Advertisements

Monday, December 22, 2014

Chadema waibua mapya kashfa ya Escrow

Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Chadema, Arcado Ntagazwa.

Wakati Rais Jakaya Kikwete akitarajia kutoa maamuzi ya maazimio yaliyotolewa na Bunge kuhusiana na sakata la uchotwaji wa zaidi ya Sh. bilioni 300 katika akaunti Tegeta Escrow, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeibua mapya kwa kutaja orodha mpya ya viongozi wanaopaswa kuwajibishwa kutokana na kashfa hiyo.

Aidha, Chadema kimesema Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdrahaman Kinana, anafahamu jinsi uchotwaji fedha hizo kwa kuwa alikuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya Stanbic.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Chadema, Arcado Ntagazwa, akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, alisema wapo viongozi ambao hawakutajwa kuchukuliwa hatua kwenye taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) wakati wizara zao zilihusika katika mchakato wa utoaji fedha kwa namna moja au nyingine.


Alisema wanaopaswa kuingizwa katika kundi viongozi wanaopaswa kuwajibishwa ni Waziri wa Fedha, Saada Mkuya, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dk. Silviaciua Likwelile, Gavana wa Benki Kuu (BoT) Prof. Benno Ndulu (pichani) na Mkurugenzi wa Shirika la Ugavi Umeme (Tanesco), Felichismi Mramba.

“Watanzania wanasubiri kusikia Rais Kikwete anachukua hatua dhidi ya Waziri wa Fedha, Saada Mkuya ambaye wakati fedha katika akaunti ya Escrow zinatolewa kati ya Septemba na Desemba mwaka jana alikuwa ndiye Kaimu Waziri wa Fedha,” alisema.

Waziri wa Fedha, Mkuya, Katibu Mkuu,Likwelile na Mkurugenzi wa Tanesco, Mramba walipotafutwa simu zao zilikuwa zikiita bila kupokelewa na hata walipotumiwa ujumbe mfupi wa maneno hawakujibu.

Kwa upande wa Katibu Mkuu CCM, Kinana na Ndulu walipotafutwa simu zao zilikuwa hazipatikana kutwa nzima.

Ntagazwa alisema suala la miamala iliyofanyika kupitia Benki ya Stanbic katika sehemu ya kashfa hiyo ya akaunti ya Escrow siyo suala la kufanyia mzaha katika ufisadi huu.

Alisema kupitia benki hiyo kiwango kikubwa cha fedha zaidi ya Sh. bilioni 160 zilichukuliwa kwa magunia na hakuna benki ndani ya nchi inayoweza kufanya miamala ya mabilioni ya fedha bila BoT kuidhinisha.

“Gavana Prof. Ndulu hawezi kukwepa uwajibikaji kwenye jambo hili zito kwa kuwa alilifahamu na kulilidhia,tunataka Rais Kikwete atueleze umma wa Watanzania hatua zilizochukuliwa dhidi ya watumishi hawa na siyo kuja na visingizio vya miamala iliyochukuliwa katika Benki ya Mkombozi,” alisema.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mafunzo, Oganaizesheni na Usimamizi, Benson Kigaila, alisema kama Rais Kikwete hatachukua hatua dhidi ya viongozi waliotajwa katika kashfa hii atakuwa ameingia katika mgogoro na bunge ambalo lilitoa maazimio.

 
CHANZO: NIPASHE

2 comments:

Anonymous said...

peoples power nakuaminiyeni.

kweli mwenye akili zake timamu na mpenda haki kwa tabaka la chini atakuwa anaishangilia ccm si kweli lazima na yeye atakuwa anaroho ya KIFISADI FISADI KUWAZA KUNA SIKU ATAPATA NA YEYE ZA KIFISADI FISADI

Anonymous said...

Hivi hii.siri mbona mpaka leo hatujasikia ikiwekwa.hadharani madhali MZEE ARCADO NTAGAZWA umejitokeza hebu tupe huu UTAMU ili MAFISADI waache kuuza SURA MAJUKWAANI