ANGALIA LIVE NEWS

Friday, December 26, 2014

SIMBA YAMSHITAKI MLIBERIA WA YANGA

Mshambuliaji mpya wa Yanga, Kpah Sherman.

Na Mwandishi Wetu
YANGA inatarajiwa kujitupa uwanjani keshokutwa Jumapili kukipiga dhidi ya Azam FC katika mechi ya Ligi Kuu Bara, lakini upande wa pili ni kuwa wapinzani wa Wanajangwani hao wanajiandaa kumshitaki mshambuliaji mpya wa Yanga, Kpah Sherman raia wa Liberia ambaye anatuhumiwa kutoroka kazini nchini Cyprus.

Awali gazeti hili liliripoti juu ya straika huyo ambaye amekuwa kipenzi cha mashabiki wengi wa Yanga ndani ya muda mfupi na sasa Simba inatajwa kutaka kufungua mashitaka ya kupinga mchezaji huyo kuichezea Yanga kwa kile kilichoelezwa kuwa hajakamilisha taratibu za kuichezea timu hiyo.

“Ndiyo tunataka kumzuia huyo mshambuliaji kwa kuwa tumeambiwa hajakamilisha taratibu za uhamisho, tumeshapewa data zote, hivyo ndani ya muda wowote kuanzia sasa (jana) tutapeleka malalamiko yetu kwa TFF (Shirikisho la Soka Tanzania),” alisema mtu kutoka ndani ya uongozi wa Simba na kuendelea:
“Tunataka mechi ya Jumapili asicheze na hata kama akicheza, kama tukifuatilia kisha tukajua usajili wake haukuwa sahihi basi Yanga wajiandae kupokwa pointi baadaye.”

Uongozi wa Klabu ya Centikaya TSK ya Cyprus kupitia kwa Rais wake, Meric Erulku, ulilithibitishia gazeti hili na kudai kuwa Sherman aliondoka nchini humo akidai ana matatizo ya kifamilia na wanashangaa kusikia amejiunga na klabu ya Tanzania, ambapo nao wameanza mipango ya kufungua mashitaka kwenye Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa).

Sherman alitua Yanga akitokea Cyprus lakini hati yake ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) ilitokea nchini Liberia.Alipoulizwa na gazeti hili juu ya sakata hilo la ITC, Mkurugenzi wa Mashindano wa TFF, Boniface Wambura alifunguka kama ifuatavyo:

“Yule mchezaji alikuwa anacheza Liberia, lakini baadaye akahamia Cyprus ambapo alikuwa akicheza kwa mkopo, hivyo ITC yake ilitolewa Liberia kwa kuwa ndipo klabu yake ilipo, siyo ile ya mkopo aliyokuwa akiichezea, kwa ufafanuzi zaidi mnaweza kuuliza Chama cha Soka cha Liberia kuhusiana na wao kwa nini walitoa ITC ya mchezaji huyo.” 

Mapema wiki hii, Rais wa Centikaya TSK, Meric Erulku alisema: “Kweli tuna mkataba naye (Sherman), haujaisha na haujavunjwa. Pia hatujalipwa na kulikuwa na mpango wa kwenda Fifa, lakini meneja wake amezungumza nasi na tunaendelea na mazungumzo baadaye nitawapa ripoti kamili.
”credit:GPL

No comments: