Advertisements

Sunday, November 16, 2014

Urais CCM kazi pevu

Dar es Salaam. Wakati joto la urais ndani ya CCM likiendelea kupamba moto, watu watakaoingia kundi la tano bora ambalo litapitishwa na Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC), wamefahamika.
Uchambuzi uliofanywa na makada mbalimbali wa chama hicho unaonyesha kuwa makundi hayo ambayo yatatoa wagombea mmoja, ni kundi la wagombea vijana, kundi la kifo, kundi la waziri mkuu aliyepo madarakani, wagombea wanawake na kundi la wagombea kutoka Zanzibar.
Kila kundi katika hayo litatoa mgombea mmoja ambaye jina lake litapelekwa kupitishwa kwenye mkutano wa NEC kupitishwa kabla ya kupigiwa kura kwenye Mkutano Mkuu wa CCM (CC).
Kundi la Vijana
Uchambuzi unaonyesha kwa vyovyote vile CCM lazima iteue jina la mgombea kijana hata kama watakuwa hawamtaki ili kuonyesha kuwa chama hicho kimekomaa na kinawapa moyo vijana kuwania nafasi za uongozi.
Wanasiasa vijana wa CCM ambao tayari wametangaza nia ya kuwania nafasi ya urais ni Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia, January Makamba na Mbunge wa Nzega, Dk Hamis Kigwangalla.
Wengine ambao wamekuwa wakitajwa katika kundi hilo ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, Mbunge wa Songea Mjini, Dk Emmanuel Nchimbi, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.
Kundi la vijana linatarajiwa kuwa na nguvu wakati wa mchakato huo, kutokana na kauli ya hivi karibuni ya Rais Jakaya Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM ambaye anaonekana dhahiri kulipigia chapuo.
Rais Kikwete akizungumza wakati wa maadhimisho ya Sikukuu ya Mwalimu Nyerere Oktoba 14 mwaka huu mjini Tabora, aliwataka vijana kumchagua mtu anayefanana na kijana kurithi nafasi yake.
Alirejea kauli hiyo alipokuwa akilihutubia taifa kupitia wazee wa Mkoa wa Dodoma Novemba 4, mwaka huu pale aliposema licha ya kauli yake ya awali kuwakera baadhi ya watu, lakini bado kuna umuhimu wa vijana kupewa nafasi za uongozi.
Kundi la kifo
Kuna kundi lingine la wazi ambalo mgombea yeyote anaweza kulitumia kugombea kuwania nafasi hiyo ya uongozi wa juu wa nchi.
Kundi hili ndilo linatajwa kuwa gumu zaidi kwa wagombea kwa sababu huwa lina idadi kubwa ya wanaojitokeza, wengi wakiwa viongozi wastaafu au wale waliomo ndani ya serikali pamoja na waliowahi kushindwa katika michakato iliyotangulia.
Kutokana na ugumu wa kundi hili baadhi ya watu ndani ya chama wamelipachika jina la kundi la kifo.
Baadhi ya makada ambao wapo katika kundi hili ni pamoja na Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa na mtangulizi wake katika nafasi hiyo, Frederick Sumaye, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu), Profesa Mark Mwandosya, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.
Wegine ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Steven Wasira, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa Bunge Maalumu, Samuel Sitta, Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe.
Kundi la Waziri Mkuu
Waziri Mkuu aliyepo madarakani siku zote CCM imekuwa ikimpa nafasi ya kuingia katika majina ya wagombea watano ambayo hupelekwa NEC ili yachujwe na kubakia matatu.
Kumbukumbu zinaonyesha kuwa mawaziri wakuu wote ambao wamewahi kuchukua fomu za kuwania nafasi ya urais, CCM ilipitisha majina yao kuingia katika tano bora.
Kinachosababisha CCM ilazimike kutoliacha jina la waziri mkuu aliyepo madarakani ni kuohofia wananchi kukiona chama kuwa hakiko makini hasa pale inapofikia hatua ya kushindwa hata kumwamnini waziri mkuu wake.
Mawaziri wakuu ambao waliwahi kuchukua fomu na kupitishwa majina kuingia mkutano mkuu ni Cleopa Msuya mwaka 1995 na Sumaye 2005. Historia hiyo inampa nafasi Waziri Mkuu wa sasa, Mizengo Pinda ambaye tayari ametangaza nia ya kuwania nafasi hiyo, fursa ya kusonga mbele.
Kundi la Wanawake
Kwa vyovyote vile CCM lazima itapitisha jina la mgombea mwanamke kuingia katika tano bora kwa sababu chama hicho kitataka kuonyesha kuwa kinazingatia jinsi kama sehemu ya demokrasia.
CCM inataka kuonyesha kuwa wanawake wanachukua nafasi za juu za uongozi wa nchi ili kuonyesha dunia kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa katika ushirikishwaji wanawake.
Kutokana na hali hiyo kama atatotokea mwanamke akachukua fomu za kuwania nafasi ya urais, basi ana nafasi jina lake kuingia katika tano bora.
Tayari baadhi ya wanawake wameanza kutajwa kwamba watawania nafasi hiyo wakiwamo Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka na Waziri wa Katiba, Sheria, Asha-Rose Migiro na Spika wa Bunge, Anne Makinda.
Kundi la Zanzibar
Kama itatokea kuna kada wa CCM kutoka Zanzibar akachukua fomu za kuwania nafasi hiyo, basi atakuwa anafasi kubwa ya kuingia jina lake katika tano bora.
Chama hata kama hakitaki safari hii mgombea wake atoke Zanzibar, lakini hakiwezi kumuacha ili kuonyesha kuwa hakina ubaguzi kwa misingi ya Ubara na Uzanzibari ikiwa ni hatua ya kuzuia mgawanyiko ndani ya chama.
Mpaka sasa habari zinasema kuwa Balozi Ali Karume huenda akachukua fomu kuwania nafasi hiyo.
Wasemavyo wadau
Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Hamad Salim alisema wananchi wasitarajie mabadiliko makubwa kutoka CCM, kwani wataendelea kuwaingiza wagombea wenye umri mkubwa na uzoefu katika tano bora.
“Tusitegemee kuona jina la kijana likiingia kwenye tano bora, mimi naona kama historia itajirudia tu,” alisema Salim.
Alisema CCM italazimika kumchagua mtu atakayekiuza chama na siyo anayekubalika na wanachama.
“Ni kweli kuna makundi ndani ya chama lakini mwishowe wataangalia nani anakiuza chama, hawawezi kuhangaika na hizi takwimu za tafiti,” aliongeza.
Salim alisema muda uliobaki kufikia siku ya uchaguzi ni mrefu, hivyo ni rahisi kwa wagombea kuanza kupakana matope na kubadilisha upepo wa kisiasa.
Mbunge wa Mchinga (CCM), Saidi Mohamed Mtanda, alisema wananchi watarajie kumwona mgombea mwanamke kwenye tano bora ya CCM, lakini wasitegemee kumpata rais mwanamke.
“Watu wanaweza wasinielewe lakini huu ndiyo mtazamo wangu, wakati wa kumpata rais mwanamke bado, watu hawajabadilika,” alisema Mtanda.
Alisema kwa kuwa mawazo ya wananchi yanabadilika kulingana na wakati, hivyo Watanzania watarajie kuona sura za watu wapya wakichomoza kuwania urais.
Hata hivyo, alisema kiongozi anayetaka kwenda Ikulu lazima atoke kwenye Baraza la Mawaziri tena awe asiye na ‘madoa madoa’ ya kashfa mbalimbali.
Mtanda alisema matokeo ya utafiti wa Twaweza yaliyotolewa hivi karibuni yamepotosha wananchi kwa kuonyesha kuwa vijana hawakubaliki na wananchi.
Naye Mbunge Ester Bulaya, (Viti Maalumu-CCM), alisema ingawa mchuano ndani ya chama tawala ni mkali, wanachama wanapaswa kumchagua kiongozi mwenye maadili.
Akitolea mfano alisema: “Kuna wanawake wengine wamejitokeza kuwania urais si waadilifu, mimi siwezi kumchagua mwanamke mwizi kama ambavyo siwezi kumchagua mwanaume mwizi, hivyo kuwa mwanamke siyo sifa pekee itakayomwezesha kupata kura.”
Bulaya aliwataja Spika wa Bunge la Muungano, Anne Makinda, Getrude Mongella na Asha-Rose Migiro kuwa ndiyo wanawake wasio na rekodi mbaya ya maadili.
Mbunge wa Sikonge (CCM), Said Juma Nkumba alisema vyovyote itakavyokuwa apatikane kiongozi atakayetatua matatizo ya wananchi.
“Mimi sitaki kutaja majina ya watu lakini tunahitaji mtu ambaye hata akipelekwa mbele za watu wamkubali kuwa ana maadili,” alisema Nkumba.
Hata hivyo, alitahadharisha kuwa kila anayesema kuwa kiongozi hana maadili atoe ushahidi kwa kuwa katika kipindi cha kuelekea kwenye uchaguzi kila mgombea anaweza kuambiwa hana maadili.
Imeandikwa na Julius Magodi na Goodluck Eliona.
Mwananchi

No comments: