Rais Kikwete aliyasema hayo jana Ikulu jijini Dar es Salaam, baada ya kuwaeleza waandishi wa habari walichozungumza faragha na mgeni wake, Rais wa Ujerumani, Joachim Gauck, na baadaye kuja mbele ya waandishi wa habari na kujibu maswali mbalimbali.
Akijibu swali la waandishi wa habari wa Ujerumani, aliyetaka kujua hali ya usalama na haki za binadamu nchini ikoje hasa ikizingatiwa Januari 27, mwaka huu, kulikuwa purukushani kati ya polisi na wafuasi wa Cuf, na kutumia nguvu kubwa katika kuwadhibiti.
Akijibu swali hilo, Rais Kikwete alisema zipo sheria, kanuni na taratibu zinazoongoza watu wanapotaka kuandamana au kufanya mikutano ya hadhara na kwamba ni lazima zifuatwe kwa kupata kibali cha Polisi.
“Huwezi kuamka asubuhi na kuanza kuandamana au kufanya mkutano wa hadhara ni lazima sheria na taratibu zilizopo zifuatwe…vyama vya upinzani vimekuwa vikifanya mikutano na maandamano bila kubugudhiwa iwapo wamefuata sheria zilizopo,” alisema na kuongeza:
“Usipokuwa na kibali Polisi hawawezi kukuruhusu uandamane au ufanye mkutano.”
Kauli ya Kikwete imekuja siku mbili tangu Mwenyekiti wa Cuf, Prof. Ibrahim Lipumba (pichani), kuwaeleza waandishi wa habari kuwa ameanza taratibu za kuonana na kiongozi huyo ili kujadiliana namna ya kuweka utaratibu wa kutenda haki kwa vyama vya siasa dhidi ya Jeshi la Polisi kuelekea uchaguzi mkuu, Oktoba, mwaka huu.
NIPASHE iliwasiliana na Prof. Lipumba kujua hatua aliyofikia katika kutafuta nafasi ya kuonana na Rais, ambaye alisema amepeleka taarifa kwa njia ya mtandao (Info line), na anasubiri jibu na kwamba amehofia kupeleka taarifa kwa barua kwa kuwa kuna uwezekano wa barua kufunguliwa kabla ya kumfikia.
Hata hivyo, baada ya msimamo huo wa Rais Kikwete, Prof. Lipumba alisema watawasilisha kilio cha vitendo vya uonevu vinavyofanywa na Polisi kwa Rais Gauck.
Aidha, Rais Kikwete alizungumzia pia uhuru wa vyombo vya habari akieleza kuwa serikali inaheshimu uhuru wa vyombo vya habari na ni nchi yenye vyombo vingi ikiwamo magazeti, runinga na radio zinazomilikiwa na watu binafsi na kukiwa na vichache vinavyomilikiwa na serikali.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment