ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, December 10, 2014

CAG AHUDHURIA KIKAO CHA BODI YA WAKAGUZI WA UMOJA WA MATAIFA

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali mwenye tai nyekundu akimsikiliza kwa makini Mwenyekiti wa Bodi ambaye pia ni Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu kutoka Uingereza aliyekuwa akimkaribisha kwenye Bodi hiyo, upande wa kulia ni Ujumbe wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu kutoka India. Uingereza, India na Tanzania ndiyo inayounda Bodi ya Wakaguzi wa Hesabu za Umoja wa Mataifa na Mashirika yake. Katika mkutano huo ilielezwa kuwa Tanzania kwa maana ya CAG itachukua uenyekiti wa Bodi ifikapo Januari Mosi mwakani, uenyekiti huo ni wa miaka miwili.
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Profesa Mussa Juma Assad na ambaye kwa wadhifa wake ni Mkaguzi wa Hesabu za Umoja wa Mataifa akiwa na baadhi wa wasaidizi wake katika Kikao cha Bodi ya Wakaguzi wa Umoja wa Mataifa kilichofanyika jana ( Jumanne) Hapa Umoja wa Mataifa.
Pamoja na Kushiriki Vikao vya Bodi, CAG alipata nafasi ya kufika katika Uwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa ambako alipokelewa na Mwenyeji wake, Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa Balozi Ramadhani Mwinyi. Akiwa katika Uwakilishi wa Kudumu CAG alijionea maendeleo ya ukarabati wa Jengo la Uwakilishi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa

Na Mwandishi Maalum, New York

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za  Serikali, Profesa Mussa Juma Assad  ameelezea kuridhishwa kwake na mwenendo wa vikao vya Bodi ya Wakaguzi ya Umoja wa Mataifa ( UNBoA) na kuahidi kushirikiana na  kufanya kazi kwa karibu na wajumbe wenzie wanaounda bodi hiyo.
Ameyasema hayo  siku ya jumanne  wakati wa  wajumbe wa Bodi hiyo walipokutana  hapa Umoja wa Mataifa. Hii ni  mara ya kwanza kwa CAG kuhudhuria vikao vya Bodi hiyo  ambayo  wajumbe  wake ni  wadhibiti na wakaguzi   wakuu wa hesabu za serikali kutoka Uingereza,  Tanzania na India
 Profesa Mussa Juma Assad  ambaye ameteuliwa  hivi Karibu  na Mhe. Rais Jakaya Mrisho Kikwete kuwa  Mdhibiti na  Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali akichukua nafasi ya Bw. Ludovick  Utouh ambaye amestaafu kwa  mujibu wa sharia, amewaeleza wajumbe wenzie kuwa amejifunza mengi.
Katika kikao chao cha siku  moja  kilichotanguliwa na  kikao cha jopo la wakaguzi wa nje kilichojadilia taarifa mbalimbali za  mashirika ya Umoja wa Mataifa   ikiwamo  taarifa ya  Shirika la  Kimataifa la Nguvu za Atomic, wajumbe wa  Bodi walijadiliana pamoja na mambo mengine  changamoto  zinazowakabili katika utekelezaji wa majukumu yao kama wakaguzi wa hesabu za  Umoja wa Mataifa.

Awali wakizugumza kwa nyakati tofauti, Mdhibiti na Mkaguzi  Mkuu kutoka Uingereza Bw.Amyas Morse na  Bw. Shashi  Sharma Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu  kutoka India  pamoja na kumkaribisha Profesa Assadi katika Bodi hiyo pia walimuahidi ushirikiano  katika  utekelezaji wa majukumu  waliyokabidhiwa.
Aidha katika  kikao hicho cha  Bodi  ilitolewa taarifa kuwa   Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu  kutoka Tanzania ( CAG)  atashika uenyekiti wa Bodi kuanzia Januari  Mosi mwakani. Nafasi hiyo ya   uenyekiti huwa ni ya mzunguko wa kipindi  cha miaka miwili ambapo  hivi sasa  inashikiliwa  na Mdhibiti na Mkaguzi  Mkuu  kutoka  Uingereza.
Aidha   Mkurugenzi wa  Ukaguzi wa Nje, Bw. Fransis Kitauli ambaye ndiye anayemwakilisha CAG katika  utekelezaji wa mukumu ya kila siku  ndani ya Bodi hiyo naye atakuwa mwenyekiti wa   Kamati ya Operesheni za Ukaguzi ( AOC)
Bodi ya Ukaguzi wa Umoja wa Mataifa, ni chombo   huru na kinachojitegemea chenye jukumu la kukagua vitabu vya hesabu za Makao Makuu ya  Umoja wa Mataifa,  Mashirika na Taasisi zote zilizochini ya Umoja wa Mataifa,  Misheni za Ulinzi wa Amani za Umoja wa Mataifa na  Miradi mbalimbali inayosimamiwa na Umoja  wa Mataifa.
Tanzania kupitia Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ilichaguliwa kuwa Mkaguzi wa Hesabu za  Umoja wa Mataifa mwaka  2012 ikichukua nafasi ya Afrika ya Kusini. Aidha Tanzania ambayo itadumu katika Bodi ya Wakaguzi ya Umoja wa Mataifa kwa Miaka sita inakuwa nchi ya Tatu ya Afrika kushika wadhifa huo  nyeti ikitanguliwa na Ghana na Afrika ya Kusini.

No comments: