Advertisements

Saturday, November 1, 2014

Waziri Nyalandu: Nitachukua uamuzi mgumu

Arusha. Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu amesema anaamini kuwa rais ajaye wa Tanzania, atakuwa ni kijana na kusema kwamba kila zama zina kitabu chake.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili hivi karibuni, waziri huyo alisema kuwa itakuwa ni kosa iwapo Rais Jakaya Kikwete atakabidhi kijiti kwa mtu mwenye umri unaofanana naye.
Nyalandu alibainisha kwamba wakati ukifika, atatangaza iwapo atagombea urais au kuendelea kugombea ubunge katika jimbo lake la Singida Kaskazini.
“Ukifika wakati ni lazima kubadilishana vijiti. Ni lazima kizazi kinachomaliza muda wake, kikabidhi kijiti kwa kizazi kinachofuata. Ni wazi mtu mwenye umri unaofanana na kiongozi anayeondoka madarakani hana nafasi,” alisema Nyalandu akiongeza:
“Kijiti hiki anachokiacha Jakaya Kikwete, aliachiwa na kaka yake Rais Benjamin Mkapa na Mkapa naye aliachiwa kijiti na kaka yake Mzee Ali Hassan Mwinyi ambaye ndiye alisema kila zama na kitabu chake.”
Alieleza kuwa huo ni uhalisia wa maisha na kwamba ni lazima kila mtu kukubali hivyo.
“Sasa tunahangaika kuandika hitimisho la zama za Rais Kikwete, ndiyo sisi tunapambana kuhakikisha tunakomesha ujangili na wengine wanafanya kazi nyingine. Haya yakikamilika ni zama zake (Rais Kikwete), zimekamilika,” alisema Nyalandu.
Alifafanua: “Rais Kikwete atakabidhi kitabu kwa zama nyingine na sharti akabidhi kijiti kwa kizazi kinachofuata. Haitawezekana ikiwa atakabidhi kijiti kwa kizazi chake hichohicho. Ni kosa kurudia zama zilizopita.”
Nyalandu alisema kuwa ni vyema mtu yeyote mwenye umri unaofanana na kiongozi anayeondoka madarakani akasahau kupewa kijiti kwani historia na hata maandiko ya Mungu vipo tofauti.
Makundi ya urais
Akizungumzia taarifa za kutakiwa na makundi ya waliojitangaza kugombea urais ili awaunge mkono na yeye asubiri  kupewa uwaziri mkuu, Nyalandu alisema taarifa hizo siyo sahihi.
“Hakuna kiongozi anayechaguliwa na mtu mmoja. Sisi sote ni viongozi na hakika hakuna anayependa tuwe viongozi, bali ni Mwenyezi Mungu tu. Kwa mfano, mimi najiona mwenye bahati tu, kwani kabla ya kuwa waziri, nilikuwa Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara na kulitokea matatizo, wenzangu waliondoka. Baadaye, nilikuwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, pia wenzangu kama saba waliondoka na nikapanda hadi nilipo sasa. Haya ni mapenzi ya Mungu…”
Hata hivyo, Nyalandu ambaye amekuwa akitajwa kuwa na nia ya kugombea urais alisema bado wakati mwafaka haujafika kutangaza nia yake.
“Mimi kama kiongozi wa kitaifa, kama waziri na mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, naweza kukuhakikishia kama nitagombea lakini hili ni jambo linalokwenda na wakati. Wakati ukifika nitafanya uamuzi mgumu kuwa nitagombea au la. Kugombea ni uamuzi mgumu na kutogombea ni uamuzi mgumu pia,” alisema.
Alisema kwamba mtu anayetangaza kugombea urais au anayekaa kimya, ajue kuwa Watanzania huwapima watu kwa matendo yao wanayofanya.
“Kupimwa tunapimwa, mtu ambaye hajatangaza nia siyo kama hapimwi, watu wanatupima tu. Tunaishi vipi na watu, je, familia yako ipo vipi, je jimboni wanakuonaje, umesaidia maisha ya watu au unapandisha mabega baada ya uwaziri au unashirikiana na wananchi vizuri?  Kiongozi anapimwa na vitu vingi,” alisema na kuongeza:
“Mwanasiasa akiwa ametangaza nia au hajatangaza ajue yupo katika vipimo. Kinachopimwa siyo maneno ni kazi tunazofanya. Kama kiongozi, sote tutapimwa hata kama ulitangaza nia tangu mwaka 2010.”
Rais ajaye atatoka CCM lakini…
Kuhusu nafasi ya CCM kutoa rais ajaye, Waziri Nyalandu alisema: Kama taa ikikuangazia na Watanzania wakasema sisi tunakutaka wewe kupitia chama chao, basi utakuwa kiongozi wao.”
Nyalandu alisema kuwa anaamini rais ajaye atatoka CCM, lakini akatahadharisha kwamba lazima chama hicho kihakikishe kinatimiza wajibu wake kwa kumpitisha mgombea wake kikizingatia misingi ya uwazi na ushirikishwaji.
“CCM inapaswa kuhakikisha rais ajaye atatokana na mapenzi ya wanachama walio wengi ili iwe rahisi kumnadi,” alisema.
Alifafanua kuwa ni muhimu ijulikane kwamba hakuna mtu yeyote aliye na hatimiliki ya siasa za Tanzania na hakuna mtu ambaye familia yake ina hakimiliki ndani ya CCM.
“Ijulikane, Mtanzania yeyote ana haki ya kuchukua fomu na kugombea kama lengo lake ni kuwasaidia Watanzania. Mtu ambaye ana nia ya kuendeleza kazi anayomalizia Rais Kikwete. Lazima apokee mtu ambaye atajenga kwenda juu na siyo kubomoa,”alisema.
Kuhusu tuhuma juu yake
Akizungumzia tuhuma zinazoelekezwa kwake, Nyalandu alisema ni za kupangwa na za uongo, huku akitolea mfano wa tuhuma za kudaiwa kutaka kuuza Hifadhi ya Katavi na kuruhusu wanyama 700 kuwindwa bure.
“Huu ni uongo, hivi kama ni waziri anataka kuuza Hifadhi ya Taifa, kweli angemaliza hata saa mbili bila ya kufukuzwa na rais?” anahoji Nyalandu .
Alisema tuhuma nyingi dhidi yake zinatokana na msimamo wake katika vita dhidi ya ujangili nchini na kwamba kuna watu ndani ya Serikali na idara mbalimbali walikuwa wakihusika na matukio ya ujangili na sasa wanajitahidi kumchafua.
“Na hapa ieleweke kuwa tunawafahamu watu wote waliopo katika mtandao huu, ujumbe wanaotumiana na simu wanazopigiana, wakati ukifika tutawakamata mmoja baada ya mwingine, kwani tayari maofisa wengi wizarani tumewaondoa na wengine kuwabadilisha idara,” anasema.
Mgogoro kati yake na Katibu Mkuu
Kwa muda mrefu, Waziri Nyalandu, anatajwa kuwa na uhusiano mbaya na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii.
Hata hivyo, Nyalandu alisema kuwa taarifa nyingi zinazoelezwa siyo sahihi na kwamba yeye ni kiongozi wa wizara na kila mtu ana wajibu wake.
“Mengi yanasemwa sisi hatuelewani, lakini ukweli ni kuwa kila mtu anafanya kazi kwa kuzingatia taratibu na sheria na hatuna msuguano wowote,” alisema.
Akizungumzia uamuzi wa kuhamishwa watendaji kadhaa katika wizara hiyo, Nyalandu alisema suala hilo halimaanishi kuna mgogoro, kwani waliohamishwa wapo ambao tayari wameripoti vituo vyao vya kazi.
“Kama nilivyosema awali kuna mambo mengi yanaendelea pale wizarani na kuna watu wanatoa taarifa potofu kwenye vyombo vya habari, kwa kuchomoa madokezo tu ya mambo na kufanya yametendeka, lakini tutahakikisha tunakomesha mambo haya,” alisema.
Safari za nje na kufanya kazi nje ya ofisi
Akizungumzia tuhuma za kufanya safari nyingi za nje ya nchi na kuhamisha ofisi yake kutoka wizarani na kuipeleka hotelini, Nyalandu alisema tuhuma hizo hazina ukweli.
“Mimi ni Waziri wa Maliasili na Utalii, ofisi yake ni mapori yote ya akiba yenye ukubwa wa kilomita za mraba 200,000. Ofisi yangu ni kutafuta watalii na kufikia Machi mwakani utalii ndiyo unatarajiwa kuongoza katika kuchangia pato la taifa, sasa unaposema sikai ofisini sijui ofisi ipi?” anahoji.
Hata hivyo, alisema kuwa uamuzi wa kuanzisha Mamlaka ya Wanyamapori, aliutangaza akiwa wizarani na hilo ni kati ya mambo makubwa aliyofanya ili kunusuru rasilimali za taifa kuendelea kupotea.
“Katika mpango huu wafanyakazi wengi ajira zao zitakoma na watakuwa chini ya mamlaka yenye bodi yake ambayo inaongozwa na wananchi na hapo tutaweza kuratibu vyema mapori ya akiba na maeneo mengine ya hifadhi za wanyama,” alisema.
Ujangili umenisababishia vita
Kuhusu ujangili, Waziri Nyalandu alisema mapambano dhidi ya ujangili nchini yamemsababishia vita kubwa.
Alisema wizara hiyo ina rasilimali nyingi na kwamba kuna watu walizoea njia za mikato.
Matatizo ya wanyamapori yaani tembo na faru kuuawa yanatokana na uchu wa watu wachache na hasa wenye mamlaka ambao walitumia nafasi zao kwa namna moja ama nyingine.
Anafafanua kuwa watu hao walifanya vitendo hivyo kwa kutofanya kazi ipasavyo ama kufumbia macho vitendo hivyo ama kushirikiana na majangili.
“Vitendo hivi vilifanya ujangili kufikia mahali ambapo haiwezekani tena kudhibitiwa. Hadi kufikia mwaka 2013  tembo walikuwa wanakwisha kabisa kutokana na ujangili,” alisema,
 “Ukipita katika kila pori unakutana na mizoga ya tembo ambayo meno yao yamechukuliwa.  Kwa mujibu wa taarifa za Shirika la Umoja wa Mataifa la  Cites tembo wapatao 10,000 walikuwa wanauawa kwa mwaka. Idadi hii ilifikia mahali ambapo imekuwa ni janga kuu la kitaifa,” alisema na kuongeza:
“Nilipoteuliwa kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii mwezi Februari mwaka huu, moja ya maagizo ambayo Rais alinipa ni kuhakikisha kuwa hali hiyo tunaisimamisha mara moja.”
Alisema walianzisha Operesheni Tokomeza kwa ajili ya kukomesha matatizo hayo lakini kwa bahati mbaya operesheni hiyo haikwenda vizuri kutokana na shutuma mbalimbali za uvunjifu wa haki za binadamu.
“Kama mnakumbuka Rais pia aliunda tume kuchunguza nani alihusika, nani alifanya nini, ili kuhakikisha kuwa tunaposimamia haki, ni muhimu kuonekana inatendeka. Kwa kuwa hatuwezi kusimamia sheria za nchi tukavunja haki za msingi za wananchi,” alisema.
Hatua zilizochukuliwa
Nyalandu alisema majangili yalitawala kutokana na askari wanyamapori kutokuwa na fedha, silaha na pia kutokana na kuwa wachache.
Alisema maaskari wanyamapori walikuwa na magobori wakati majangili walikuwa na silaha kali.
“Lakini kulikuwa na silaha aina ya AK-47 zipatazo 500, kulikuwa na ubishi kati ya wizara na Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) na kwa muda wa miaka miwili ambayo silaha zilikuwa bandarini, majangili yalikuwa yakitandika wanyama porini kila asubuhi na usiku,”alisema.
“Katika saa 24 tu tangu nilipoteuliwa niliamua kutoa Sh250 milioni kulipia hizo silaha na zikaingia katika mapori,” alisema.
Alisema hadi kufikia Julai mwaka huu alikuwa ameajiri wafanyakazi wengine wa wanyamapori 430 ambao wengi wamepelekwa katika maeneo ya Selous.
Pia alisema wameongeza idadi ya vijana wanaojitolea ambao wamemaliza mafunzo lakini hawajapata ajira.
“Na hawa tumewapeleka kwa mamia katika mapori tumewapa silaha na magari,” alisema.
Nyalandu alisema lazima ijulikane kuwa kiini cha ujangili kipo katika namna gani unawapa motisha wafanyakazi.
“Fedha zile zilikuwa hadi zifike kwa katibu mkuu, waziri, ndiyo ziende kunakohusika, nikasema ninataka fedha ziidhinishwe moja kwa moja na wakuu wa idara kwa hiyo nikakata ukiritimba na urasimu. Vijana hawa wakaanza kupata fedha hata kama wanapata kidogo lakini wanapata kwa wakati.”
Alisema hatua hizo ziliongeza morali kwa wafanyakazi.
Meno ya tembo yalindwa na UN
“Nilijiuliza kwa nini meno ya tembo ambayo tuliyakamata yalikuwa ni ya zamani? Kwa nini siyo mapya? Ukiambiwa tani za meno ya tembo zimekamatwa Zanzibar, Dar es Salaam zote zilikuwa ni za zamani.”
Aligundua kuwa kuna mchezo ulikuwa ukichezwa ndani ya ghala la meno ya tembo.
“Na hiyo ilikuwa inachangia ujangili kwa sababu watafanya watu wao waende wakafanye ujangili wa meno ya tembo ili walijalizie (ghala). Niliagiza kuwa kuanzia sasa meno ya tembo tutayalinda kwa pamoja nikawaita Umoja wa Mataifa, serikali za Uingereza na Tanzania ili tujadili kwa pamoja jinsi tutakavyoyalinda,”alisema.
Aliagiza kuwa kila jino la tembo lifanyiwe DNA ili ijulikane linatokana na tembo wa mwaka gani, alikufa wapi.
Alisema hatua hizo zimemletea upinzani mkubwa.
Hata hivyo, alisema baada ya kubadilisha watu waliokuwa wakilinda ghala na kulinda kwa ushirikiano, meno ya tembo yameongezeka kutoka tani 100,000 hadi 130,0000.
“Ni hatua ambayo imeniletea vita vikubwa sana lakini ni hatua ambayo imeponya tembo wengi sana. Ni hatua ambayo imewabania ulaji watu wengi sana. Lakini ukiwa kama Waziri wa Maliasili na Utalii, inakupunguzia sana marafiki,” alisema Nyalandu.
Idadi ya vibali yapunguzwa
Alisema ukichukua DVD ambayo iliwasilishwa na Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (Chadema) ilikuwa ikionyesha idadi kubwa ya wanyama wakiuawa.
“Niliwaondelea vibali na hatua hii ilisaidia sana kuleta woga kwa makampuni ya uwindaji,”alisema.
Alisema pia waliwafundisha kanuni za uwindaji ili wawe wawindaji mahiri.
Alisema pia wamepunguza vibali vya uwindaji kwa mwaka kutoka 200 hadi 100.
“Nimepiga marufuku uwindaji wa tembo vijana na watoto sasa ni tembo wazee tu wanaweza kuwindwa,” alisema.
Akizungumzia hali ya ujangili nchini, Waziri Nyalandu alisema wizara yake kwa kushirikiana na vyombo vingine vya serikali na wananchi wema, wanaendelea kudhibiti ujangili, kwani idadi ya tembo inaongezeka na watuhumiwa wanakamatwa.
Pia alisema hivi sasa wananchi wamekuwa wakishirikiana na serikali kutoa taarifa za ujangili na wizara imeongeza motisha kwa askari wa wanyamapori.
Aidha Waziri Nyalandu aliwasifu wanahabari kuwa wamefanyakazi kubwa  kuzungumzia ujangili na sasa jambo hili linapigwa vita kila kona,” anasema.
Alisema katika kuhakikisha ulinzi unaimarishwa, askari zaidi ya 400 wamepewa kazi ya ulinzi wa wanyamapori katika mapori mbalimbali na wengine bado wanaendelea na mafunzo.
Tume ya oporesheni tokomeza
Akizungumzia Tume ya Rais ya kuchunguza athari za Operesheni Tokomeza, Nyalandu alisema inaendelea na kazi na wote ambao watatajwa na tume hiyo bila kujali nafasi zao watashughulikiwa kwa mujibu wa kanuni na taratibu.
“Tutahakikisha haturudii makosa yaliyofanyika katika operesheni iliyofanyika na tumekubaliana kufuata kanuni na taratibu katika utendaji wetu,” alisema.
Kuna watendaji serikalini wanahusika na ujangili
Akizungumzia tuhuma za baadhi ya watendaji ndani ya serikali na vyama vya siasa kuhusika na ujangili, alisema tuhuma hizo zinafanyiwa kazi na baadhi wamechukuliwa hatua.
Waziri Nyalandu alisema ni kweli kuwa sehemu kubwa ya meno ya tembo yaliyokuwa yanakamatwa nje yalikuwa ni ya muda mrefu, hivyo kulikuwa na uwezekano wa kuibiwa kutoka katika ghala maalum la kuhifadhi memo hayo.
“Tanzania inaongoza kwa kuwa na meno ya tembo mengi katika ghala la taifa na sasa yapo tani 130,000 ambapo thamani yake ni zaidi ya dola milioni 60,” alisema.
Kadhalika Waziri Nyalandu alisema: “Kuna watu walinipinga ndani ya serikali, lakini sasa tumekubaliana kuwa askari wetu watashirikiana na vyombo vingine kulinda meno haya ili kuhakikisha yanakuwa salama na dunia inajua yapo salama,” anasema.
Mamlaka ya wanyamapori suluhu ya ujangili
Waziri Nyalandu alisema kuanzisha mamlaka ya wanyamapori anaamini ndiyo suluhu ya vitendo vya ujangili kwani, chombo hicho kitakuwa na uwezo mkubwa wa kulinda wanyamapori hapa nchini.
“Tutahamisha wafanyakazi wengi kwenda katika mamlaka hii, ambayo makao makuu yatakuwa Morogoro na tutaongeza usimamizi wa mapori ya akiba, askari wengi wataajiriwa wakiwa na silaha za kisasa,” alisema.
Alisema mamlaka hiyo, pia inaungwa mkono na wahisani mbalimbali, ambao wamekubali kuisaidia serikali ya Tanzania katika vita dhidi ya ujangili.
“Tutakuwa na helikopta za kutosha, ndege na vifaa vingine pia kuna fedha nyingi tumepata katika kuiwezesha mamlaka hii kukabiliana na ujangili.”
Nimejifunza mengi kwa walionitangulia
Waziri Nyalandu, ambaye ameshika wizara hiyo, ambayo imekuwa kaa la moto kwa mawaziri wengi waliomtangulia kutokana na kuondolewa alisema kuwa, kuna mambo mengi mazuri yaliyofanywa na mawaziri waliomtangulia.
“Serikalini tunafanyakazi kwa pamoja, hivyo maamuzi ya mawaziri waliotangulia huwezi kupingana nayo yote.”
Hata hivyo, alisema kuna changamoto  zilizosababisha wao kuondolewa katika wizara naye amekuwa akikabiliana nazo na Mungu anamsaidia anaendelea kuzishinda.
Kuhusu Jimbo lake
Waziri huyo alisema jimbo lake kwa sasa ndiyo wazalishaji wakubwa wa chakula katika Mkoa wa Singida kutokana na kuzalisha chakula kingi cha ziada na mazao mengi ya biashara ikiwamo vitunguu vinavyouzwa ndani na nje ya nchi.
Waziri Nyalandu amekuwa mbunge wa jimbo la Singida Kaskazini kwa miaka 14 sasa.
Mwananchi

No comments: