Advertisements

Tuesday, December 2, 2014

Kinana kuwaweka kiti moto mawaziri wanne

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana (pichani), ameahidi kuwaweka kitimoto mawaziri wanne ambao wizara zao zimeonekana kutetereka katika kutimiza majukumu yake kwenye mikoa ya Lindi na Mtwara.

Mawaziri hao ni wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo; Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Abdallah Kigoda; Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe na Waziri wa Nchi, ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Dk. Binilith Mahenge.

Aidha, ametoa mwezi mmoja kuhakikisha kila wizara inatoa majibu sahihi ya kero zinazowakabili wananchi hao. Baadhi ya kero hizo ni kukosekana kwa umeme wa uhakika.
“Nitaenda kuzungumza na mawaziri hawa na kila mmoja ajibu maswali yake na kupatikana kwa ufumbuzi wa kudumu,’’ alisema Kinana

Kinana alitoa kauli hiyo wilayani Mtwara, wakati akizungumza na wakazi wa mkoa wa Mtwara, katika mkutano wa hadhara wakati wa kuhitimisha ziara yake ya siku 16 katika mikoa ya Lindi na Mtwara ya kukagua na kuhimiza utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya mwaka 2010/15.

Alisema, viongozi wana wajibu wa kuwasikiliza wananchi na kutatua kero zinazowakabili, hivyo mawaziri hao wanapaswa kuwajibika kwa kwenda kuzungumza na wananchi na kuweka mambo yao sawa.

“Natoa wiki mbili kwa Mwakyembe atueleze habari ya bandari ya Mtwara na hatua atakazochukua, mwezi mmoja kwa mawaziri wote watatu wahakikishe wamejibu kero ambazo zinasumbua wananchi katika mikoa hii, hatuwezi kuendelea kukaa kimya wakati wananchi wanalalamika kila siku,” alisema Kinana.

“Bandari ipo, lakini cha kushangaza kwa zaidi ya miaka miwili sasa mazao ya korosho yanasafirishwa kwa magari kwenda Dar es Salaam badala ya kupitia bandari ya Mtwara, naomba waziri mwenye dhamana atueleze sababu ikiwa ni pamoja na kuhakikisha mazao yote yanapitia katika bandari hii ili kuongeza mapato ya halmashauri haraka iwezekanavyo,” alisema Kinana.

Kuhusu Waziri wa Nishati na Madini, Kinana alisema anapaswa ajibu sababu za kukosekana kwa umeme wa uhakika katika mikoa ya Lindi na Mtwara wakati gesi inachimbwa katika mkoa wa Mtwara.

“Nilichoshangaa Mtwara na Lindi ni tatizo la umeme, ninaelezwa kuwa umeme uliopo katika mikoa hii ni mwingi, lakini wananchi hawana, gesi inavunwa Mtwara, iweje umeme ukatike kila mara. Waziri mwenye dhamana ajibu hili ni lini umeme utaacha kukatika katika mikoa hii,” alisema Kinana.

Kinana alisema Waziri wa Viwanda na Biashara anapaswa kueleza sababu za wafanya biashara wakubwa wanaoingia nchini kufanya biashara katika mkoa wa Mtwara, lakini wanalipa kodi Dar es Salaam.

“Tunataka majibu kutoka kwa waziri mwenye dhamana, haiwezekani biashara wafanye Mtwara, kodi walipe Manispaa ya Ilala na Kinondoni, Dar es Salaam,” alisema Kinana.
Kadhalika, alimtaka Mahenge kueleza sababu za kumuacha mwekezaji amwage taka zenye kemikali ya sumu katika eneo la katikati ya mji, na kuwa viongozi wanapohoji na kumtaka ahame hakuna hatua zinazochukuliwa.

“Haiwezekani kuwe na taka katikakati ya mji, tena ambazo zina kemikali, halafu viongozi wanapohoji na kutaka aondoke, haondoki na hakuna hatua zinazochukuliwa, lazima kuna mtu anampa jeuri, Waziri ajibu,” alisema Kinana.
CHANZO: NIPASHE

1 comment:

Anonymous said...

Chama Cha Majambazi...