ANGALIA LIVE NEWS

Friday, January 23, 2015

TFF yatekeleza maagizo ya Yanga

Yamfungia refa aliyeachia Tambwe akabwe koo
Wachezaji wa Ruvu Shooting na Yanga wakigombana wakati wa mchezo uliozikutanisha timu hizo mwishoni mwa wiki.

Katika kile kinachoonekana kama kuendeshwa na Yanga, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limemfungia refa Mohamed Teofile kuchezesha mechi za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) msimu huu.

Jana mchana NIPASHE ilipata taarifa kutoka ndani ya TFF zikieleza kuwa refa huyo ameondolewa katika ratiba ya waamuzi wa msimu huu, taarifa ambazo baadaye zilithibitishwa na kamati husika.

Akiwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza jana jioni akifuatilia mechi ya kimataifa ya kirafiki ya Taifa Stars Maboresho dhidi ya Rwanda, Mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi ya TFF, Salum Chama alithibitisha kufungiwa kwa Teofile.

"Ni kweli tumemwondoa kwenye ratiba ya marefa wa msimu huu Mohamed Teofile kwa sababu hakuimudu mechi iliyopita ya Yanga dhidi ya Ruvu Shooting. Ni mwamuzi huyo tu ambaye tumemchukulia hatua hadi sasa," alisema Chama. Katika mechi hiyo Teofile alisaidiwa na Michael Mkongwa na Yusuph Sekile wakati mezani alikuwapo Kenneth Mapunda.

Uamuzi huo umetoka ikiwa ni saa chache baada ya uongozi wa Yanga kutoa tamko la kuishinikiza TFF kuwafungia marefa waliochezesha mechi na kuanika hadharani ripoti ya kamisaa wa mechi hiyo iliyomalizika kwa suluhu.

Katika mkutano na waandishi wa habari kwenye ofisi za Makao Makuu ya Yanga jijini juzi, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Yanga, Jerry Muro alitoa masharti manne kwa TFF kuchukua hatua kali dhidi ya wachezaji wa Ruvu Shooting, kuwafungia marefa na maofisa wa Ruvu Shooting pamoja na kutowapanga tena waamuzi husika katika mechi zinazohusisha kikosi cha Yanga.

Katika kinachoonekana kuwa ni muingiliano wa matukio, ripoti ya mechi ya Yanga imejadiliwa kwa muda mfupi na kutolewa maamuzi ilhali Kamati ya Waamuzi ya TFF ilikaa kupitia mechi 49 za raundi saba za mwanzo za msimu huu wa VPL baada ya kusimama kwa ligi hiyo Novemba Mosi, mwaka jana.

KUNG'OLEWA VITI TAIFA
Teofile ambaye ameponzwa na kile kinachoonekana kuchezeana undava kati ya mfungaji bora wa VPL msimu uliopita, Mrundi Amisi Tambwe wa Yanga na George Michael wa Ruvu Shooting katika mechi yao ya Jumamosi, amekuwa na historia ya kukumbana na vurugu katika mechi anazopangwa kuchezesha.

Oktoba 31, 2013 refa huyo kutoka Morogoro alichezesha mechi ya raundi ya kwanza ya VPL msimu wa 2013/14 ambayo ilimalizika kwa sare ya 1-1 huku kukitokea vurugu kubwa zilizosababisha kung'olewa kwa viti vya Uwanja wa Taifa na baadhi ya mashabiki wa Simba.

Tukio hilo lilitokea mara tu baada ya beki wa zamani wa Simba, Salum Kanoni kuisawazishia Kagera Sugar kwa penalti iliyotolewa na refa huyo katika dakika ya mwisho ya mchezo baada ya kiungo George Kavilla wa Kagera kupenyeza pasi ndefu kwa Daudi Jumanne aliyekuwa katikati ya mabeki wa Simba ndani ya boksi kisha kukwatuliwa na beki wa kati Mganda Joseph Owino.

Wiki moja baada ya mechi hiyo Teofile alikamatwa na polisi akiwa kwenye nyumba ya kulala wageni maeneo ya Mji Mpya mkoani Morogoro akidaiwa kukutwa na mwanafunzi wa kike wa kidato cha pili. Baadaye iliripotiwa kuwa mwamuzi huyo aliachiwa baada ya kudhamaniwa.
CHANZO: NIPASHE

No comments: