ANGALIA LIVE NEWS

Monday, December 22, 2014

UANDIKISHAJI BVR WAISHA KWA CHANGAMOTO

Mwandikishaji wa Vitambulisho vya uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura, Hawa Mpole akimsaidia, Zainabu Liwena jinsi ya kuchukua alama za vidole katika kituo cha Bunju A, Dar es Salaam jana, ikiwa ni sehemu ya majaribio  ya kutumia mashine za teknolojia ya elektroniki (BVR). Picha na Venance Nestory
Dar es Salaam. Wakati majaribio ya uandikishaji wa wapigakura kwa kutumia mfumo mpya wa BVR yakiisha leo, wananchi wengi wameshindwa kujiandikisha kutokana na mpango wenyewe kusuasua.
Kutokana na hali hiyo, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Julius Malaba amesema kuna uwezekano kazi hiyo ikafanyika tena mwakani kwa nchi nzima.
“Haya ni majaribio tu, changamoto tulizopata ndizo tutakazozifanyia kazi ili mfumo huu ufanye kazi kama ilivyokusudiwa,” alisema Malaba.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, baadhi ya wananchi waliojitokeza kujiandikisha, walisema muda uliowekwa ni mdogo na kushauri kama ingefanyika kwa wiki mbili.
Mmoja wa wananchi hao, Rajabu Mohamed alisema kila kituo kina mwandishi mmoja ambaye anatumia dakika 15 kuchukua maelezo ya watu wanaoingia kwa ajili ya kujiandikisha.
“Niko hapa tangu Ijumaa, sijamwona mtu wa kuchukua maelezo ya watu na hapohapo tunaambiwa kuwa mwisho ni leo,” alisema Mohamed.
Aloyce Mwanjile alisema ni lazima kuwepo na mashine zaidi ya tano kila kituo ili kazi hiyo ifanyike haraka. “Elimu nayo ni muhimu kwa wananchi, wengi hawana taarifa na mfumo huu mpya wa uandikishaji,” alisema Mwanjile.
Majaribio hayo yamefanyika katika Jimbo la Kawe, Dar es Salaam, Kilombero mkoani Morogoro na Katavi. Mwananchi

No comments: