshwa na kisha hurudishwa tena wodini kwa matumizi na huondolewa kwenye mzunguko zinapochanika.
Katika madai ya madaktari mwaka 2011, madaktari walipendekeza viwango vifuatavyo kwa posho mbali mbali kwa asilimia ya mshahara kwenye mabano: muda wa ziada wa kazi (5), kufanya kazi katika mazingira magumu (40), makazi (40) na posho ya kufanya kazi katika mazingira hatarishi (30).

CHANZO: NIPASHE
3 comments:
Nafikiri ndiyo maana rais aliamua kuja Marekani kutibiwa.
Kwanini hawa wagonjwa hawaendi India.
Fanya harambee WaTanzania dunia nzima watatoa.
Post a Comment