ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, December 10, 2014

UNASEMA WA NINI, WENZAKO WANAJIULIZA WATAMPATA LINI?


HUU ni msemo maarufu sana katika jamii yetu. Umekuwa ukitumika kama moja ya misemo ya kupeana faraja baina ya watu, kwani mahangaiko na mizunguko ya maisha inawafanya watu wengine kukata tamaa mapema, wakiamini kuwa wao hawana thamani.

Ndiyo, kuna watu wengi wanaumizwa sana na mapenzi, wakubwa kwa wadogo. Wapo wanaoumia sana wakiwa katika ndoa zao, kinachowaumiza ni nyenendo zenye kutia shaka za wenza wao. Siyo kwamba wana ushahidi wa kinachofanywa nao, isipokuwa roho zao zimekuwa hazina amani wakiamini kuwa wanafanyiwa michepuko.

Waliopenda sana (kama wapo) hupata taabu zaidi kama wenza wao wakiwa na nyendo za mashaka. Hujiona kama wenye mikosi, ambao upendo wao unajibiwa kwa taabu na mateso ya moyo pasipo na sababu. Hufikia wakati wakajiona kama wenye kasoro katika maumbile yao.

Ndiyo, wapo akina baba wenye maumbile madogo, hawa huwa wanyonge sana linapokuja suala la tendo la ndoa, hujiona kama wasio na thamani, hasa kama mwenza wake atakuwa na maneno au vitendo vinavyoashiria dharau. Chukulia kwa mfano baba atamfuata mama na kumuomba ule mchezo, halafu mama atoe jibu kama ‘usumbufu tu, mtu mwenyewe..’

Na hata akina mama pia, nao wana matatizo yao ya kimaumbile, wengine makubwa, wengine hutoa harufu na vitu vingine kama hivyo. Hawa nao huwa hawana furaha sana linapokuja suala la uhusiano wao wa kimapenzi. Kama wenza wao watakuwa ni wenye nyodo na dharau, daima huwa ni watu wa kulia, kwa vile wanaamini wanaadhibiwa kutokana na udhaifu wa maumbile yao!

Ukiachana na mambo haya ya maumbile, ipo pia misuguano inayodhorotesha uhusiano wa watu kutokana na tabia za wahusika. Tabia moja ya mtu, yenye kumtia dosari, huweza kutumiwa na mwenza wake, kumuadhibu na hivyo kumletea mateso katika maisha yake.

Kama mwanaume atakuwa na tabia ya ulevi wa kupindukia, unaoambatana na vitendo vya kijinga, kama kuvua nguo au kujikojolea hadharani, kwa vyovyote, hatakuwa na sauti kwa mke wake wakati wa mjadala wa maana katika familia.

Wote hawa, kwa ujumla wao, hawana sababu ya kuwa wanyonge kwa vile kila jambo linawezekana na furaha ikaja kiasi cha kutoamini. Mimi ni mmoja wa watu ambao kukata tamaa halijawahi kuwa jambo linalolipa nafasi. Ninaishi katika kujifunza na ni mwepesi kukiri makosa yangu kwa nia njema ya kujifunza.

Zipo tabia zinazoweza kubadilishwa, siyo na mtu mwingine lakini na wewe mwenyewe. Na kwa vyovyote, unajua ni jambo gani ambalo linamkera mwenzio. Hili una uwezo nalo kama kweli unahitaji maisha yenye faraja katika uhusiano wako.

Ukiona hamuendani, licha ya jitihada zako za kujishusha, usikate tamaa, nafasi yako iko kwa mtu mwingine sehemu inakusubiri. Usiogope kuonekana hujatulia, kuna mtu alioa na kuacha wanawake sita, hadi alipokuja kumpata wa saba, chaguo sahihi katika umri wa miaka 50!

Hata wewe mwanamke, usijilize, eti kila mwanaume au mvulana unayekuwa naye baada ya muda mfupi mnatengana. Ukajiona mtu mwenye mikosi.

Hapa lazima nieleweke, kama wewe siyo chanzo cha tatizo, basi nikupe moyo kuwa hujachelewa, kwa sababu maisha ni kama gwaride, afande akisema nyuma geuka, wa kwanza anakuwa wa mwisho huku aliyekuwa wa mwisho anakuwa wa kwanza!

Wanaweza kukutangulia kwa kila kitu, lakini siku yako ikifika, unaishi kwa raha na amani kuliko miaka mingi ya watangulizi wako ambao wanalia kila siku!

GPL

No comments: