Advertisements

Thursday, December 18, 2014

Mkwasa atoa siri nzito Yanga

Ofisa Mtaalam wa Mafunzo wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF),Boniface Mkwasa.

Ofisa Mtaalam wa Mafunzo wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Mkwasa amesema ana mkataba wa kuinoa Yanga aliopewa na uongozi wa Wanajangwani kabla ya kuchezwa kwa mechi ya 'Nani Mtani Jembe 2'.

Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Jumamosi, Yanga ilipokea kichapo cha mabao 2-0 dhidi ya Simba, matokeo ambayo yamewafukuzisha kazi aliyekuwa Kocha Mkuu, Mbrazil Márcio Máximo na msaidizi wake, Leonardo Neiva.

Akizungumza katika kipindi cha 'Spoti Leo' cha Radio One usiku wa kuamkia jana, Mkwasa aliweka wazi kwamba kabla ya kuchezwa kwa mechi hiyo, alikuwa ameshapewa mkataba wa kuinoa Yanga akiwa kama kocha msaidizi.

"Ni kweli nimeshazungumza na uongozi wa Yanga juu ya kuwa sehemu ya benchi lao la ufundi, walinipa mkataba siku nyingi tu zilizopita," alisema Mkwasa.


Hata hivyo, Mkwasa anayesifika kwa kufundisha soka la pasi fupi fupi, hakuweka wazi muda wa mkataba wake mpya na Yanga utakaovunja ajira yake na TFF.

Baada ya kumtema Máximo, uongozi wa Yanga umemrejesha Mholanzi Hans van der Pluijm na Mkwasa ambao walikuwa pamoja katika benchi la ufundi la timu hiyo ya Jangwani kabla ya kutimkia Saudi Arabia lakini nako walifungasha virago kutokana na kile walichodai kuingiliwa majukumu yao na kutolipwa kwa wakati na Klabu ya Shaola.

Ajira ya Mkwasa Yanga, ni miongoni mwa sababu kubwa za kufungashiwa virago kwa Máximo kwani Mbrazil huyo hakuwa tayari Mbrazil mwenzake (Neiva) atemwe na kumpokea kocha huyo wa zamani wa Ruvu Shooting na Twiga Stars baada ya kutakiwa kufanya hivyo.

Kabla ya ujio wa Máximo Yanga, Pluijm na Mkwasa waliiongoza timu hiyo katika mechi 19 wakishinda 11, sare sita na vipigo viwili dhidi ya Mgambo Shooting (2-1) na Al Ahly (1-0).

Pluijm na Mkwasa walirithi mikoba ya Mholanzi Ernie Brandts na msaidizi wake mzawa Felix Minziro waliotimuliwa muda mfupi baada ya Yanga kufungwa mabao 3-1 dhidi ya Simba katika mechi ya 'Nani Mtani Jembe' kwenye Uwanja wa Taifa Desemba 21, mwaka jana.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: