ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, December 16, 2014

BAN KI MOON ATAKA USHIRIKIANO ZAIDI BAINA YA UN NA AU

Katibu Mkuu Umoja wa Mataiifa Ban Ki Moon

Na  Mwandishi Maalum, New York
Katibu Mkuu wa Umoja wa  Mataifa  Ban Ki Moon,  amesema, ushirikiano  kati ya Umoja wa Mataifa na  Umoja wa Afrika katika operesheni za ulinzi wa Amani  umekuwa  wa  mafanikio makubwa katika urejeshwaji wa hali ya amani na utulivu katika maeneo yenye  migogoro.
Hata hivyo  amesema pamoja na mafanikio hayo kuna  umuhimu wa ushirikiano huo kuboreshwa zaidi na kuwa wenye tija .
Alikuwa akizungumza  wakati wa majadiliano ya wazi ya siku  moja juu ya ajenda ya Operesheni za  Ulinzi wa Amani,  mkazo mkubwa ukielekezwa zaidi katika ushirikiano baina ya Umoja wa Mataifa na  Umoja wa  Afrika.
 Majadiliano hayo  ambayo  pamoja  na  kuhudhuriwa na  Katibu Mkuu Ban Ki Moon, pia  mshiriki mwingine alikuwa  Rais Mstaafu wa Burundi, Pierre Buyoya ambaye ni  Mjumbe Maalum wa AU huko  Mali na Ukanda wa Sahel. Yameandaliwa na  Baraza  Kuu la  Usalama la Umoja wa  Mataifa ambalo kwa mwezi huu wa Desemba lipo chini ya Urais wa Jamhuri ya Chad.

Ban Ki Moon ameeleza kuwa  kwa miaka mingi ushirikiano kati ya UM  na washirika wake wa Kikanda  umezidi kuimarika na kwamba Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa na  Baraza  la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika yamekuwa yakifanya kazi kwa karibu zaidi.
Amesisitiza kuwa ni kutokana na ushirikiano huo,  kumekuwapo na uongezeko  la uungwaji mkono wa  operesheni za kulinda Amani ambazo zimekuwa zikifanyika chini ya  Umoja wa  Afrika.
Akizungumzia zaidi kuhusu ushirikiano huo na mafanikio yake, Ban Ki Moon amebainisha  kwamba,  katika   Kanda ya Maziwa  Makuu, ushirikiano   baina ya  Umoja wa Mataifa,  Umoja wa Afrika,  Mkutano wa Kimataifa wa  Nchi za Maziwa Makuu na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini  mwa Afrika   umesaidia sana  katika  kurejesha hali  ya utulivu katika DRC na eneo  la Maziwa Makuu.
Akaeleza pia kuwa   huko Somali taasisi hizo mbili kwa maana ya UM na AU pamoja   na  wadau wengine wanafanya kazi kwa karibu katika kuisaidia serikali ya shirikino ya nchi hiyo katika hatua  muhimu ya ujenzi wa Amani na ujenzi wa taifa la Somalia.
“ pia tunafanya kazi kwa  karibu na AU na Taasisi zingine za Kikanda huko  Sudan na Sudani ya Kusini katika suala zima la kutafuta Amani na usalama wa kudumu katika maeneo hayo”. Amesema   Katibu Mkuu
Na kusisitiza kuwa pamoja na   kuwapo kwa mafanikio  bado  kuna umuhimu  kwa kuongeza juhudi zaidi katika eneo hilo la ushirikiano na hasa kutokana na ukweli kuwa walinzi wa Amani wanaohudumu katika Taasisi hizo wanakabiliwa na changamoto nyingi na hatari kubwa zaidi.
Ban Ki  Moon, ameleza kuwa walinzi hao  wa Amani wanafanya kazi katika mazingira magumu  na hatarishi huku wakilazimika kukabiliana na makundi ya waasi wenye silaha, makundi ya  kigaidi na makundi ya uhalifu wa kupangwa.
Na kwa sababu hiyo anasema  ili kuboresha ushirikiano  uliopo baina ya  UM na AU panahitajika mbinu na fikra  mpya na mbadala  zitakazokwenda sambamba na  mabaliliko  yanyojitokeza hivi sasa katika eneo hilo la operesheni za ulinzi wa Amani.
Aidha anasema panahitajika  si tu ushirikiano wa kisiasa bali pia uwepo wa uwazi, uwajibikaji na vile vile kujua nani anafanya nini wapi na kwa wakati gani na majukumu ya kila Taasisi.
Akasisitiza kuwa   Jumuiya ya Kimataifa inatambua vema kuwa migogoro inayoikuba   si matatizo ya  Afrika peke yake bali  inahusu Jumuiya  yote ya Kimataifa na kwamba  utatuzi wake  unahitaji ushirikiano wa pamona na kufanya kama kama kitu kimoja.
Akizungumzia      kuhusu Afrika kuwa na  vyanzo vyake vya mapato vitakavyogharamia shughuli za ulinzi, Ban Ki Moon amesema inagaya naye amekuwa muumini wa  dhana hiyo lakini bado anaamini kuwa mchango wa Jumuiya ya Kimataifa unahitajika pia.

Akaushukuru Umoja wa Afrika  kwa namna ambavyo imekuwa ikishughulikia migogoro mbalimbali inayojitokeza katika Afrika pamoja na ushirikiano wake na Umoja wa Mataifa

No comments: