Advertisements

Sunday, November 23, 2014

Sakata la ardhi Loliondo: Wafugaji sasa watishia kuinyima kura CCM

Mwenyekiti wa Halmashauri ya CCM Wilaya ya Ngorongo, Mkoa wa Arusha, pamoja na madiwani wake wamesema wamechoka kwa vitendo vya usumbufu, unyanyasaji na kuishi maisha yasiyoeleweka kufuatia hatua ya Waziri wa Maliasili na Utalii kutaka kutwaa ardhi yao.

Wamesema malengo hayo ya waziri yakitekelezwa wapo tayari kurudisha kadi zote za CCM na kuwaeleza wananchi wao katu wasiwapigie kura wagombea wote wa chama hicho.

Walisema serikali kupitia Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, ilitangaza rasmi kutenga eneo la kilomita za mraba 1,500 ya ardhi ya vijiji kuwa Pori Tengefu la Loliondo, jambo walilosema limezua taharuki kubwa ndani na nje ya nchi na kutishia usalama kwenye jamii ya wafugaji na hatimaye kumalazimu Waziri Mkuu kuilingilia kati.

“Waziri Nyalandu amezuri Loliondo mara mbili kwa nia ya kuhamasisha na kushawishi madiwani na wenyekiti wa vijiji kukubali pendekezo la serikali/OBC kutoa fidia ya Sh. bilioni moja kwa vijiji endapo watakubali kuachia eneo la kilomita za mraba 1,500. Pendekezo lake halijakubaliwa hata na viongozi wachache aliokutana nao,” alisema Mwenyekiti wa Halmashauri ya Ngorongoro, Elias Ngorisa.

Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ngorongoro, Ibrahim Sakai, alisema hazina ya kura za CCM zipo kwa jamii ya wafugaji wa Kimasai, lakini ikitokea wananyang’anywa ardhi yao, wanaweza kuhama CCM.

Akisoma tamko lao kuhusu mgogoro wa ardhi Loliondo, alipinga madai ya Waziri Nyalandu, kuwa ziara zake Loliondo zimekuwa za kuhamasisha matumizi ya ardhi ya vijiji.

Lakini kwa upande wake wanasema amekuwa akienda Loliondo kuhamasisha wananchi wa huko kukubali kulipwa fidia pale maeneo yao yatakapochuliwa na serikali.

Kufuaitia mkanganyiko huo, mwenyekiti na madiwani wake wameishauri serikali kufuta uwindaji katika ardhi yao kwani hauhifadhi wanyamapori wala sio rafiki na mazingira, ufugaji na utalii wa picha.

Alisema uwindaji katika eneo la Loliondo ni mpango wa kuwamaliza wanyama katika ikolojia ya Serengeti, Ngorongoro na Maasai Mara, hivyo kuendelea kuruhusu uwindaji katika eneo hilo, mgogoro utaendelea na kusababisha madhara endelevu kwa uhifadhi wa wanyamapori, maisha na ustawi wao.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments: