Advertisements

Saturday, November 8, 2014

TULIZA AKILI, NDO UNAANZA MAISHA!

NIANZE kwa kuwapa pole sana madenti wa kidato cha nne kwa kufanya mitihani ya kumaliza elimu yao, nchi nzima. Miaka mingi iliyopita, nami pia nilikuwa katika chumba cha mitihani, nikifanya kile ambacho vijana wa enzi hizo na hata sasa, mnaita ‘paper’.

Wakati ule, kwangu mitihani hata sikuona kama kilikuwa kitu muhimu, kwa sababu home mambo yalikuwa mazuri tu, tunakula, tunalala na kila wikiendi disko kama kawa. Ingekuwa hivi sasa, ningesema kwetu kulikuwa tambarare.

Ingawa sikuwa na mchecheto na mitihani kwa sababu kichwani kidogo nilikuwa vizuri, lakini bahati mbaya sana sikuichukulia kwa umakini mkubwa, niliona ni kama mitihani mingine ya mwisho wa wiki, mwezi na hata muhula. Sema tofauti niliyoiona ni wale wasimamizi kuwa makini na nje kuna askari mwenye silaha!

Ninapokumbuka hivi sasa wakati vijana wakiwa ndani ya vyumba vya mitihani nchi nzima, ninajikuta nikiwa na haja ya kusema nao kidogo, ingawa nilipaswa kufanya hivi mapema kabisa kabla hawajaanza. Hata hivyo, bado sijachelewa kwa sababu neno litabaki kuwa neno hadi lisemwe.
Ninachotaka kuwaambia, na hiki ni kama nyongeza kwa sababu nimekuwa nikisema mara zote, mitihani hii ndiyo mwanzo wa maisha yao. Unapofaulu au kufeli, ni kipimo kizuri kwa hali yako ya baadaye.

Mara kwa mara ninawaambia, mimi ni mfano mzuri sana wa jinsi dharau za shule zilivyoni-cost, kwa sababu nilipigika bila sababu za msingi, maana wale niliokuwa nao skuli, ambao kipindi hicho niliwaona washamba kwa kujifanya wanasoma sana, hivi sasa wanakula maisha hadi wanakera!

Kwa maana hiyo, nataka kusema kuwa madenti waingie katika vyumba vya mitihani wakiwa na akili kwamba hicho ni kipimo chao kikubwa kabisa katika kuona dalili ya maisha yao. Wasiingie darasani kama kutimiza wajibu tu kwa sababu labda kwao mambo safi. Wasidanganyike na mambo safi ya home kwa sababu yale ni maisha ya wazazi wao.

Wazazi wao walitengeneza maisha yao kwa sababu zao. Tunakosea sana kuishi kwa kuwategemea life ya wazazi. Nina mifano mingi ya vijana ambao enzi zetu walikuwa wanaringa kutokana na wazazi wao kuwa vizuri, wana nyumba nzuri, magari na uwezo mzuri wa kifedha.

Walitamba na kutudharau, lakini mwisho wa siku wazazi wao walizeeka, uwezo wao wa kutafuta ukafifia na wao hawakuwa na uwezo wa kuendeleza miradi yao, walizoea kutumia tu. Hivi sasa huwezi kuamini, mimi kapuku ninaishi vizuri kuliko wao kwa sababu angalau elimu kidogo niliyopata, ilinisaidia kujitambua na hivyo kuanza pilikapilika bado mapema.

Ninawashauri wafanye mitihani yao kwa umakini, waone paper hii ni tofauti na zingine zote walizowahi kufanya kwa sababu hii, itaamua kama waendelee na masomo au ndiyo mwisho. Elimu ya kidato cha nne, kwa maisha ya sasa, bado ni ndogo ambayo haiwezi kuwa msingi mzuri sana wa maisha.

Tatizo ya elimu yetu bado inatuelekeza kwenye kuajiriwa, sasa ili angalau uwe na sifa ya kuajiriwa, uwe na cheti cha kidato cha sita na kuendelea kwa sababu kazi zenyewe ni chache halafu wanaotafuta ni wengi. Si mnajua, kila mwaka maelfu ya kaka na dada zenu wanamaliza elimu ya vyuo vikuu na wote hao wanategemea kuajiriwa na ofisi zenyewe ndiyo hizi hizi, haziongezeki.

Nimalizie kwa kuwapa hongera sana wanangu waliomaliza darasa la saba ambao matokeo yao yalitoka mwanzoni mwa wiki hii. Ninajua wengi wamefaulu kuelekea kidato cha kwanza. Nao yawapasa kujiandaa kwa mwanzo wa masomo mwakani. Muwe na wikiendi njema!

GPL

No comments: