ANGALIA LIVE NEWS

Friday, November 21, 2014

UFANYEJE MWENZI WAKO ANAPOKOSA HAMU YA TENDO?

Yatupasa kumshukuru Mungu kwa kutujalia kuiona tena siku ya leo, najua ni wengi waliitamani nafasi hii lakini hawajaipata.Ni matumaini yangu kwamba msomaji wangu uko poa, karibu tena katika busati zuri la mahaba, mahali tunapobadilishana mawazo, kujuzana na kuelimishana kuhusu mambo mbalimbali yahusuyo uhusiano wa kimapenzi.

Mada ya leo ni maalum kwa wanandoa au watu waliopo kwenye uhusiano unaotambulika. Inahoji; nini cha kufanya mwenzi wako anapokosa hamu ya kuwa na wewe kwenye tendo la ndoa? Sanaa ya mapenzi ni pana sana, ndani yake kuna changamoto nyingi ambazo unapaswa kuwa na upeo wa ziada kuweza kuzitambua na kupambana nazo.

Tatizo la kukosa hamu ya kukutana kimwili ni pana lakini ili tuelewane vizuri, ningependa kulizungumzia katika makundi makuu mawili; upande wa wanawake na upande wa wanaume.

KUKOSA HAMU YA TENDO KWA WANAWAKE
Wanaume wengi wanapoingia kwenye ndoa, akili zao huzielekeza kwenye urahisi wa kupata haki yao ya ndoa muda wowote wanaohitaji kufanya hivyo. Wanaamini kwamba wanawake wapo kwa ajili ya kuwaburudisha na inapotokea wakakumbana na hali tofauti, ikiwemo ya mwanamke kukosa utayari na msisimko wa tendo, huanza kufikiria tofauti kwamba huenda wameanza kusalitiwa.

Ukosefu wa maarifa ndiyo unaosababisha hali hii, kwamba mwanaume anaamini muda wote atakaojisikia kuwa na mkewe faragha, bila kujali utayari wa mwenzake, basi mwanamke hatakiwi kuwa na kipingamizi chochote.

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Dr. Sheryl Kingsberg, mshauri wa mapenzi na mtaalamu wa saikolojia ya uhusiano, kati ya asilimia 50-70 ya wanawake waliopo kwenye ndoa, huwa wanabakwa na waume zao.

Kwa tafsiri nyepesi, wanaingiliwa kimwili na waume zao bila kuwa na utayari lakini wanashindwa kukataa kutokana na mila na tamaduni zao. Katika utafiti huo, mtaalamu huyo anaenda mbali zaidi na kueleza kuwa wanawake wote wenye umri wa kuanzia miaka 18- 59, hupitia katika kipindi cha kukosa msisimko na utayari wa kufanya tendo la ndoa mara kwa mara kwenye maisha yao, kabla na baada ya ndoa.

NINI HUSABABISHA HALI HII?
Zipo sababu nyingi zinazosababisha tatizo la kukosa hamu ya tendo kwa wanawake. Msongo wa mawazo unatajwa kuongoza kwa kusababisha tatizo hili. Pia migogoro ya kimapenzi, matatizo ya homoni na kutoridhishwa kimapenzi, ni sababu nyingine zinazotajwa kuchangia mwanamke kupoteza msisimko na hamu ya kuingia faragha na mwenzi wake.

Hata hivyo, sababu huwa hazifanani kwa kila mmoja, kila mwanamke ana sababu iliyomfanya akafikia hatua ya kukosa hamu ya tendo la ndoa na kama asipopata ushauri wa kitaalamu, au kuzungumza na mwenzi wake kurekebisha tatizo hilo, hali huzidi kuwa mbaya kiasi cha kusababisha ndoa nyingine kuvunjika.

DALILI ZAKE NI ZIPI?
Zipo dalili za wazi na nyingine za kificho ambazo huashiria kwamba mwenzi wako amepoteza msisimko na hamu ya tendo akiwa na wewe. Yawezekana kila siku wewe ndiye unayemuanza mkiwa faragha na usipomuanza, basi siku itapita kimyakimya. Hiyo ni dalili ya kwanza. Dalili nyingine kubwa ni kuhisi maumivu makali wakati wa tendo.

Ukiziona dalili hizi na nyingine nyingi zikiwemo kila siku kusingizia anaumwa tumbo au kichwa ili usimguse, basi ujue kuna tatizo hapo na badala ya kuwa mkali au kumhisi kwamba huenda anachepuka, unapaswa kumsaidia ili arudi kwenye hali yake ya kawaida.

Ili kujua nini unapaswa kufanya kumsaidia mwenzi wako ili wote mrudi kwenye hali ya kawaida na kuyafurahia mapenzi, usikose kufuatilia mwendelezo wa mada hii wiki ijayo.
GPL

No comments: