Advertisements

Friday, February 27, 2015

Ajali yaua watatu, nyingine yajeruhi 21

Askari wa Kikosi cha Zimamoto, wakizima moto baada ya lori la mafuta kupinduka kisha kuwaka moto na kusababisha watu watatu kufariki dunia eneo la Wedi, Kijiji cha Maseyu, Tarafa ya Mikese katika Barabara Kuu ya Morogoro-Dar es Salaam jana. Picha na Juma Mtanda.

Morogoro\Dar. Watu watatu wamefariki dunia papo hapo baada ya lori la mafuta walilokuwa wamepanda kupinduka na kuwaka moto eneo la Wedi, katika Kijiji cha Maseyu mkoani Morogoro, huku wengine 21 wakijeruhiwa katika ajali nyingine iliyotokea Kimara, Dar es Salaam.
Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho, Juma Kipile alisema jana kuwa ajali ya lori ilitokea saa 11.30 alfajiri katika barabara kuu ya Dar es Salaam-Morogoro.
Waliofariki dunia ni dereva wa lori la Kampuni ya Petro Africa ya Dar es Salaam, Ahmed Dilia, utingo wake, David Omela na mtu mwingine aliyefahamika kwa jina moja la Ahmed.
Kipile alisema baada ya lori hilo kupinduka, ulifuka moshi na kusababisha barabara hiyo kutopitika kwa saa mbili.
“Nilipigiwa simu na mwenyekiti wa kitongoji akinijulisha kutokea kwa ajali hii.” alisema
Mkaguzi Msaidizi wa Kikosi cha Zimamoto Morogoro, Hamad Dadi alisema walifika eneo hilo saa mbili baada ya kutokea ajali.
Alisema walibaini kuwa kulikuwa na watu waliokandamizwa na tenki la mafuta.
Dadi alisema baada ya kazi ya kuzima moto na kunyanyua tenki la mafuta kukamilika, waliiona miili ya watu hao ikiwa imeungua.
Mmoja wa wafanyakazi wa kampuni hiyo, Farhan Yusuph aliyewatambua marehemu hao alisema waliondoka katika ofisi za kampuni hiyo kuelekea Mwanza na lori hilo lililokuwa limebeba lita 37,000 za mafuta ya dizeli.
Katika tukio lililotokea Dar es Salaam, watu 21 walijeruhiwa baada ya daladala walilopanda kupinduka katika eneo la Kimara Suka wakati dereva akijaribu kuikwepa bodaboda iliyokuwa katika mwendo kasi.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura alithibitisha tukio hilo.
“Ajali imetokea leo (jana) mchana katika eneo la Kimara. Hakuna aliyefariki dunia isipokuwa wapo waliopata majeraha makubwa. Hao wamepelekwa Hospitali ya Mwananyamala,” alisema.
Mwananchi

No comments: