Advertisements

Sunday, December 21, 2014

Kikwete na mambo manne hukumu ya Escrow kesho

Kesho ni siku ya 23 kamili tangu Bunge litoe maazimio manane juu ya uwajibikaji wa wahusika wote katika kashfa ya uchotwaji wa zaidi ya Sh. bilioni 300 kutoka akaunti ya Tegeta Escrow, ambayo Rais Jakaya Kikwete anatarajiwa kutoa maamuzi yake, lakini akikabiliwa na mambo makuu manne.

Katika hukumu ambayo Rais Kikwete ataitoa kesho, suala la maazimio ya Bunge kuhusu kuwawajibisha viongozi waandamizi wa serikali ambao aliwateua, linatarajiwa kupata ufumbuzi.

Hawa ni pamoja na mawaziri, Profesa Sospeter Muhongo (Nishati na Madini); Profesa Anna Tibaijuka (Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi) na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi.

Azimio la Bunge lilitamka wazi kwamba mamlaka ya uteuzi wao ambayo ni Rais Kikwete, atengue nafasi zao kutokana na kuhusika kwao katika kashfa hiyo.

Hadi sasa mtu pekee ambaye amewajibika kwa kujiuzulu ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Fredrick Werema. Alimwandikia Rais barua ya kujiuzulu kwa kile alichodai kutokueleweka kwa ushauri alioutoa kwa serikali juu ya Escrow hivyo kusababisha kuchafuka kwa hali ya hewa.

Jambo la pili linalomkabili Rais Kikwete kesho ni kuchukua maamuzi ambayo yatajibu kiu ya nchi wafadhili zinasosaidia bajeti ya serikali, baada ya kuzuia kutoa takribani Sh. trilioni moja kwa ajili ya kusaidia bajeti ya maendeleo ya mwaka wa fedha wa 2014/15 hadi watakapopata taarifa ya hatua zitakazochukuliwa na serikali juu ya uchotwaji wa fedha za Escrow.

Jambo la tatu linalosubiri hukumu ya Rais Kikwete kesho ni matarajio ya umma ya kutaka kuona uwajibikaji kwa vigogo wote wa serikali waliotajwa katika kashfa hiyo hasa baada ya ripoti ya uchunguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kusema wazi kuwa ndani ya fedha ambazo zilikuwa zimewekwa kwenye Escrow ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), zilikuwako fedha za umma ndiyo maana hata Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilikuwa inadai kiasi cha Sh. bilioni 21 kama kodi, lakini hazikulipwa.

Nne, hotuba ya Rais Kikwete kesho inatazamwa na baadhi ya makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kama tiba ya kejeli na kusakamwa kwa chama chao na Umoja wa Kutetea Katiba ya Wananchi (Ukawa), kwamba serikali yao inahusika na kashfa hiyo.

Matokeo ya uchaguzi wa serikali za mitaa na vitongozi uliofanyika Jumapili iliyopita, yemeonyesha kuzidi kuimarika kwa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) unaoundwa na Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi, huku CCM ikiporomoka kwa kiwango kikubwa.

Baadhi ya wachambuzi wa mambo ya siasa waliozungumza wiki hii juu ya uchanguzi huo, kuimarika kwa Ukawa kumeelezwa kuchangiwa pia na kashfa ya Escrow ambayo imeonekana kuwagusa viongozi serikalini, huku serikali ikitakiwa kuchukua hatua za kuwajibisha wahusika wote.

HISTORIA
Historia inaonyesha kuwa maamuzi magumu yamekuwa yakiwafanywa na marais wa awamu zote zilizokuwa madarakani wakati yanapojitokeza matukio yanayohitaji maamuzi ya viongozi wa nchi wakati wanapozungumza na wazee kwa niaba ya watanzania.

NYERERE
Awamu ya kwanza, Mwalimu Julius Nyerere, mwaka 1983 kupitia mkutano na wazee wa mkoa wa Dar es Salaam, alitangaza kufuta operesheni dhidi ya wahujumu uchumi iliyokuwa inaongozwa na Waziri Mkuu, Edward Sokoine.

Alipoulizwa na wazee wa Dar es Salaam sababu ya kuifuta, alisema “Mimi ndiye dereva ninayejua wapi barabara ina mashimo.”

Mwaka 1977 alitoa maamuzi ya kuanza vita na Idi Amini wa Uganda baada ya kuhutubia wazee wa Dar es Salaam. Mwaka 1967 alitangaza Sera ya Ujamaa na Kujitegemea pamoja na kuanzisha vijiji vya ujamaa.

MWINYI
Kwa kutumia utaratibu wa kukutana na wazee, Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hasan Mwinyi, mwaka 1990 aliwafukuza wanafunzi wote wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (sehemu ya Mlimani) kwa mwaka mmoja wa masomo.

Mwinyi alitetea uamuzi wake na kutaka wananchi wamuhukumu kwa hatua hiyo. Baada ya mkutano huo baadhi ya mikoa ilifanya maandamano ya kuunga mkono maamuzi ya Mwinyi.

MKAPA
Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa (pichani), mwaka 1998 kupitia waraka wake maalumu (White Paper) aliunda Tume ya Jaji Robert Kisanga, ambayo ilitoa mapendekezo ya Muungano wa Serikali tatu, kupunguzwa kwa madaraka ya Rais, ushindi wa Rais uwe kwa zaidi asilimia hamsini ya waliojiandikisha kupiga kura (absolute majority), wagombea binafsi na kuimarisha uhuru wa Mahakama na Bunge.

Baada ya kukabidhiwa ripoti ya tume hiyo, alikutana na wazee wa Dar es Salaam na kuituhumu Tume hiyo kuwa imefanya mambo ambayo haikupewa katika hadidu za rejea.

Akiwa katika hali ya kukasirishwa na ripoti hiyo, Mkapa alisema Muungano utabaki kuwa wa serikali mbili na kupuuza baadhi ya vifungu vya ripoti hiyo.

KIKWETE
Mwaka 2010 akizungumza na wazee wa Dar es Salaam, Rais Kikwete alieleza kuwa yupo tayari kukosa kura za wafanyakazi lakini mshahara wanaotaka serikali haina fedha ya kuwalipa.

“Mgomo huu una lengo la kuongezewa mshahara tu au kuna lingine? Mimi naona mnataka kuninyima kura zenu, basi kama mmepanga hivyo mninyime tu, wengine watanipa.”

Alionya mfanyakazi yeyote atakayegoma atakuwa amejifukuzisha kazi na kukosa haki yake ya msingi katika miaka yake aliyoitumika serikali.

MAAMUZI YANAYOMSUBIRI SASA
Kesho Rais Kikwete atakapoongea na wazee wa Dar es Salaam, anasubiriwa kutoa maamuzi magumu kuhusu sakata la akaunti ya Tegeta Escrow dhidi ya watuhumiwa waliotajwa na Bunge.

Wakati sakata hilo likiwa bichi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Frederick Werema, wiki iliyopita aliandika barua ya kujiuzulu wadhifa wake kwa kueleza kuwa ushauri wake kuhusu akaunti hiyo haukueleweka.

Wengine waliotuhumiwa ni Waziri wa Ardhi, Nyuma na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi.

Sakata hili siyo tu limegusa Watanzania, kwani hata mataifa makubwa duniani ambayo yamekuwa yakitoa msaada kuunga mkono maendeleo, yamesitisha misaada yao hadi muafaka utakapopatikana.

Pia lilisababisha takribani trilioni 1 ambazo zilikuwa zinategemewa kutoka kwa wafadhili hao kutotolewa hadi hapo maamuzi ya serikali yatakapotolewa.

Serikali ya Marekani ilisema haitatoa fedha za changamoto za Milenia (MCC) hadi utekelezaji wa maazimio ya Bunge kuhusu ufisadi katika akaunti ya Escrow ya Sh. bilioni 306 utakapofanyiwa kazi.

MAAZIMIO YA BUNGE
Maazimio kadhaa yalitolewa yakiwamo ya kuwawajibisha kwa kutengua uteuzi wa Profesa Muhongo, Maswi, Profesa Tibaijuka na Jaji Werema ambaye amejiuzulu mwenyewe.

Wengine waliopendekezwa kuvuliwa uongozi wao kwenye kamati za Bunge ni Endrew Chenge (Bajeti), William Ngeleja (Katiba, Sheria na Utawala) na Victor Mwambalaswa (Nishati na Madini). Chenge akipewa Sh. bilioni 1.6 na Ngeleja Sh. milioni 40.2, kwa mujibu wa taarifa ya CAG na PAC.

Pia Bunge hilo liliazimia, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Jeshi la Polisi na vyombo vingine husika vya ulinzi na usalama, vichukue hatua stahiki kwa mujibu wa sheria za nchi kwa watu wote waliotajwa kuhusika na vitendo vyote vya jinai, kuhusu miamala ya akaunti ya Tegeta Escrow, na watu wengine watakaogundulika baada ya uchunguzi mbalimbali unaondelea katika vitendo hivyo vya jinai.

Miongoni mwao ni mmiliki wa kampuni ya PAP, Harbinder Singh Sethi, James Rugemalira wa VIP Engineering Ltd, Jaji Werema, Profesa Muhongo, Maswi, wajumbe wa Bodi ya Tanesco, ambao inasemwa kuwa walihusika kwa namna moja au nyingine kufanikisha kufanyika kwa miamala haramu ya fedha katika akaunti ya Tegeta Escrow kwenda PAP na VIP Engineering and Marketing Ltd.

Kuhusu ushiriki wa majaji katika kashfa hiyo, ni kwamba Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, imeweka utaratibu mahususi wa Tume ya Kijaji ya Uchunguzi kuchunguza tuhuma za utovu wa nidhamu wa maadili dhidi ya Jaji Aloysius Mujulizi na Jaji Profesa Eudes Ruhangisa wa Mahakama Kuu ya Tanzania.

Bunge liliazimia kushughulikia nidhamu ya majaji ambao kwa mujibu wa Katiba hiyo, unamtaka Rais aunde Tume ya Uchunguzi ya Kijaji kuchunguza tuhuma za utovu wa maadili dhidi ya majaji.

Pia Bunge liliazimia serikali iandae na kuwasilisha Muswada wa Marekebisho ya Sheria iliyounda Takukuru kwa lengo la kuanzisha taasisi mahsusi itakayoshughulikia, kupambana na kudhibiti vitendo vya rushwa kubwa, ufisadi, na hujuma za uchumi zinazotishia uhai wa Taifa kiuchumi, kijamii na kisiasa kutokana na kushamiri kwa vitendo hivyo.

Kadhalika Serikali iangalie uwezekano wa kununua mitambo ya kufua umeme ya IPTL na kuimilikisha kwa Tanesco kwa lengo la kuokoa fedha za shirika hilo.

Habari imeandaliwa na Romana Mallya, Beatrice Shayo na Moshi Lusonzo
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

3 comments:

Anonymous said...

Ifike mahali viongozi wetu waache kufanyakazi kwa mazoea. Nini mantiki ya kuhutubia taifa kupitia kwa the so called " Wazee wa Dar es Salaam"?kama hoja ni wazee,then wazee wa Dodoma wangeleta maana zaidi kwakua mji mkuu ni Dodoma.

Anonymous said...

Kasumba ya kuhutubia kupitia wazee wa jiji la Dar ni uongo. Hebu badili dira uhutubie WaTanzania walio wengi ndani na nje ya Tanzania utakuw aumefanya vyema Mheshimiwa>>!!

Anonymous said...

BADO MOVIE INAENDELEA CHANGA LA MACHO CCM OYEEE OYEE CCM JUU JUU ZAID.TUMETHUBUTU TUNAWEZA NA TUNASONGA MBELE HATUJALI LOLOTE SISI NDO SISI.HAAAAAAAAAAAAAAAAAAAA

CCM.