ANGALIA LIVE NEWS

Friday, December 26, 2014

ANAKUPENDA, UNAMPENDA, KWA NINI MAPENZI YENU YAWE YA SIRI?- 2

Ni matumaini yangu kwamba kwa kudra za Mwenyezi Mungu, msomaji wangu umesherehekea vyema sikukuu ya Krismasi na leo unamalizia na Boxing Day, tuzidi kumuomba Mungu atuvushe salama kuingia mwaka mpya wa 2015.

Karibu tena kwenye uwanja wetu huu mzuri, Lets Talk About Love! Tuzungumzie mapenzi na kubadilisha mawazo kuhusu mambo mbalimbali yahusuyo maisha yetu ya kila siku.

Wiki iliyopita tulianza kuijadili mada yetu kama inavyojieleza hapo juu. Nilikufafanulia maana ya mapenzi ya siri na tukaanza kuangalia sababu zinazofanya baadhi ya watu wapende uhusiano wa siri.
Tuliangalia kwamba wengi wanaopenda mapenzi ya siri, yawezekana wakawa wameoa/kuolewa lakini hawataki wenzi wao wapya wajue ukweli wa maisha yao. Sababu nyingine tuliona kwamba yawezekana mpenzi wa namna hiyo anao wengi na kila mmoja anamhakikishia kwamba yupo peke yake.

Nimepokea meseji nyingi kutoka kwa wasomaji wangu, wengi wakilalamika kwamba nao walipitia au wapo kwenye mapenzi ya siri na wanachovuna kila siku ni maumivu. Leo tuendelee kuangalia sababu nyingine zinazowafanya baadhi ya watu wapende kuwa kwenye uhusiano wa siri.

3. BADO HAJAKUKUBALI MOYONI MWAKE
Ukweli mwingine ambao unaumiza ni kwamba kama una mpenzi na hataki mtu yeyote ajue kuhusu uhusiano wenu, huenda hajakukubali ndani ya moyo wake kwamba una sifa na vigezo anavyovitaka hivyo anaona aibu kwamba marafiki zake au wafanyakazi wenzake wakijua, watamdharau.

Huenda mkiwa peke yenu wawili anakupamba kwa kila aina ya sifa lakini ndani ya moyo wake, anakutumia kama daraja ili siku akimpata mwenye sifa anazozitaka, kama uzuri wa sura, umbo, fedha au kazi nzuri, akuache kwenye mataa. Kuwa makini na mtu wa aina hii na ni bora ukachukua hatua mapema kwani huenda akakuumiza sana baadaye.

4. HAJIAMINI
Sababu nyingine inayosababisha mtu akapenda kuwa na uhusiano wa siri, ni matatizo ya kisaikolojia ambayo yamesababisha akakosa kujiamini ndani ya moyo wake.

Huenda kabla yako, aliwahi kuwa na mpenzi ambaye alimpenda sana na kumtambulisha kwa kila mtu, matokeo yake akaja kumuumiza na kumuacha katika wakati mgumu.Mtu wa namna hii, anakuwa mgumu kukutambulisha kwa watu wake wa karibu kwa kuhofia kwamba huenda kesho na keshokutwa na wewe ukamkimbia na kumfanya aonekane hajatulia mbele ya jamii.

Anaogopa kuonekana anabadilisha wapenzi kila kukicha, hajiamini tena, hataki kujifunga kwa mpenzi mpya na njia pekee anayoona inafaa, ni kuwa na uhusiano wa siri ili hata siku mkiachana, asiwepo wa kumuuliza.

Ni vizuri kumsaidia mwenzi wako mwenye tatizo hili ili aanze kujiamini upya na kukubaliana na hali iliyotokea mwanzo. Taratibu ataanza kuona umuhimu wa kukutambulisha na kuliweka wazi penzi lenu.

5. ANAKUHISI MABAYA
Sababu nyingine inayoweza kumfanya mtu akapenda kuwa na uhusiano wa siri, huenda anakuhisi mabaya na hataki mtu yeyote ajue kwamba yupo na wewe.

Upo ushahidi wa watu ambao walitokea kuwapenda watu fulani maishani mwao lakini wakakatishwa tamaa na marafiki zao wa karibu kwa kauli kama: ‘Yule hajatulia kabisa, ana wanawake mtaa mzima,’ au ‘yule dada kicheche sana, hakuna mwanaume ambaye hamjui.’

Kwa mtu ambaye anakupenda kwa dhati kutoka ndani ya moyo wake, ataumia sana kusikia watu wakikusema vibaya lakini kamwe hatakubali kusikiliza maneno ya watu, atahakikisha anakupata lakini ili kukwepa manenomaneno, atataka uhusiano wenu uwe wa siri mpaka atakapojiridhisha mwenyewe kwamba yaliyokuwa yanasemwa ni kweli au si kweli.

HITIMISHO
Mtu anayekupenda kwa dhati, hataona ugumu wowote kukutambulisha ili watu wote wakujue. Hata hivyo, si kila mtu anayetaka mapenzi ya siri anakuwa na nia mbaya na wewe.
Wapo wengine ambao wanakuwa na mapenzi ya kweli lakini kuna sababu kadhaa zinazofanya wapende mapenzi ya siri. Cha msingi ni kukaa na mpenzi wako na kuzungumza naye au kumchunguza kwa karibu ili ujue sababu zinazomfanya apende mapenzi ya siri.

Kama ana tatizo kwa mfano hajiamini, alishaumizwa sana, anakuhisi mabaya na mengine kama hayo, msaidie kuondokana na tatizo alilonalo na taratibu ataanza kuona umuhimu wa kuliweka wazi penzi lenu.

Lakini kama ana jambo baya analificha, kwa mfano ameoa/ameolewa, ana wapenzi wengi au hakupendi ila anakutumia tu, huyo hakufai kwani ipo siku atauvunja sana moyo wako. Zungumza na moyo wako kisha chukua hatua mapema.

GPL

2 comments:

Anonymous said...

Ni kweli kwani umfiche mbele za watu ukiona watu unajifanya .una mpango naye ,mwanaume wa hivyo ,maana yake anwanawake wengi,hawataki watu wajue ,tabia mbaya sanaaaaa.

Anonymous said...

mwanamme michepuko asiyechepuka ni kuku gonjwa kuku goi goi si kijongoo kuku la kizungu.kuku jongo la Kiswahili linachepuka na vingi vya mitaani,mezani,kichochoroni,jalalani na anajua utamu wake,tena BAD BOYS MTAMU SANA KULIKO GOOD BOY.

chunguzeni mtaona wenyewe.michapuko forever nakinogeo cha mapenzi.