
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete alisema kuwa atakayekuwa mgombea wake wa urais baadaye mwaka huu bado hajajitokeza mpaka sasa.
Akihutubia Jumapili katika sherehe za miaka 38 ya kuzaliwa kwa chama hicho katika Uwanja wa Majimaji Mjini Songea mkoani Ruvuma, Rais alisema:
“Wapo watu wenye sifa zote za urais lakini hawajitokezi na hata wakiambiwa kuwa wanaweza husema kuwa hawajajiandaa. Hawa ndiyo tunaowahitaji kwa kuwa wanahitaji kukumbushwa.”
Katika tukio jingine, kundi la watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi walivamia kituo kidogo cha Polisi cha Mngeta, Kilombero na kuiba bunduki aina ya SMG ikiwa na risasi 30.
Kituo hicho ni cha tatu kuvamiwa mwaka huu baada ya Kituo Kikuu cha Polisi Rufiji mkoani Pwani na Bukombe kuvamiwa na majambazi na kuua polisi wawili na kupora bunduki saba na risasi 60.
Jumanne wiki iliyopita, Rais wa Shirikisho la Ujerumani, Joachim Gauck aliwasili nchini kwa ziara ya kikazi na kupokelewa na mwenyeji wake, Rais Jakaya Kikwete.
Pia, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ilisema imeanza kumhoji na kumchunguza mmiliki mwenza wa Kampuni ya Kufua Umeme ya Independent Power Tanzania Ltd (IPTL), James Rugemalira.
Akizungumza na gazeti hili, Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk Edward Hoseah alisema, vigogo wote waliohusika katika sakata la uchotaji fedha katika Akaunti ya Tegeta Escrow ya Benki Kuu (BoT) wanachunguzwa akiwamo Rugemalira.
Wiki hii, Ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa nchini ilitoa siku 80 kuanzia Jumanne wiki iliyopita kwa uongozi wa Chama cha Tanzania Labour Party (TLP) kuhakikisha unafanya uchaguzi wa kuwapata viongozi wapya.
Hatua hiyo, ilifikiwa baada ya wanachama wa chama hicho kupeleka malalamiko yao kwa msajili wakidai kuwa uongozi wa mwenyekiti wa chama hicho, Augustine Mrema umefika kikomo.
Akizungumza baada ya kusikiliza malalamiko hayo, Msaidizi wa Msajili wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza alisema ingawa uchaguzi huo ulichelewa kufanyika kutokana na hali ya afya ya mwenyekiti wao, aliutaka uongozi kuhakikisha unafanya uchaguzi kabla ya Aprili 26, 2015.
Kutoka Bungeni Dodoma, Serikali ilitangaza kuuchomoa muswaada wa kuanzisha Mahakama ya Kadhi uliokuwa uwasilishwe jengoni humo ili yafikiwe maridhiano kwanza.
Wakati Serikali ikieleza uamuzi huo, Taasisi 11 za Jumuiya na Taasisi za Kiislamu zilitangaza kuwahamasisha wanajumuiya wake kususia Kura ya Maoni ya Katiba Mpya hadi watakapopata uhakika wa mahakama ya kadhi yenye meno.
Katika taarifa nyingine, Taasisi ya Utafiti ya Repoa ilizindua ripoti kuhusu rushwa iliyoonyesha kuwa Takukuru ni moja ya taasisi zinazotajwa kushika nafasi za juu kwa kupokea rushwa nchini.
Utafiti huo ulioitwa, ‘Baada ya muongo mmoja wa kupambana na rushwa, tumepiga hatua kiasi gani?’ ulibaini kuwa asilimia 64 ya wananchi waliohojiwa walisema rushwa inazidi kuongezeka.
Mtafiti kutoka Repoa, Rose Aiko alisema asilimia 29 ya wananchi waliohojiwa walisema Takukuru wanapokea rushwa na hivyo kuifanya taasisi hiyo kushika nafasi ya nne ikitanguliwa na Polisi (50%), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) (37%) na majaji na mahakimu (36%).
Mwananchi
No comments:
Post a Comment